NA MWANDISHI WETU
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kutekeleza miradi yote ya kimkakati nchini na kwamba hakuna mradi wowote utakaokwama.

“Wale wenye mashaka kuhusu miradi hii, niwahakikishie hakuna mradi utakaokwama, miradi yote iliyoanzishwa na Serikali yenu ya Chama cha Mapinduzi itakuwa endelevu na itakamilika, miradi hii yote inalenga kuwanufaisha Watanzania na Rais Samia anaiendeleza miradi yote.”
Amesema kuwa ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati, Serikali imeendelea kuhakikisha hakuna mkandarasi yoyote atakayecheleweshewa malipo pindi anapotoa hati ya madai.
Aidha, Mheshimwa Majaliwa amewataka wakazi wanaoishi maeneo yanayozunguka miradi hiyo watumie fursa hiyo kuanzisha shughuli mbalimbali za kiuchumi zitakazowaletea maendeleo ikiwemo ujenzi wa nyumba za kulala wageni.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza kuhakikisha anaimarisha ulinzi katika maeneo yote yanayotekelezwa miradi ili kuzuia vitendo vya wizi wa vifaa mbalimbali ikiwemo saruji na nondo.

Kwa upande wake, Mhandisi Mshauri wa Ujenzi wa Daraja la Magufuli Abdulkarim Majuto amesema daraja hilo lenye urefu wa kilimota 3.2 litagharimu shilingi bilioni 716.333 na mpaka sasa limetoa ajira 885 kwa watanzania.
Naye, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Amina Lumuli amesema kuwa mpaka sasa ujenzi wa kipande cha Mwanza-Isaka ambacho kitaghrarimu shilingi trilioni 3.12 umefikia asilimia 14 hadi sasa. “Kipande hiki kitakuwa na stesheni 10 na kimeshazalisha ajira kwa Watanzania 5,400 na hadi kitakapokamilika kitatoa ajira 11,000.”