NA GODFREY NNKO
WAWAKILISHI wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mashindano ya Utanashati, Urembo na Mitindo ya Viziwi Duniani ambayo yanafanyika hapa nchini Oktoba 29, 2022 wamesema wapo tayari kuwapa heshima Watanzania na Taifa kwa ujumla.
Hayo wameyasema kwa nyakati tofauti leo Oktoba 27, 2022 wakati wakiwa katika hatua za mwisho za maandalizi kupitia kambi ya pamoja na wawakilishi wengine kutoka mataifa mbalimbali duniani yanayoendelea katika Hoteli ya Peacock jijini Dar es Salaam.
Tanzania ambayo inawakilishwa na wawakilishi sita katika mashindano hayo, wamesema Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imewapatia kila wanachohitaji ili waweze kushiriki kikamilifu na waweze kutoa ushindani wa kutosha katika mashindano hayo.
"Maandalizi yameenda vizuri, ninaamini tutafanya vema sana, pia ninawaomba Watanzania wenzangu waendelee kutuombea kwa Mwenyenzi Mungu tunaamini uwezo wa kubakiza mataji yote tunao. Nichukue nafasi hii kuwaomba tena wasikose kutufuatilia na hata wale ambao wamepata nafasi ya kushiriki siku ya tukio waje ili kutuunga mkono,"amesema mshiriki Hadija Rajabu, binti Kanyama.
Hadija ambaye ni miongoni mwa wawakilishi sita wa Tanzania ana umri wa miaka 24 na amezaliwa Julai 8, 1998 huko Majengo Wilaya ya Muheza mkoani Tanga.
"Mimi ni miongoni mwa Watanzania sita ninaowawakilisha katika Mashindano ya Viziwi ya Urembo, Utanashati na Mitindo ya Dunia yanayofanyika Oktoba 29, pale Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam,"amesema.
Binti huyo ambaye elimu ya msingi aliipata huko Mwanga Viziwi mkoani Kilimanjaro mwaka 2006 hadi 2015 na elimu ya sekondari Moshi Ufundi kati ya mwaka 2016 hadi 2019 amesema, ana uwezo wa kufanya vizuri zaidi katika mashindano hayo.
"Ninaamini kuwa kupitia mashindano haya ya Dunia ninakwenda kuipeperusha vema bendera ya Tanzania na ninaahidi kuliacha taji hilo hapa nchini, hivyo ahadi yangu kwa Watanzania ni kwamba nitashinda na ndiyo ahadi pia kwa wanzangu ambao tupo nao hapa kambini kwa ajili ya kuliwakilisha Taifa,"amesema.
Kwa upande wao, Nasra Swalehe na John Mushi ambao ni wakufunzi wanaofundisha miondoko kwa washiriki wa Tanzania katika kambi hiyo wamesema, wanafarijika kuona kuwa, wawakilishi hao wa Tanzania wameonesha juhudi kubwa ambazo zinawapa faraja kuwa, Oktoba 29, 2022 watafanya mambo makubwa.
Nao baadhi ya washiriki kutoka Sudan Kusini, Zimbabwe, India, Zimbabwe na Afrika Kusini wameieleza DIRAMAKINI kuwa, Serikali ya Tanzania imewapa heshima ya kipekee kupitia maandalizi wanayoendelea nayo katika kambi ya pamoja.
Wamesema,viongozi wa Serikali muda wote wameendelea kuwapa ushirikiano wa hali ya juu, hivyo kujihisi kuwa maandalizi wanayoyafanya ni sawa na wakiwa nyumbani kwao.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa, Dkt.Emmanuel Ishengoma amesema, Tanzania kama nchi mwenyeji wa mashindano hayo makubwa ya utanashati, urembo na mitindo duniani imetoa ushirikiano wote kwa washiriki ili kuhakikisha kila mmoja anashiriki kikamilifu mashindano hayo Oktoba 29, 2022.
Dkt.Ishengoma ametumia nafasi hiyo kuishauri jamii kuendelea kuwathamini watu wenye ulemavu, kwani hata wao wamekirimiwa vipaji vya kipee ambavyo vikiendelezwa vitaleta matokeo bora kwa jamii na Taifa kwa ujumla.
Mashindano hayo yatafanyika Oktoba 29, 2022 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JICC) jijini Dar es Salaam ambapo yatawashirikisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania.