WADAU:Wapo akina baba wanaopigwa makofi, wanaonyimwa chakula, hawafuliwi nguo na vitendo vingine haya si siri tena, toeni taarifa

NA DIRAMAKINI

WANAUME wametakiwa kutoa taarifa katika vyombo husika kuhusu vitendo vya ukatili dhidi yao vinavyofanywa na wanawake badala ya kukaa kimya kama ilivyo sasa.
Wito huo umetolewa mjini Musoma Septemba 30, 2022 na Sista Annunciata Chacha kutoka Shirika la Jipe Moyo la mjini Musoma kwenye mafunzo kwa wajumbe wa kamati ya Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (Mtakuwwa), mafunzo yaliyondaliwa na Manispaa ya Musoma na kufadhiliwa na Taasisi ya Social Action Trust Fund (SATF).

Amesema kuwa, vitendo vya ukatili dhidi ya wanaume katika jamii vipo ila wanaume wamekuwa wakiona aibu kuvitolea taarifa ili hatua zichukuliwe na kwamba umefika wakati wanaume wanatakiwa kutoa taarifa ili wadau katika kupinga ukatili waweze kupaza sauti kwa pamoja kama ilivyo kwenye vitendo vya aina hiyo dhidi yawanawake na watoto.

"Wapo akina baba wanaopigwa makofi, wanaonyimwa chakula, ambao hawafuliwi nguo na vitendo vingine vingi hili jambo sio siri tena, hebu jitokezeni na mtoe taarifa ili hatua zichukuliwe,"amesema.

Akizungumza kuhusu mafunzo hayo, mratibu wa mradi wa elimu kutoka SATF, Helena Chikomo amesema katika kukabiliana na matukio ya ukatili kwa watoto taasisi yake imetoa ufadhili wa mafunzo hayo ili kuwajengea uwezo wajumbe wa kamati za Mtakuwwa kuweza kutekeleza majukumu yao ipasavyo katika kuzuia vitendo vya ukatili kwa watoto vitendo ambavyo kwa namna moja ama nyingine vimekuwa pia chanzo cha watoto kushindwa kufikia ndoto zao ikiwemo ndoto ya elimu.
Amesema kuwa, dhamira kuu ya SATF ni kuwawezesha vijana waliopo katika mazingira magumu kuchangia katika maendeleo ya taifa ambapo ili kufikia malengo hayo yapo mambo kadhaa yanayotakiwa kufanyika ili vijana hao waweze kupata fursa ya kushiriki katika ujenzi wa taifa ikiwa ni pamoja na kutengeneza mazingira wezeshi kwa watoto walio katika mazingira magumu ili waweze kupata fursa.

Helena amesema kuwa wapo watoto ambao wamekuwa wakilazimishwa kuolewa katika umri mdogo hivyo kamati hizo zikiweza kutekeleza majukumu yao vema zitaweza kuzuia vitendo vya aina hiyo kwa kuwaibua wazazi na walezi wenye tabia hizo hivyo hatua kuchukuliwa mapema kuwanusuru watoto hao.

"Kushiriki katika maendeleo ya nchi kunahitaji wahusika kuwa na ujuzi utakaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa lakini haya yote yanawezekana endapo hawa watoto kutoka mazingira magumu hawatakuwa na kikwazo katika kuzipata haki zao kubwa ikiwa ni haki ya elimu na ilikufanikisha hili lazima kuwe na ushirikiano wa wadau kama wajumbe wa Mtakuwwa,"amesema.

Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Musoma, Jacqueline Wanzagi amesema kuwa kumekuwepo na matukio ya ukatili yanayotokea katika jamii lakini matukio hayo hayatolewi taarifa.

"Hapa tutajifunza namna ya kutoa elimu kuzuia ukatili dhidi ya watoto vile vile tutajifunza namna ya kutoa taarifa sambamba na kuelimishwa kwa kina zaidi nini maana ya ukatili kwa hiyo tukitoka hapa naamini kutakuwa na mabadiliko katika maeneo yetu,"amesema.

Jumla ya wanakatamati 160 kutoka katika kata kumi za Manispaa ya Musoma ambazo ni Mwisenge, Makoko, Nyakato, Mshikamano na Buhare nyingine ni Bweri, Kwangwa, Mwigobero, Rwamlimi na Kitaji wanashiriki mafunzo hayo ya siku mbili.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news