NA MATHIAS CANAL-WEST
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda ametoa onyo kwa uongozi wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kutokana na kitendo cha bodi hiyo kutotoa ushirikiano kwa kamati ya kuchunguza utoaji wa mikopo.
Waziri Mkenda ametoa onyo hilo Oktoba 25, 2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kusema kuwa Bodi inasuasua kutoa ushirikiano kwa kamati aliyoitangaza Julai 31, mwaka huu alipotembelea ofisi za bodi hiyo maeneo ya Tazara jijini Dar es salaam.
Waziri Mkenda ameeleza kuwa majukumu aliyoyatoa kwa kamati hiyo ilikuwa ni kuchunguza uhalali katika utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2017/2018 mpaka 2021/2022 ili kubaini kama kulikuwa na upendeleo wa utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wasiokuwa na sifa zilizoainishwa.
Prof. Mkenda amesema kuwa atakula kichwa cha mtu kama Bodi ya Mikopo itaendelea kusuasua katika utekelezaji wa kazi hiyo. “Mara wapite huku mara watokee huku lengo la timu hii tungependa kile kidogo tulichonacho kitolewe kwa haki kusaidia wale wenye mahitaji makubwa zaidi.
“Lakini pia kuhakikisha kwamba hakuna fursa ya mimi waziri, mtoto wangu au ndugu zangu wenye uwezo kuhakikisha wao wanapata kwa sababu wao wana connection wakati mtu ambaye hana connection hapati,” amesisitiza.
Waziri Mkenda ameonyesha masikitiko yake dhidi ya Bodi ya Mikopo (HESLB) na kueleza kuwa kamati hiyo imechelewa kufanya kazi yake kwa sababu ya ‘lobbying’ (inashawishi) huku na kule ilihali wakifahamu kwamba kamati ya waziri haisimamishwi kufanya kazi.
“Wasi-lobby na bodi ya mikopo nitawachukulia hatua wakiendelea kufanya lobby-lobby kwa sababu wanataka kutuambia na wenyewe wanataka kuficha mambo, ile kamati ifanye kazi, taarifa ni yetu tutaifanyia kazi kwa ndani kwa sababu sisi hatulengi kwenda kumuumbua sijui mtoto wa Salum amepata mkopo hapana.
“Sisi tunataka kujisahihisha ili kuhakikisha kwamba kile ambacho serikali imetenga kwa ajili ya mikopo kwa wanafunzi kinaenda kwa mlengwa, sasa ninataka kutoa onyo ya kwamba kwenda kulobby sijui eti waziri asimamishe kamati isifanye kazi… hiyo lobbying inaonesha kuna madudu.
“Natuma salamu kwa bodi ya mikopo kwa sababu niliona wamejaribu wanasema ooh tumeitwa sijui tumetuma tusimamishe wakati kazi nimeitoa mimi na mimi ndio nimepewa kazi ya kusimamia mikopo.
“Bungeni watu wanalalamika sana, wanasema kuna yatima hawapewi mikopo, halafu watu wenye uwezo wanapewa mikopo, mimi naunda kamati halafu nisikie kuna mtu anasema waziri asiunde kamati, aah! Nitakula kichwa cha mtu,”amesisitiza.
Kamati hiyo ya kufuatilia utoaji wa mikopo kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2017/2018 mpaka 2021/2022 aliyoitangaza Waziri Mkenda, inaongozwa na Profesa Allan Mushi ambaye ni mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe Morogoro, Idd Makame kutoka Zanzibar na Dk. Martin Chegeni ambao wote kwa pamoja ni wataalamu wa mifumo waliobobea katika sayansi ya kompyuta na takwimu.