Waziri Dkt.Jafo awaonya wanaokwamisha wawekezaji

NA ROTARY HAULE

WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira,Dkt.Selemani Jafo amewataka watendaji wa Serikali wanaochelewesha nyaraka na vibali vya wawekezaji kuacha mara moja tabia hiyo.
Amesema,kukwamisha vibali vya wawekezaji hao ni kukwamisha juhudi zinazofanywa na Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan za kutengeneza mazingira mazuri kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza hapa nchini.

Dkt.Jafo ametoa kauli hiyo Oktoba 8, mwaka huu wakati alipokuwa akifungua Kongamano la Uwekezaji na Biashara Mkoa wa Pwani lililofanyika katika Chuo cha Siasa cha Mwalimu Julius Nyerere kilichopo Kwamfipa Kibaha.

Amesema,Serikali inapambana katika kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kuunganisha maji, barabara na umeme kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji, lakini bado kuna baadhi ya watendaji wanakwamisha juhudi hizo.
"Rais ameitangaza nchi hii kila sehemu na nchi imefunguliwa kweli kweli, lakini kitendo cha mtendaji kuleta urasimu ni sawa na kumkwamisha Rais mwenye dhamira njema ya kuiletea nchi maendeleo,"amesema Dkt.Jafo

Aidha,Dkt.Jafo amewatoa wasiwasi wawekezaji hao kuwa Mkoa wa Pwani upo salama kwa uwekezaji huku akiwataka kuhakikisha wanafungua ofisi na kulipa ushuru kwenye mkoa husika ili uweze kupata mapato kikamilifu

Amesema, wapo wawekezaji wamewekeza katika mkoa wa Pwani lakini ushuru wanalipa walipofungulia ofisi zao ambapo ni Dar es Salam jambo ambalo linashusha mapato ya mkoa.
"Wawekezaji fungueni ofisi Pwani ili wilaya ziweze kupata mapato na kufanya maendeleo kutokana na ushuru mnaolipa, sio mwekezaji amewekeza Pwani ofisi ipo Dar es Salaam na analipa ushuru huko utaratibu huo unakosesha mapato,"amesema.

Aidha, Dkt.Jafo amesema kwa sasa nchi imejipambanua kwa kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji na kufungua fursa kwa wawekezaji wa nje ya nchi kuja kuwekeza.

"Rais wetu Samia Suluhu Hassan ameitangaza nchi kila sehemu na sasa tunaona wawekezaji wanavyoongezeka mazingira yameboreshwa barabara zimejengwa, usafiri wa anga na nchi kavu na hii itarahisisha bidhaa zinazozalishwa zisafirishwe kwa urahisi,"amesema
Waziri huyo pia aliishauri Wizara ya Viwanda na Biashara kushirikiana na Mkoa wa Pwani kuandaa kongamano la biashara na uwekezaji kwa mkoa huo ambalo litautangaza zaidi ya mkoa huo na mikoa mingine ipate fursa ya kufika kujifunza.

"Wizara ya Viwanda na Biashara itangaze mkoa wa Pwani kama mkoa wa Maonesho ya Kibiashara iwe inafanyika kila mwaka na kongamano la uwekezaji kama hili mikoa mingine ije ijifunze na nchi itangazike,"amesema.

Awali Mkuu wa mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amesema mkoa una dhamira ya kuwa wa mfano katika sekta ya uwekezaji na kwamba kongamano hilo pamoja na maonesho ya biashara vinafanyika kupitia vipaumbele vya Rais Samia Suluhu Hassan.
Kunenge amesema, kongamano hilo limefanyika kwa lengo kupata ufumbuzi na suluhisho la kuongeza uwekezaji na kwamba maazimio yake yatasaidia kupanua wigo kwa wawekezaji wengine kuja kuwekeza Pwani.

Amesema, kwa sasa mkoa huo una viwanda 1,460 vikubwa vikiwa 90 huku kukiwa na kongani 23 za viwanda na kwamba katika kongani ya Sino Tan iliyopo Kwala katika Halmashauri ya Kibaha Vijijini inatarajia kuwa na viwanda 350.

Mkurugenzi wa SinoTan, Janson Huang amesema, kwa sasa wanaendelea kuwashawishi wawekezaji kutoka nje ya nchi kufika kujenga viwanda katika kongani hiyo na kwamba itajengwa kwa awamu na itakamilika kwa kipindi cha miaka mitano.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news