NA MUNIR SHEMWETA-WANMM
NAIBU
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega ametaka wafugaji kumilikishwa
ardhi na kupatiwa hati kwa ajili ya shughuli za ufugaji.
Naibu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akifurahia na wananchi
wa Kitongoji cha Ikanka katika Kijiji cha Itumba wilayani Ileje Mkoa wa
Songwe wakati Kamati ya Mawaziri Nane inayoshughulikia migogoro ya
Matumizi ya Ardhi katika vijiji 975 ilipotembelea kitongoji hicho.
(Picha na WANMM).
Ametoa kauli hiyo Oktoba 24, 2022
mkoani Songwe kwa nyakati tofauti wakati Kamati ya Mawaziri nane wa
Wizara za Kisekta inayoshughulikia migogoro ya matumizi ya ardhi katika
vijiji 975 ilipozungumza na uongozi wa Mkoa wa Songwe pamoja na
kutembelea wananchi wa Kitongoji cha Ikanka Kijiji cha Itumba wilayani
Ileje.
Amesema, wakati ikisisitizwa ardhi inayomegwa kwenye
maeneo mbalimbali ya hifadhi kupangiwa mipango ya matumizi ni wakati
muafaka sasa kwa ardhi hiyo nayo kutolewa kwa shughuli za mifugo na
wamiliki wake kupatiwa hati.
Naibu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi , Mhe. Abdallah Ulega (wa pili kulia) na
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt.Angeline Mabula
wakimsaidia Bi.Eliminia Mbuhi mkazi wa kitongoji cha Ikanka katika
kijiji cha Itumba wilayani Ileje mkoa wa Songwe wakati Kamati ya
Mawaziri Nane inayoshughulikia migogoro ya Matumizi ya Ardhi katika
vijiji 975 ilipotembelea kitongoji hicho.
"Kwa nini
tuna mashamba ya kilimo mazao mengi na kwa nini kilimo mifugo hakina
hati? Wafugaji wana hamasa za kutaka kununua na kumiliki ardhi kwa kuwa
siyo maskini na uwezo wanao,’’amesema Mheshimiwa Ulega.
Ameongeza
kwa kusema kuwa, hatua ya kuyapatia mashamba mifugo hati mbali na
kuwasaidia wafugaji kuwa na umiliki wa ardhi, lakini itawazuia kuhama
kutoka sehemu moja kwenda nyingine sambamba na kuwatambua kwa urahisi
ambapo alisema kwa sasa inakuwa vigumu hata wafugaji kukopesheka wakati
ni matajiti.
Alisema, haiwezekani kumaliza migogoro ya ardhi kwa
maneno na watendaji katika ngazi zote wanapaswa kufanya kazi kwa
vitendo na kusisitiza kuwa hata kama utekelezaji huo utaanza kwa mfugaji
mmoja mmoja itasaidia na kutaka watendaji kubadilika ili kuiboresha
sekta ya mifugo.
Kwa
mujibu wa Ulega, pamoja na kuwepo fursa nyingi za uhitaji wa nyama
kwenye nchi mbalimbali duniani na Tanzania kuwa na idadi kubwa ya mifugo
kama vile ng’ombe, mbuzi na kondoo, lakini imeshindwa kuchangamkia
fursa hiyo.
Alisema, kwa sasa wizara yake inaboresha sera ya
mifugo na kutaka kila mmoja kushiriki katika kuhakikisha sekta ya mifugo
inaimarika na kufanya vizuri.