NA ROTARY HAULE
JESHI la Zimamoto na Uokoaji Tanzania limewahakikishia wawekezaji kuwepo kwa usalama wa viwanda vyao na mali zao kwa kuwa limejipanga kikamilifu kupambana na majanga ya moto yanayotokea sehemu mbalimbali hapa nchini.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ambaye pia ni msemaji wa jeshi hilo nchini, Puyo Nzalayamis ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na waandishi katika Maonesho ya Tatu ya Wiki ya Uwekezaji na Biashara yanayofanyika Kibaha mkoani Pwani.
Nzalayamis amesema kuwa, Jeshi la Zimamoto linashiriki maonesho hayo kwa ajili ya kuelimisha umma masuala ya usalama lengo likiwa ni kuhakikisha kila mshiriki anapata elimu ya kutosha juu ya masuala ya uzimaji wa moto.
Aidha,amesema kuwa kwa sasa jeshi limejipanga vizuri na wana vifaa vya kisasa na vya kutosha kukakabiliana na majanga ya moto na kwamba wawekezaji wasiwe na wasiwasi juu ya jeshi hilo.
"Niwahakikishie wawekezaji usalama wa viwanda vyao kwa kuwa tumejipanga vizuri kukabiliana na majanga ya moto, lakini tunawaomba watoe taarifa mapema pale ambapo wanagundua kuwepo kwa hitilafu ya moto katika viwanda vyao,"amesema Nzalayamis.
Nzalayamis ameongeza kuwa, kwa sasa jeshi hilo limeboresha mawasiliano ambapo wanaweza kupatikana muda wowote kupitia namba 114 ambayo ni bure na haina malipo.
"Tunawaomba wana jamii, wananchi na wawekezaji wote kushirikiana kwa kupiga namba hiyo na sisi tukipata taarifa mapema itatusaidia kufika eneo la tukio kwa wakati kwa ajili ya kuokoa mali husika kwa wakati,"ameongeza Nzalayamis.
Kuhusu vifaa, Nzalayamis amesema kuwa jeshi limejipanga kikamilifu na kwasasa Kila Mkoa una magari ya Zimamoto na bajeti ya mwaka huu magari mengine mawili yatanunuliwa.
Katika hatua nyingine jeshi hilo limekabidhiwa hati ya ardhi kutoka Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya Zimamoto katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze .
Hata hivyo, Nzalayamis amesema eneo hilo linaukubwa wa mita za mraba 317 ambapo ameishukuru Wizara hiyo kwa kuona umuhimu wa kukabidhi hati hiyo katika Jeshi lake na kusema kuwa ardhi hiyo itatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wa Mkoa wa Pwani Jenifa Shirima amesema, baada ya maonesho hayo watapita kila shule kwa ajili ya kutoa elimu ya Zimamoto kwa wanafunzi.
Shirima amesema, kampeni hiyo itakuwa maalum kwa wanafunzi wa sekondari na shule za msingi ili kuwajengea uelewa mapema na kwamba baada ya elimu hiyo watakuwa makini kudhibiti majanga ya moto.
Hata hivyo,Shirima amewaomba wadau pamoja na wawekezaji wa viwanda na biashara wanaoshiriki maonesho hayo kutembelea banda la Zimamoto lililopo katika viwanja hivyo ili waweze kupata elimu zaidi.