NA MWANDISHI WETU
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua Mkakati wa Kitaifa wa Uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (National Strategy for NGOs Sustainability) na kuagiza utafsiriwe kwa Kiswahili mara moja.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na mtoto mwenye ulemavu Chipowenga Zayeye, wa pili kulia ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Doroth Gwajima na wapili kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu wa CCBRT Brenda Msangi, katika wa Maonesho ya Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete, Oktoba 4, 2022 Dodoma (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
“Katika kuhakikisha uratibu wa shughuli za Mashirika Yasiyo ya Serikali unatekelezwa kwa ufanisi, ninaielekeza Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu kukamilisha tafsiri ya Mkakati wa Kitaifa wa Uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili kutoa fursa kwa wadau mbalimbali kuuelewa sambamba na kuunga mkono jitihada za kukiendeleza Kiswahili.”
Ametoa wito huo leo Jumanne, Oktoba 4, 2022 wakati akizindua Mkakati wa Kitaifa wa Uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (National Strategy for NGOs Sustainability) pamoja na Madawati ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Kisekta katika ukumbi wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipewa maelezo na Mkurugenzi Mkuu wa Asasi ya Msaada wa Kisheria (LSF) Lulu Ng’wanakilala kuhusu machapisho mbalimbali yanayotolewa na Asasi hiyo katika wa Maonesho ya Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma , Oktoba 4, 2022. Kushoto ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Doroth Gwajima (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, ameitaka Wizara hiyo ihakikishe Mkakati huo unazingatia maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa Septemba 30, 2021 kuhusu kufungamanisha mipango ya NGOs na ya Serikali ili kuhakikisha shughuli zao zinakuwa endelevu.
Amesema, Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa kutoka kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii. Ameiagiza Wizara hiyo ianze mara moja kufanya mapitio ya Sera ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya Mwaka 2001 ili kutoa fursa ya maboresho kwa Sheria, Kanuni na Miongozo inayosimamia Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea kutoka kwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt Doroth Gwajima Tuzo kwa niaba ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan wakati alipowahutubia kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Oktoba 4, 2022. Katikati ni Mwenyekiti Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Mwantumu Mahiza kulia ni Mwenyekiti wa NaCONGO, Dkt. Lilian Badi (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
“Viongozi wetu wakuu wanatambua mchango mkubwa unaotolewa na mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali ikiwemo huduma mbalimbali za kijamii kwa Watanzania. Serikali itaendelea kutoa ushirikiano wa dhati ili shughuli zenu ziwe endelevu,”amesema.
Ameyataka mashirika yote yasiyo ya Kiserikali yaboreshe mawasiliano na Mamlaka za Serikali katika maeneo yaliyopo na kutoa taarifa sahihi kuhusiana na shughuli zinazofanywa ili kuimarisha dhana ya uwazi na uwajibikaji.
Amezitaka Wizara na Mamlaka za Mikoa na Wilaya zihakikishe mashirika yote yasiyo ya Kiserikali yanatekeleza shughuli zao kulingana na usajili, malengo na vipaumbele vya Taifa. Aidha ameyataka mashirika yasiyo ya Kiserikali yajielekeze kufanya kazi maeneo yenye uhitaji ikiwemo vijijini badala ya kujikita katika maeneo ya mijini pekee.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Wadau wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Oktoba 4, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Kuhusu madawati yaliyozinduliwa leo, Waziri Mkuu amesema amepewa taarifa kuwa wizara 19 tayari zinayo madawati hayo. Ameziagiza Wizara nyingine ambazo bado hazijaanzisha madawati hayo, zihahakikishe zinateua maafisa dawati ili kurahisisha uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika sekta zao.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka viongozi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yenye makao makuu nchini waweke fedha kwenye benki za ndani ili fedha zinazoletwa nchini ziwe na thamani zaidi.
“Fedha hizo kama zinaingia Tanzania makao makuu au kwenye tawi, ni vema ziwekwe kwenye mabenki ya Kitanzania badala kuwekwa kwenye mabenki ya nje ya nchi na kuzileta nchini kwa ajili ya matumizi tu. Kufanya hivyo, zinakuwa hazina thamani kubwa kuliko kama fedha hiyo itakaa kwenye mabenki ya ndani,” amesema.
Amesema taarifa iliyowasilishwa ya mwaka 2021 kuhusu mashirika zaidi ya 900, imebainisha kuwa mapato yao yalikuwa kiasi cha sh. trilioni 1.1.
Baadhi ya washiriki wa Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali wakakimsikiliza mgeni rasmi Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipowahutubia kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Oktoba 4, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
“Taarifa iliyowasilishwa ya utendaji kazi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa mwaka 2021, imeonesha mapato ya sampuli ya mashirika 939 yaliyochambuliwa yalikuwa shilingi trilioni 1.1 wakati matumizi yalikuwa shilingi bilioni 900. Maeneo yaliyopewa kipaumbele ni utekelezaji wa afua za kujenga uwezo kwa jamii, afya, elimu, ustawi wa jamii, utawala, mazingira, kilimo, haki za binadamu, maji, jinsia, nishati na viwanda,” amesema.
Akitoa mfano, Waziri Mkuu amesema mwaka 2017, alipokwenda Ngorongoro alibaini kuwa kuna NGO moja ya ambayo ilikiri kupokea sh. bilioni moja lakini katika kipindi cha miaka miwili ilikuwa haina ofisi na iliweza kuchimba visima nane tu vya maji.