Watanzania mguu sawa kutwaa taji la Mrembo na Mtanashati Kiziwi wa Dunia 2022

NA GODFREY NNKO

WAWAKILISHI wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mashindano ya Utanashati, Urembo na Mitindo ya Viziwi duniani wamesema wana vigezo na sifa zote za kutwaa taji hilo kwa mwaka huu wa 2022.
Hayo wameyabainisha kwa nyakati tofauti wakati wakiendelea na mafunzo maalumu kupitia kambi inayosimamiwa na Serikali kupitia Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo leo Oktoba 21, 2022 jijini Dar es Salaam. Ikiwa ni siku chache zimesalia kabla ya mashindano hayo kufanyika Oktoba 29, 2022 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JICC) jijini humo.

DIRAMAKINI imeshuhudia washiriki na viongozi mbalimbali waandamizi kutoka nje ya nchi wakiwasili kwa ajili ya tukio hilo la kwanza na kubwa hapa nchini.
Tanzania inawakilishwa na washiriki sita huku wanawake wakiwa wanne na wanaume wawili ambapo Serikali imewapa ushirikiano mkubwa kuanzia gharama zote wawapo kambini hadi mashindano hayo yatakapofikia tamati.

Washiriki hao akiwemo Carolyne Mwakasasa na Rajani Ally wamesema kuwa, wana imani kubwa na wataweza kuipeperusha vema bendera ya Tanzania na kutwaa taji hilo.

Pia wamesema kuwa, ahadi yao ni kushinda huku wakitoa wito kwa watu wenye ulemavu kutokata tamaa, na fursa zinapojitokeza wazichangamkie kwani uwezo, ari na nguvu ya kusonga mbele wanayo.

Rajani Ally amesema,vigezo vyote vya kushinda katika shindano hilo la kidunia anavyo ikizingatiwa kwamba, walimu wao wanaendelea kuwamegea maarifa na mbinu mbalimbali za kuweza kulimudu jukwaa siku ya mashindano hayo.
"Ninaamini nitafika mbali, kwani ninapenda sana mitindo, urembo,utanashati na kufundisha watu wa aina mbalimbali wakiwemo wenye ulemavu, hivyo ni ahadi yangu kwa Watanzania kwamba, nitashinda kaika mashindano haya na siku za mbeleni nina maono mazuri kwa ajili ya jamii na Taifa kwa ujumla,"amesema.

Naye mshindi wa pili katika mashindano ya Urembo, Utanashati na Mitindo kwa Viziwi Afrika yaliyofanyika hapa nchini mwaka jana, Bi.Carolyne Mwakasasa amesema, kuwa na ulemavu si kigezo cha kushindwa kujumuika na wengine katika kuziendea ndoto zako.

Mwakasasa ametoa ushauri kwa vijana ambao wana ulemavu wa aina yake wajitokeze kwa wingi kushiriki mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi na wasione aibu kushiriki kwani, uwezo wa kufanya vizuri wanao.

Serikali

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa, Dkt.Emmanuel Ishengoma amesema, Tanzania kama nchi mwenyeji wa mashindano hayo makubwa ya utanashati, urembo na mitindo bora ya Dunia wamejipanga kwa maandalizi ya awali hadi hatua za mwisho na wanatarajia kufanya vizuri.
Dkt.Ishengoma amesema,maandalizi ya awali yalianza tangu Agosti, mwaka huu katika Chuo cha Sanaa cha Bagamoyo na sasa wanaendelea katika hatua za mwisho ili kuhakikisha vipaji vya wawakilishia hao wa Tanzania vinang'ara.

Amesema, ni jambo la kujivunia na kupongeza juhudi za Rais wa Jmahuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuja na ubunifu mbalimbali ikiwemo kuasisi filamu ya Tanzania The Royal Tour ambayo imekuwa dira na mwongozo kwa watu wengi kutoka nje ya nchi, kuja nchini kwa ajili ya kutalii, kuwekeza na hata kuendesha matukio makubwa ambayo yalipaswa kufanyika kwenye mataifa yenye nguvu za kiuchumi duniani.

Dkt.Ishengoma amesema, mbali na maandalizi hayo pia Idara ya Uhamiaji inaendelea kupokea wageni kutoka nchi mbalimbali kwa ajili ya kuanza kuwasili kambini kusubiri fainali rasmi ambayo inatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu jijini Dar es Salaam.

Rais

Kwa upande wake Rais wa Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Kimataifa linalojihusisha na Uandaaji wa Mashindano ya Urembo, Utanashati na Mitindo kwa Viziwi Duniani (Miss & Mister Deaf International, Inc), Bi.Bonita Ann Leek amesema, mwaka huu wameamua kuiteua Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano hayo kidunia kutokana na ukarimu wa Watanzania, upendo, mshikamano na amani iliyopo nchini.
MMDI ni shirika lisilo la faida ambalo limenuia kuwezesha, kuimarisha, na kuunga mkono vipaji vya wanawake na wanaume viziwi ili viweze kutambuliwa na kuendelezwa duniani kwa ustawi bora wa maisha yao na Taifa kwa ujumla.

Amesema, mshindi wa jumla wa shindano hilo huwa ndiye Balozi wa Jumuiya ya Viziwi na huwa sehemu ya hamasa kwa jamii kushiriki katika shughuli za maendeleo ikiwemo elimu, afya na nyinginezo.

Dhamira ya shirika hilo ni kuonesha Dunia kuwa, jamii ya watu wenye ulemavu wa kutosikia inayo uwezo mkubwa wa kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii na Kitaifa achilia mbali uzuri walio nao.
Hata hivyo, hii inakuwa heshima kubwa zaidi kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano hayo Duniani kwa mwaka huu, baada ya heshima nyingine waliopewa Oktoba Mosi, 2021 kwa kuwa mwenyeji wa mashindano ya namna hiyo barani Afrika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news