WANASIASA NI BALAA:Hata ukitaka mzizi wa Bahari ya Hindi anakuletea

NA WILLIAM BOMBOM

NDUGU yangu ukajichanganya ukaingia kwenye kumi na nane za mwanasiasa kumsikiliza unaweza ukaamini umekutana na malaika.

Ni wastaarabu waliojawa busara na hekima pindi wanapozungumza, unaweza ukaamini anachokueleza ni kweli tupu. Huwa wanazungumza kwa vituo kwa ulimi laini hawana matao wala tambo pindi anakuingiza mkenge.
PICHA NA YOURLIFECHOICES.

Wanasiasa wengi mishipa yao ya aibu imekata, hawanaga aibu hata kidogo. Wanasiasa hasa hawa wa nywele ngumu wanaweza wakakuambia watakuletea mbegu za jiwe ili upande nyumbani kwako usisumbuliwe na maji kama unaishi sehemu yenye majimaji.

Hawana aibu hata kidogo, kesho atakuja na jambo jingine gumu zaidi ya lile la mwanzo. Anaweza kukuambia nyumbani kwake amebakiza mbegu tatu za wingu, maana mbegu nne za wingu alishazigawa akipata muda atakuletea.

Wanasiasa ndugu zangu si wa kuamini hata kidogo, ni pasua kichwa. Mwanasiasa ni mwanasiasa haijalishi ni kaka yako, mjomba baba au shangazi wote ni waongo tu.

Kwanza neno "Siasa* limetokana na neno "sihasa" baada ya kufanya udondoshaji wa konsonati "h" likiwa na maana ya "si kweli" ni "uongo" ndiyo maana ni rahisi kwa mwanasiasa kukuambia kuku wake ametotoa vipaka viwili huku akiwa na majonzi. Kwa mwanasiasa hakuna kinachoshindikana, hata ukitaka mzizi wa Hahari ya Hindi anakuletea.

Wanasiasa wanaweza kusimama jukwaani, wakapinga kwa nguvu zote suala la waganga. Lakini ni wanasiasa hao hao huongoza kupishana kwa waganga mchana na usiku, wengine wanavuja mikononi mwao damu za wapendwa wao waliowatoa kafara kwenye ulingo wa siasa.

Ni rahisi kwa mwanasiasa kukuchanganyia maji aliyooga kwenye chakula utakachokula ili atimize malengo yake. Siasa! Siasa! Kweli sihasa.

Ni wanasiasa wachache sana wenye huruma na jamii hasa hii ya nywele ngumu. Ukitaka kuliamini hilo angalia maisha ya wanasiasa na raia wa kawaida.

Raia wamechoka...huku wanasiasa wamenawiri. Zigo la kodi katwishwa raia huku mwanasiasa anafyonza asali na maziwa.

Huduma za maji si za uhakika, umeme bado ni janga, huku baadhi ya wanasiasa wakifanya kazi kwa kusuasua.

Mwanasiasa kukuambia sukari ni mchanga na mchanga ni sukari ni suala la kawaida. Mwanasiasa kukuambia siasa siyo nzuri ni suala la kawaida, lakini ukichunguza kwa upande wake haachi tena wengine huwalithisha mpaka watoto wao.

Siasa za namna hii ndizo chanzo cha taifa letu kutopea kwenye lindi la umasikini. Lini taifa letu litakuwa miongoni mwa mataifa matano bora duniani kwa uchumi?

Lini taifa letu litakuwa na viwanda vya kutengeneza magari, treni, ndege na meli kama tutaendelea kuwa na siasa ya namna hii?.

Lini taifa letu litaanza kununua na kuendeleza teknolojia yake ya vifaa vya kivita kama bado tumekumbatia siasa hii?.

Tumebaki kuwa mashabiki wa wenzetu huku tukitumia gharama kubwa kununua vitu kwao wakati malighafi wanazitoa kwetu?.

Ushauri

Mosi, kuna umuhimu wa kubadili mfumo wa siasa yetu. Jambo hilo si la haraka, ni vyema nchi ikawekeza kwa vijana na watoto wetu siasa ya uzalendo wa vitendo kuliko maneno.

Pili, kuna umuhimu wa kuiangalia kwa jicho jingine katiba yetu. Kipengele muhimu kinachotakiwa kuingizwa ni kwa wahujumu wa uchumi wa nchi yetu, watu hao wanapaswa kunyongwa hapa tunaweza kutibu suala la wanasiasa wala rushwa.

Tatu, kuna umuhimu wa kubadili mfumo wa elimu yetu iendane na matakwa yetu. Elimu iliyopo ina mazuri na mapungufu yake inamuandaa mwanafunzi kuwa tegemezi kwa serikali badala ya serikali imtegemee.

Elimu ijikite kwenye vitendo zaidi, mtoto aandaliwe kwenye eneo lake toka utotoni mpaka ukubwani atakuwa na uwezo mkubwa.

Nne, serikali iwakusanye watu wenye fani zinazofanana, mfano Masoud Kipanya na watu wa sampuli yake. Wakikaa pamoja miaka mitano wanaweza kutengeneza gari zinazoendana na uchumi wetu.

Hapo tutakuwa tumezalisha ajira kuanzia machimboni, viwandani, mitaani nk. Huo ni mfano mojawapo, endapo watakusanywa watu wa fani mbalimbali na kuwekwa kwenye makundi yao ninaamini tutapata sehemu ya kuanzia.

Hatujachelewa sijui wanasiasa wa leo wananielewa? Tuangalia ustawi wa taifa letu baada ya miaka thelathini mbele.

Siasa za kuneemesha matumbo yetu na siasa za kelele hazina mashiko, siasa za mjuano zinaturudisha nyuma.

Ni vyema tukawapa watu nafasi kulingana na uwezo wao, mie siyo muumini wa siasa za jinsi bali ni muumini wa uwezo wa mtu.

Endapo ndani ya jamii wanawake ndiyo wenye uwezo wa kutuvusha wapewe hata kama nafasi zote. Vivyo hivyo kwa wanaume.

HII NI NDOTO YANGU
THE BOMBOM

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news