NA MATHIAS CANAL
MBUNGE wa Jimbo la Rombo ambaye pia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe.Prof.Adolf Mkenda tarehe 1, Oktoba 2022 ameanza ziara ya kikazi ya siku tatu wilayani Rombo katika mkoa wa Kilimanjaro.
Katika siku ya kwanza ya ziara yake Waziri Mkenda amezundua kisima cha kuvuna maji ya mvua lita 100,000 kilichojengwa kwa ufadhili wa Engineers Without Borders pamoja na nguvu za wananchi.
Akizindua kisima hicho kilichogharimu kiasi cha shilingi milioni 63.970 ambapo shilingi milioni 5.0 ni nguvu za wananchi, Prof.Mkenda amewapongeza wananchi wa Kijiji cha Maki kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki shunghuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo ujenzi huo wa kisima.
Kadhalika, Waziri Mkenda ameshiriki mahafali ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Maki ambapo amewasisitiza wanafunzi hao kuwa Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan imeanzisha ufadhili kwa wanafunzi waliofanya vizuri kwenye masomo ya Sayansi ambao wamemaliza kidato cha sita na kudahiliwa na vyuo vikuu hapa nchini kusoma Sayansi, Uhandisi na Elimu tiba.
Ameeleza kuwa, ufadhili huo unaojulikana kama Samia Scholarship utagharamia wanafunzi 640 watakaokuwa na vigezo vilivyowekwa ambavyo ni pamoja na ufaulu wa kiwango cha juu.
Ametoa ufafanuzi kuwa ufadhili huo umepewa jina la Rais Samia ikiwa ni kutambua juhudi za kuimarisha Sekta ya Elimu katika maeneo ya Sayansi, Uhandisi na Elimu Tiba.
Pia Waziri Mkenda amesema kuwa wizara yake imetambua muktadha wa Rais Samia katika kuendeleza sekta ya elimu hivyo lengo la kuita jina la Rais Samia ni pamoja na maamuzi yake ya dhati ya kukubali kutoa ufadhili kwa wanafunzi hao.
Katika hatua nyingine Waziri Mkenda amesema kuwa, Rais Samia amefuta ada ya mitihani kwa wanafunzi wa kidato cha sita iliyokuwa mzigo kwa wazazi wengi nchini badala yake ada hiyo italipwa na serikali.
Pia Waziri Mkenda amesema kuwa serikali inaendelea kupitia mfumo wa utoaji mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kwa kipindi cha miaka mitano ili kubaini kama kulikuwa na udanganyifu au utoaji mikopo kwa wanafunzi wasiokuwa na sifa na vigezo vilivyowekwa.
Amesema, lengo ni kuimarisha utoaji wa mikopo na kuwanufaisha wanafunzi wengi wenye sifa za kupewa mikopo.