Watu 13 mbaroni kwa kuhujumu TANESCO wakiwemo watumishi wa Mungu

NA DIRAMAKINI

JESHI la Polisi Mkoa wa Shinyanga limewakamata watu 13 wakituhumiwa kuhujumu na kuharibu miundombinu ya Shirika la Umeme (TANESCO) na kulisababishia hasara zaidi ya shilingi milioni 10 kati yao wapo watumishi wawili na wachungaji wa dini wawili.Kamanda wa Jeshi la Polisi wa Mkoa wa Shinyanga,ACP Janeth Magomi amewaeleza waandishi wa habari kuwa,watuhumiwa hao walikamatwa kwa nyakati tofauti wilayani Kahama.

Amesema, TANESCO kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi walifanya operesheni maalumu kwa lengo la kuwakamata watu wanaojihusisha na vitendo vya kuhujumu miundombinu ya umeme pamoja na waliojiunganishia bila utaratibu na kufanikiwa kuwakamata watu 13.

Amesema, kati ya watuhumiwa hao wapo watumishi wawili wa Tanesco, vishoka wanne, Akofu wa Kanisa la CAG na mchungaji mmoja pamoja na wateja saba ambao walibainika kujiunganishia umeme kinyume cha utaratibu na wafanyakazi hao wasiokuwa waaminifu kwa kushirikiana na vishoka na kufanya wateja hao watumie umeme bila malipo yeyote.

Kamanda Magomi amesema katika operesheni hiyo ilibainika watumishi hao wawili wasiokuwa waaminifu kwa kushirikiana na vishoka wanne walibainika kuhujumu miundombinu ya shirika kwa kuiba vifaa pamoja na kuwaunganishia wateja umeme bila kufuata taratibu na kwa maslahi binafsi.

Pia amesema katika hujuma hiyo jumla ya transfoma 73 za umeme zilihujumiwa na kusasabisha uharibifu mkubwa kutokana na kuibiwa vifaa mbalimbali zikiwemo waya za kopa na kulitia hasara shirika zaidi ya shilingi milioni 10 pamoja na wateja hao waliounganishiwa umeme kinyume cha utaratibu na kutumia bure.

Kaimu Meneja wa TANESCO wa Wilaya ya Kahama, Mhandisi Tumaini Chonya akifafanua kuhusu hujuma hiyo amesema, wafanyakazi hao wasiokuwa waaminifu walikuwa wanaiba vifaa vya shirika na kwenda kuwaunganishia umeme watu kinyume cha utaratibu yakiwemo makanisa ya viongozi hao waliokamatwa na kutumia umeme bure siku zote.

Mhandisi Choya amesema, hujuma iliyofanywa na watu hao ni kubwa kwa sababu wamelitia hasara shirika na kukwamisha jitihada za kupanua huduma kwa wateja hali iliyomfanya kutoa wito kwa wananchi wenye mapenzi mema kutoa taarifa kwa Tanesco na kwa jeshi la polisi kuhusu vitendo vya hujuma dhidi ya miundombinu ya shirika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news