NA GODFREY NNKO
WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imesama, imedhamiria kushirikiana kikamilifu na benki zikiwemo kampuni mbalimbali za simu nchini ili ziweze kushiriki kufanikisha ukusanyaji wa kodi na tozo mbalimbali zitokanazo na Sekta ya Ardhi kidigitali.
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dkt.Allan Kijazi ameyasema hayo leo Oktoba 3, 2022 jijini Dar es Salaam wakati akifungua kikao kazi kilichowakutanisha wadau kutoka benki mbalimbali na kampuni za simu ambao watashiriki katika ukusanyaji wa maduhuli hayo.
Amesema, wizara imeamua kupanua wigo mpana wa kuzijumuisha benki na kampuni za simu ili kwa ukubwa wao wa kutoa huduma waweze kuwafikia wananchi wengi zaidi vijijini na mijini.
"Serikali imeanzisha mkakati madhubuti wa kuhakikisha kuwa, mapato yote yanayotokana na shughuli za kiserikali yanakusanywa kwa njia ya kielektroniki, tunatoka sasa kutoka katika mifumo ya kianalojia kwenda katika mifumo ya kielektroniki.
"Na ni kwa muktadha huo huo, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na yenyewe imejipana kikamilifu kuhakikisha kwamba kodi na tozo mbalimbali zinazohusiana na masuala ya Sekta ya Ardhi zinakusanywa kwa njia ya kielektroniki.
"Na katika kufanya hivyo, tumefungua akaunti na benki mbalimbali zilizopo hapa nchini. Na katika kutekeleza utartatibu huu na makubaliano ambayo tumefanya na benki tumeona kwamba kuna mafanikio makubwa,"amefafanua Dkt.Kijazi.
Changamoto
"Lakini, pamoja na mafanikio hayo pia tumeona kwamba kuna changamoto, changamoto kubwa ambazo tumeziona tumeona zipo mbili au tatu.
"Ya kwanza ni kwamba, mtandao wa mabenki kwa kiasi kikubwa upo katika majiji, miji na baadhi ya maeneo ambayo yako maeneo ya vijijini, lakini kwenye miji. Kwa hiyo mitandao ya kibenki haijafika kwenye maeneo ya vijijini.
"Lakini changamoto ya pili ambayo tumebainisha, ni kwamba bado uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kufanya na namna ya kufanya malipo ya miamala mbalimbali ambayo inahusu masuala ya ardhi ni mdogo, kwa hiyo wananchi wanahitaji elimu,
"La tatu ambalo tumelibaini ni kwamba,baadhi ya wadau wetu hawana uelewa wa kutosha kuhusu tozo mbalimbali na utaratibu unaotakiwa kutumika katika kulipa tozo hizo,"amefafanua Dkt.Kijazi.
Dhamira
"Ninaposema wadau ninamaanisha mabenki ambayo yanatusaidia kukusanya tozo hizo, sasa kwa vile nia yetu ni kusogeza huduma kwa wananchi, lakini pia kuhakikisha wananchi wanapata uelewa wa kutosha kuhusu taratibu na mifumo inayotumika kufanya makadirio ya kodi.
"Tumeona ni vema tukakutana wadau wote ambao tunahusika na utaratibu wa makusanyo ya kodi na tozo mbalimbali za serikali katika sekta ya ardhi ili tuweze kufanya majadiliano na kuangalia namna ya kuboresha mifumo ya utendaji ili tuweze kukidhi au kutatua changamoto hizo tatu,"amesema Dkt.Kijazi.
Matarajio
Dkt.Kijazi amesema, katika kufanya hivyo wanategemea benki zitawasaidia kutoa elimu kwa wananchi ili hamasa ya kulipa kodi na tozo zinazohusiana na Sekta ya Ardhi iwe kubwa.
"Kwa sababu sisi sote ni wanufaika, Serikali inanufaika kwa tozo ambazo tumeziweka, lakini pia benki zinapokusanya tozo hizo zinanufaika, kwa hiyo jukumu la kutoa elimu kwa wananchi lisibaki kuwa la wizara au la Serikali peke yake.
"Tunategemea wenzetu wa mabenki pia mtatusaidia kutoa elimu kwa wananchi ili hamasa ya kulipa kodi iwe kubwa, msiishie tu kusubiria wale wateja wachache wanaoelewa huduma mnazozitoa waweze kuja kulipa kodi na mkae mridhike, tunaelewa kwamba benki nyingi mna mifumo mizuri ya kidigitali, lakini pia mna mbinu nyingi za kutoa elimu kwa wananchi.
"Pamoja na kutumia huduma za kibenki, tutumie pia huduma za makampuni mbalimbali ya simu ili yaweze kutoa elimu kwa wananchi na yenyewe yaweze kuchangia kukusanya mapato ya Serikali, kwa hiyo tumeona ili kuondoa usumbufu kwa wananchi, suala la ulipaji wa kodi na tozo mbalimbali ya Sekta ya Ardhi zisishie tu kwenye mabenki au kwenye makampuni ya simu kwa maana ya ofisi zile ambazo zimefunguliwa na makampuni haya,kwa ajili ya shughuli za uendeshaji,"amesisitiza Dkt.Kijazi.
Mawakala
"Tunategemea pia kwamba, benki na makampuni ya simu mtatusaidia kutoa elimu kwa mawakala mbalimbali ambao wamesambaa hadi vijijini ili mawakala hao wenyewe, nao wawe na uelewa wa kutosha kuhusu utaratibu unaotumika katika kupanga ua kufanya mahesabu mbalimbali ya kodi au ya tozo mbalimbali.
"Lakini ili tuweze kufanikiwa kama nilivyosema, lazima wote tuwe na uelewa wa pamoja, wakusanyaji tuwe na uelewa wa pamoja , lakini wale ambao wanalipa kodi pia waweze kuwa na uelewa na watimize wajibu wao kama watanzania ambao wanawajibika kulipa kodi kwa huduma mbalimbali za kiserikali.
"Kwa hiyo tukishikamana kwa pamoja nina imani kwamba tutaweza kufanikisha sekta ya ardhi kukusanya kodi ya kutosha na iweze kutoa mchango wake kwa Taifa kama ilivyokusudiwa,"amebainisha Dkt.Kijazi.
Tathimini
Katika hatua nyingine,Dkt.Kijazi ameongeza kuwa, ili kuwezesha mkakati huo kuwa na matokeo bora zaidi watakuwa wanafanya tathimini ya kila mwaka ambayo itakuwa inatambua mdau anayetoa mchango mkubwa katika kufanikisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali kupitia Sekta ya Ardhi.
"Hivyo, katika kufanya hivyo Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi itatoa hamasa kwa benki na mitandao ya simu ambayo itakuwa imefanywa vizuri,nadhani hiyo itakuwa njia nzuri ya kukuza mapato ya nchi na kutambua mchango wenu,"amebainisha Dkt.Kijazi.
Pia amesema, utaratibu huo utaendelea hivyo hivyo kwa halmashauri na mikoa ambayo inafanya vizuri katika ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kupitia Sekta ya Ardhi ambapo motisha zitatolewa ili kuongeza ari na ufanisi zaidi kwa kila mmoja.
Makusanyo
Wakati huo huo, Dkt.Kijazi amesema kuwa,mapato ya ardhi yanayolipwa kupitia miamala mbalimbali bado yako chini huku wakiwa na matarajio kuwa, kupitia hamasa na elimu kwa wananchi itaweza kupaisha makusanyo hayo.
Dkt.Kijazi amesema,kupitia ushirikiano huo na wadau inaweza kukusanya mara tatu zaidi ya lengo ambalo imejiwekea la shilingi bilioni 200 kwa sasa.
Amesema, mkutano huo ambao unahusisha majadiliano utafungua ukurasa mpya katika kutoa elimu kwa wananchi ambao wengi wao wanamiliki ardhi, lakini huwa hawalipii kodi au tozo zozote nchini.