NA DIRAMAKINI
WAHANGA wa matukio ya uhalifu ya Panya Road wamelipongeza kwa kuimarisha hali ya amani kwenye maeneo pamoja na kuliomba jeshi hilo kupitia Mkuu wa jeshi hilo, IJP Camillius Wambura kuendeleza na operesheni za kukabiliana na wahalifu ikiwemo Majambazi na Wahalifu hasa Panya Road kwa ajili usalama wao.
Wito huo umetolewa wakati wahanga hao ambao ni wakazi wa Vingunguti Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam walipozungumza na vyombo vya habari kuhusiana na matukio ya kiuhalifu yaliyofanywa na Panya Road sambamba na hatua zilizochukuliwa na Jeshi la Polisi ambapo wamesema, kwa sasa amani imerejea.
Akizungumza kwa uchungu, Bi.Aisha Rajabu ambaye mtoto wake aliyejulikana kwa jina Kinahe Baraka alifariki kwa kuchomwa kisu na Panya Road amelitaka Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua kali za kisheria wahalifu wote kwa manufaa ya wananchi.
"Wamemuua binti yangu Kinahe Rajabu alikua ananisaidia, anajituma sana katika kazi zake, kama wao Panya Road wanauwa watu kwa nini wao wasiuawe, tunaliomba Jeshi la Polisi litusaidie kukabiliana nao, maana wakiwacha watatumaliza wote,"amesema Bi.Aisha Rajab ambaye ni mzazi wa mtoto aliyeuawa na Panya Road.
Kwa upande wake Mzee Christopher John ambaye mtoto wake ni mmoja wa Panya Road waliokamatwa na Jeshi la Polisi amesema, yeye kama mzazi anaumia mtoto wake kujihusisha na uhalifu na ukizingatia amemuonya zaidi ya mara moja.
"Mimi mtoto wangu ni Panya Road na sasa amekamatwa na Jeshi la Polisi kama mzazi naumia sana kwa sababu nilishamuonya na kuna wakati nilitamani hata nimnyweshe sumu kwa sababu ya tabia yake mbaya,"amesema Christopher John ambaye ni maba mzazi wa Panya Road mmoja.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa Majengo Vingunguti, Chande
Mohammed Msoke amesema, tangu Jeshi la Polisi lifanye operesheni ya
kuwakamata wahalifu (Panya Road) kwa sasa hali ni shwari na wanatembea
muda wowote.