Vyuo vikuu vyatakiwa kufanya tafiti namna elimu itakavyokidhi matakwa ya sasa kwa Watanzania

NA MWANDISHI WETU

VYUO vikuu nchini vimetakiwa kufanya tafiti, zikiwemo tafiti kuhusu namna ambavyo elimu ya juu itakidhi matakwa ya sasa ya jamii ya kitanzania.
Agizo hilo limetolewa jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt.Francis Michael wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya Miaka 60 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na miaka 17 ya Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE).
Amesema, ni vizuri kufanya uchunguzi wa kina kuhusu mwelekeo wa sasa wa kitaifa na kimataifa na kisha kutafakari ni namna gani vyuo vyetu vitawawezesha wahitimu kuendana na mwelekeo huo.
“Kama mnavyofahamu, kumekuwa na mjadala kuhusu uwezo wa kujiajiri miongoni mwa wahitimu wa vyuo vikuu, mjadala ambao kwa namna moja au nyingine umezua maswali kuhusu mitaala ya elimu nchini. 

"Kutokana na mjadala huu, Rais Samia Suluhu Hassan alizungumzia umuhimu wa kuipitia upya mitaala ili iendane na matakwa ya ulimwengu wa sasa, ikiwemo uwezo wa wahitimu kujiajiri na kuwa wabunifu, hivyo ni muhimu kutafakari ni kwa namna gani DUCE na vyuo vingine vinachangia katika jitihada hizi,"amesema Dkt. Michael.
Aidha, amesema kama ilivyo kwenye Vyuo vingine, Serikali kupitia Wizara ya Elimu, itaendelea kutoa ushirikiano kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam katika dhamira yake ya kuendelea kutoa walimu bora, ambao wanahitajika ili kufikia lengo la kutoa elimu bora kwa watanzania wote.
Kwa upande wake, Rasi wa Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam, Prof. Stephen Maluka amesema Chuo hicho katika kipindi cha miaka 17 tangu kuanzishwa kwake kimepata mafanikio makubwa. Akitaja baadhi ya mafanikio hayo ni kuongezeka kwa wahitimu kutoka 522 Mwaka 2008 hadi kufikia 16,330 Mwaka 2021, programu kutoka Digirii za awali Nne hadi Tano.

Prof. Maluka ameishukuru Wizara ya elimu kwa kukisaidia Chuo kusomesha watumishi, ujenzi na upanuzi wa miundombinu kupitia miradi yake mbalimbali hivyo kutatua changamoto ya miundombinu katika chuo hicho na kupunguza gharana za kusomesha watumishi hadi kufikia ngazi ya shahada ya uzamivu.
Aidha, ameishukuru Serikali, kwa kukiletea Chuo hicho Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (Higher Education for Economic Transformation – HEET Project) kwani wameweza kusomesha watumishi wanataaluma katika vyuo maarufu duniani katika ngazi ya umahiri na uzamivu.
Pia, kupitia mradi huo, Chuo hiki kinatarajia kutumia zaidi ya Shilingi Bilioni Kumi (Dola za Kimarekani 4,357,827.61) kwa ajili ya kuendelea kufanya ukarabati wa miundombinu na kujenga majengo na miundombinu mingine mipya.
Maadhimisho ya miaka 60 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na miaka 17 ya Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam yamepambwa na maonesho ya kazi mbalimbali za utafiti na uvumbuzi zilizofanywa na wanataaluma wa chuo hicho.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news