NA MWANDISHI WETU
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezitaka halmashauri zote nchini ziendelee kutekeleza agizo la Serikali la kutenga maeneo rafiki yatakayowawezesha vijana kushiriki shughuli za uzalishaji mali ili kuwaepusha na kero ya kufanya biashara kwenye maeneo hatarishi.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipewa maelezo na Kamishna Msaidizi wa Kinga na Huduma za Utengemao kutoka Mamlaka ya Uthibiti wa Dawa za Kulevya, kuhusu uthibiti wa dawa za Kulevya, wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Vijana kitaifa inayofanyika Mkoani Kagera, katika viwanja vya Gymkana Oktoba 12, 2022 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Ametoa agizo hilo leo Jumatano, Oktoba 12, 2022 alipozindua Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yanayofanyika katika viwanja vya Gymkhana mkoani Kagera. “Maeneo haya ni lazima yawe na sifa zinazoendana na shughuli zinazofanywa na vijana”.
Pia, Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Nchi - Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako ashirikiane na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Angela Kairuki ili kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa ipasavyo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifafanuliwa jambo na Afisa Zimamoto wa Wilaya Inspekta Thomas Majuto namna wanavyokabiliana na matukio ya moto, wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Vijana kitaifa inayofanyika Mkoani Kagera, katika viwanja vya Gymkana Oktoba 12, 2022 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Mbali na agizo hilo, Mheshimiwa Majaliwa amewaasa vijana kutumia vizuri fursa zilizopo nchini katika kujiletea maendeleo na kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana, ambayo inayoikabili dunia kwa sasa.
“Tanzania tunayo ardhi ya kutosha na yenye rutuba, tuna bahari, tuna maziwa na mito mikubwa, tunayo madini na sisi wenyewe kwa idadi yetu ni soko tosha la bidhaa mbalimbali, tutumie vizuri fursa hii ya kuwa na rasilimali nyingi kujipatia kipato.”
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akihutubia Wananchi, kwenye uzinduzi wa Wiki ya Vijana kitaifa inayofanyika Mkoani Kagera, katika viwanja vya Gymkana Oktoba 12, 2022 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu ameongeza kuwa fursa nyingine kwa vijana ni uhusiano mwema wa kidiplomasia na nchi zote duniani. “Fursa hii ikitumiwa vizuri na kundi la vijana wataweza kunufaika na kusonga mbele kimaendeleo”.
Akizungumzia kuhusu suala la mitaji, Waziri Mkuu amesema kuna mifuko mingi ya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, hivyo waitumie ili kupata mikopo hususan mikopo itokanayo na mapato ya ndani ya Halmashauri na kuwekeza katika miradi yenye tija.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipewa maelezo na Meneja Teknolojia wa MitzKits Wilfred Richard kuhusu maabara ndogo ya kufundisha sayansi kwa vitendo alipotembelea mabanda, wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Vijana kitaifa inayofanyika Mkoani Kagera, katika viwanja vya Gymkana Oktoba 12, 2022 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Kadhalika, Waziri Mkuu amewasihi vijana wawe wazalendo na walinzi wa miundombinu ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. “Wakati Serikali inaboresha miundombinu ya kiuchumi, uendelevu wake unategemea sana uzalendo na hali ya kujitegemea kwa Watanzania.”
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma amesema maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yanatoa fursa kwa vijana kukutana, kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu mbalimbali za uzalishaji mali na uzalendo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akioneshwa na Mbunifu kutoka Idara ya Vijana na Maendeleo Zanzibar Othman Ali Faki, kiatu ambacho kinachowasaidia watu wasioona kutambua vikwazo kilichopo mbele yake, wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Vijana kitaifa inayofanyika Mkoani Kagera, katika viwanja vya Gymkana Oktoba 12, 2022 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Naye, Waziri wa Nchi - Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako amesema Wiki ya Vijana kwa mwaka huu imelenga kuhamasisha ushiriki wa vijana katika kuleta maendeleo endelevu. “Vijana wanapaswa kutafakari kikamilifu ushiriki wao katika ujenzi wa uchumi wa Taifa hasa kipindi hichi ambacho Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amefungua fursa za kiuchumi na vijana wakiwa wanufaika wakuu.”