NA MWANDISHI WETU
WAZAZI wamehimizwa kusimamia misingi ya malezi kwa vijana wanapohitimu kidato cha nne kwa kuhakikisha wanaendelea na masomo ya kidato cha tano na cha sita ili kuendelea kuwafuatilia kwa ukaribu mienendo ya tabia zao.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Mhe. George Simbachawene akiwa katika maandamano na wahitimu wa kidato cha nne shule ya Sekondari ya Mtakatifu Catherine.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Mhe. George Simbachawene katika mahafali ya nane ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Catherine iliyopo Lushoto jijini Tanga.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Mhe. George Simbachawene akihutubia mahafali ya nane ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Catherine.
"Elimu hii inaushindani mkubwa katika kazi, msome kwa ajili ya uelewa na msome kwa ajili ya kuja kushiriki udahili katika ushindani wa kupata kazi na uwezo wa kujitegemea.
“Katika kipindi hiki ambacho wanasubiria matokeo, wazazi msiwape uhuru vijana kwa sababu umri walionao bado ni mdogo na bado wanahitaji malezi. Wekeni utaratibu wa kutumia simu janja katika kipindi hiki ili waweze kuweka mkazo katika kutimiza malengo yao,”amesema Waziri.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Mhe. George Simbachawene akimsiliza Mwanafunzi Cythia Richard Mwanafunzi wa kidato cha sita Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Catherine.
"Sitegemei kumuona mmoja wa wahitimu hawa akipotea katika maadili mabovu na matumizi ya dawa za kulevya, bali ni matumaini yangu wote mtasonga mbele na kufikia ngazi za juu kabisa za taaluma. Hii ni kwa manufaa yenu binafsi na taifa letu kwa sababu bado tuna uhitaji mkubwa wa wataalamu na ninyi ni sehemu ya wataalamu tunaowahitaji hapo baadaye,"amesema.
Naye Sr.Fokas Mjema, Msaidizi wa Mama Mkuu wa Shirika la Masister wa Usambara na Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Catherine, amewashukuru walimu na wanafunzi kwa kufanya mitihani ya majaribio kwa bidii na uangalifu na kuwa makini.
“Wahitimu wetu wa kidato cha nne wanafunzi 65 wameandaliwa vizuri, tunategemea kutokana na maandalizi wapate ufaulu wa daraja la kwanza na ufaulu wa daraja la pili,”amesema.
Akieleza namna Shule ya Mtakatifu Catherine ilivyojiaanda na Mtihani wa Taifa Mwalimu wa Taaluma, Nyandwi Mathias Marko amesema, shule ina utaratibu wa kufanya mitihani ya majaribio, mitihani ya majaribio kwa vitendo, mitihani ya mwaka, mitihani ya kila wiki, mitihani ya ushirikano na shule nyingine na mazoezi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene akikabidhi vyeti katika mahafali ya wanafunzi wa kidato cha nne.
“Tunatumia mitihani hiyo kufanya tathimini kwa kuangalia udhaifu ili kuwasogeza sehemu inayostahili,”amesema Mwalimu wa Taaluma.
Akitoa nasaha kwa niaba ya wazazi wengine, Dkt.Wambuka Rangi ametoa rai kwa wanafunzi kuendelea kuwa wachamungu ili kuepukana na matendo maovu ambayo yanapoteza ndoto hasa za watoto wa kike.
“Tunaomba muwe waadilifu na wasikivu kwa wazazi mtakapokuwa nyumbani, ili muweze kufanikiwa katika maisha yenu ya baadae,”amesema.