NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amesema anatarajia kuiwakilisha Serikali ya Tanzania katika Kikao cha 73 cha Kamati Tendaji ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Wakimbizi (UNHCR).
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akizungumza Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania nchini Uswisi, Maimuna Tarishi (kushoto), wakati Waziri huyo alipowasili katika Ofisi za Ublaozi huo zilizopo jijini Geneva, Oktoba 9, 2022. Kulia ni Balozi na Naibu Mwakilishi wa Kudumu Tanzania, Hoyce Temu, na wa pili kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Huduma kwa Wakimbizi, Sudi Mwakibasi.
Kikao hicho ambacho kinaanza leo Jumatatu Oktoba 10, 2022, kitafanyika katika jijini la Geneva, nchini Uswisi, Ulaya Magharibi kitajadili masuala mbalimbali yakiwemo jinsi ya kuwahifadhi na kuwasimamia Wakimbizi waliopo katika nchi mbalimbali duniani.
Waziri Masauni ameambatana na Mkurugenzi wa Idara ya Huduma kwa Wakimbizi wa Wizara hiyo, Sudi Mwakibasi tayari wamewasili jijini Geneva nchini hapa, Jumapili Oktoba 9, 2022, akiwa tayari kuiwakilishi Tanzania katika Kikao hicho kwa kutoa taarifa ya Wakimbizi waliopo nchini.
Masauni na wasaidizi wake wamepokelewa na Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania nchini Uswisi, Maimuna Tarishi, Balozi na Naibu Mwakilishi wa Kudumu Tanzania, Hoyce Temu na Maafisa mbalimbali wa Ubalozi huo na baadaye kufanya kikao na maafisa hao wa ubalozi.
Akizungumza katika kikao hicho cha mapokezi kilichofanyika ofisi za ubalozi huo, jijini humo, amemshukuru Balozi Tarishi pamoja na maafisa wake kwa mapokezi mazuri na ameomba ushirikiano nao zaidi mpaka kikao hicho cha siku tano kitapomalizika.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (katikati) akizungumza katika kikao na Maafisa wa Ubalozi wa Tanzania nchini Uswisi wakati alipowasili katika jijini la Geneva nchini humo Oktoba 9, 2022 kwa ajili ya kuiwakilisha Serikali katika Kikao cha 73 cha Kamati Tendaji ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Wakimbizi (UNHCR). Watatu kushoto ni Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania, Maimuna Tarishi, wapili kulia ni Balozi na Naibu Mwakilishi wa Kudumu Umoja wa Mataifa, Hoyce Temu, na wapili kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Huduma kwa Wakimbizi, Sudi Mwakibasi. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi).
“Mheshimiwa Balozi pamoja na maafisa wote wa ubalozi huu, nawashukuru sana kwa mapokezi mlionipa, nashukuru kwa miongozo mbalimbali kuhusu kikao hicho, naamini tutakuwa pamoja katika kuiwakilisha Serikali katika siku zote za kikao,” alisema Masauni.
Awali Balozi Tarishi alishukuru kwa Waziri pamoja na msafara wake kwa kuwasili salama nchini humu na watakuwa pamoja naye katika kikao hicho muhimu ambacho kinatarjia kutoa dira kuhusu kuwahudumia wakimbizi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mwakibasi alisema Tanzania imekuwa mjumbe wa muhimu kwenye Kamati Tendaji ya UNHCR kufuatia historia ya muda mrefu kwenye uhifadhi na usimamizi wa masuala ya Wakimbizi nchini Tanzania.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (katikati) akimsikiliza Balozi na Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania katika Umoja wa Taifa, Geneva nchini Uswisi, Hoyce Temu akifafanua jambo katika Kikao cha Waziri huyo na Maafisa wa Ubalozi, kilichofanyika Ofisi ya Ubalozi huo, jijini Geneva, Oktoba 9, 2022. Wapili kushoto ni Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania, nchini Uswisi, Maimuna Tarishi, na kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Huduma kwa Wakimbizi, Sudi Mwakibasi. (Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi).
“Mheshimiwa Waziri, kikao hiki ni Kikao kazi ambacho ufanyika kwa mujibu wa ratiba kikiwa na lengo la kujadili masuala mbalimbali ya Wakimbizi ambapo Tanzania pia ni moja ya nchi duniani inayohifadhi na kusimamia wakimbizi,” alisema Mwakibasi.