NA DIRAMAKINI
WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe.Dkt.Ashatu Kijaji ( Mb) amesema Serikali inafanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha viwanda vya nguo nchini vinavyoajiri watu wengi hususani wanawake na vijana vinafanya kazi kwa ufanisi.

Dkt. Kijaji ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Kiwanda cha nguo cha A TO Z, Bw. Kalpesh Shah akiwa na Meneja Mauzo ya Nje wa Kiwanda hicho, Bw. Sylvester Kazi leo Oktoba 10, 2022 katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujadili na kUtatua changamoto zinazoikabili sekta ya nguo nchini.

Dkt. Kijaji pia amesema ni muhimu kuanzisha viwanda vya kuchakata pamba (spinning) nchini ili kuongeza thamani katika zao la pamba na kupunguza uuzaji wa pamba ghafi ambayo asilimia 70 ya pamba inayozalishwa nchini huwa inauzwa nje ya nchi kama malighafi.