Waziri Mhagama atoa maagizo kuhusu mashauri ya kinidhamu kwa watumishi

NA VERONICA MWAFISI

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amezitaka Kamati za Nidhamu kuhitimisha kwa wakati mashauri ya kinidhamu ya watumishi wa umma ili kuipunguzia serikali gharama kubwa ambayo imekuwa ikiingia kwa kuwalipa mishahara watumishi waliopoteza sifa ya kuendelea kuwa watumishi, ikiwa ni pamoja kupunguza gharama za kuendesha mashauri ya kinidhamu kwa muda mrefu.
Watumishi wa Halmashauri za Wilaya ya Arusha na Meru wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo wilayani Arumeru iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao.

Akizungumza na watumishi wa Halmashauri za Wilaya ya Arusha na Meru wakati wa ziara yake ya kikazi Wilayani Arumeru, Mhe. Jenista amesema Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kuwalipa watumishi ambao pengine baada ya kuhitimishwa kwa mashauri yao wanatakiwa kuondolewa katika utumishi wa umma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Watumishi wa Halmashauri za Wilaya ya Arusha na Meru wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani Arumeru iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao.

“Naziagiza Kamati za Nidhamu zote nchini kuhakikisha mashauri yote ya kinidhamu ya watumishi wa umma yanahitimishwa kwa wakati kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo ili haki itendeke, kwani Serikali imekuwa ikiwagharamia watumishi ambao wameshapoteza sifa ya kuwa watumishi wa umma na wanalazimika kutofanya kazi yoyote pindi wanaposubiri hatma ya mashauri yao,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Ameongeza kuwa, mtumishi anapotuhumiwa kuwa na kosa la kinidhamu na kufunguliwa shauri la kinidhamu, hatima yake ni aidha kuondolewa katika utumishi wa umma au kuendelea na utumishi wa umma, hivyo ni vema Kamati ziwe na utamaduni wa kuharakisha mchakato wa uendeshaji wa mashauri ya kinidhamu ili kuokoa fedha za serikali ambazo zitakazotumika kuboresha huduma mbalimbali za kijamii.
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe. Mhandisi Richard Ruyango akitoa salamu za wilaya yake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Jenista wilayani Arumeru iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa wilaya hiyo.

Aidha, Mhe. Jenista amewataka watumishi wa umma kufanya kazi kwa uadilifu, ubunifu na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuwa na tija katika maendeleo ya taifa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru, Bi. Zainab Makwinya akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa halmashauri yake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Jenista wilayani Arumeru iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa wilaya hiyo.

Waziri Jenista amesema, kila mtumishi kwa nafasi yake anao uwezo mkubwa wa kuitumia taaluma yake katika kuchangia maendeleo ya taifa na ndio maana Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuboresha maslahi yao ili kuwajengea morali ya utendaji kazi.

“Lengo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ni kuona taifa lake linapata maendeleo makubwa na sisi watumishi kila mmoja kwa nafasi yake tunaowajibu wa kuhakikisha tunatimiza ndoto ya Mhe. Rais,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella akitoa salamu za mkoa wake kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuzungumza na watumishi wa Halmashauri za Wilaya ya Arusha na Meru wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Jenista wilayani Arumeru iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa wilayani humo.

Akimkaribisha Mhe. Jenista kuzungumza na watumishi wa Halmashauri za Wilaya ya Arusha na Meru, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella amemshukuru na kumpongeza Mhe. Jenista kwa kuwa na utaratibu wa kufanya vikao kazi na watumishi wa umma ili kutatua changamoto zao na kuhimiza uwajibikaji.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Bw. Seleman Msumi akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa halmashauri yake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Jenista wilayani Arumeru iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa wilaya hiyo.

Mhe. Mongella amesema, mafanikio makubwa yanayopatikana nchini hivisasa yanatokana na uchapakazi wa watumishi wa umma ambao unachagizwa na watumishi kuridhishwa na namna serikali inavyowajali hivyo kuwaongezea morali ya kufanya kazi kwa bidii. Waziri Jenista ameendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Arusha inayolenga kutatua changamoto zinazowakabili, kuhimiza uwajibikaji na kukagua utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge (MKURABITA).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news