NA FRESHA KINASA
SHIRIKA la Victoria Farming and Fishing Organization (VIFAFIO) lililopo Musoma Mkoani Mara limetoa mafunzo kwa wajumbe ngazi ya kata wa Kamati ya Mpango kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) kutoka Kata ya Bwasi na Bukumi katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma mkoani Mara.

Mafunzo hayo yamefanyika Oktoba 5, 2022 katika Kijiji cha Busekera Kata ya Bukumi yakilenga kuwajengea uelewa na mbinu madhubuti za utekelezaji wa majukumu yao. Ili wawajibike kikamilifu kufanikisha malengo ya (MTAKUWWA).

Pia Majura amewasisitiza kuandaa na kuunganisha shughuli za mpango katika ngazi za vijiji, kuratibu upatikanaji wa rasimali kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa mpango kwenye vijiji na vitongoji, kuhamasisha utekelezaji wa mapango na kutoa taarifa za robo mwaka kwa ngazi ya halmashauri, kufuatilia na kuthimini utekelezaji wa mpango Katika vijiji, kuwezesha uibuaji, uandaaji na ujumuishaji wa afua na bajeti za utekelezaji wa mpango wa kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya Wanawake na watoto.

Ameongeza kuwa, mpango huo ni muhimu katika kueleza wadau wa utekelezaji wa (MTAKUWWA) namna ya kuandaa kamati za kusimamia utekelezaji wa mapango katika ngazi zote na kuleta uwiano katika uanzishwaji na uendeshwaji wa kamati.
Aidha amewataka wajumbe wa kamati hizo Kuzingatia afua za 'MTAKUWWA' ikiwemo suala la kuimarisha uchumi wa kaya, mazingira salama shuleni na stadi za maisha, utoaji huduma kwa waathirika wa ukatili, malezi, kuimarisha Mahusiano na kuziwezesha familia, utekelezaji na usimamizi wa sheria, uratibu, ufuatiaji na tathimini pamoja na suala la mila na desturi.

Ameongeza kuwa, mradi huo unatarajia kuleta matokeo ikiwemo kuwafanya Wanawake na watoto wachukue hatua kwa kuripoti vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa kwa mamlaka za serikali na Jamii iwe na uwezo wa kudhibiti vitendo vya ukatili wa Kijinsia sambba na kuimarisha mfumo bora katika kamati za Vijiji na kata zinazohusika na kupinga vitendo hivyo.
Awali Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Vincent John akifungua mafunzo hayo amelishukuru Shirika la VIFAFIO kwa kutekeleza mradi wa kupambana na vitendo vya ukatili maeneo ya mialo ambapo amesema Halmashauri hiyo shughuli za uvuvi zinafanyika, hivyo kupitia mradi huo utasaidia mapambano ya vitendo hivyo na kuimarisha usawa wa kijinsia kwa maendeleo ya jamii na taifa pia.
Kamati ya MTAKUWWA ngazi ya kata inaundwa na Afisa maendeleo ya jamii kata, tabibu, Afisa Ustawi wa Jamii, Polisi, Hakimu, mawakili wa azaki,Mratibu wa Elimu, Viongozi wa dini, vikundi vya watu wasiojiweza, watu wenye ulemavu, watu mashuhuri na wawakikishi wawili wa mabaraza ya watoto.