Yanga, Simba SC watambiana 'atapigwa mtu kama ngoma' Derby hii

NA DIRAMAKINI

SAA zikiwa zinahesabika kuelekea katika mchezo wa Simba na Yanga SC, wadau wa soka wameshiriki katika mkutano wa Zoom leo Oktoba 21, 2022 na kutoa mwelekeo.
Mkutano huo ambao umeratibiwa na Wacht Tanzania na kurushwa na vyombo mbalimbali vya habari ulikuwa unaongozwa na mada inayosema Kuelekea katika mchezo wa Simba na Yanga nani Mbabe: Washiriki wamesema:

AHMED ALLY, AFISA HABARI WA KLABU YA SIMBA

"Tunakwenda kwenye mchezo huu tukiwa tumekamilika kila eneo, hatuna majeraha ya mchezaji yeyote mechi yetu ya mwisho dhidi ya De Agosto, Okrah na Tshabalala kidogo walitolewa kwa sababu walianza kujisikia maumivu, lakini wamepatiwa matibabu na wenyewe ni sehemu ya kikosi ambao wamefanya mazoezi yote na leo wapo mazoezini.
"Mchango wa online media ni mkubwa sana, kwa sababu tunafahamu dunia imehamia kiganjani, nguvu ya smartphone ambazo watu wengi wanazimiliki ni nadra sana kumkuta mtu anaangalia Tv kwa siku za hivi karibuni kila kitu kinaishia kwenye simu yake ya mkononi.
"Leo unaweza kuitisha mkutano na waandishi wa habari na usione Mainstream yeyote usiione ITV, TBC, Star TV na wala hauna mashaka na huo mkutano kwa sababu una uhakika zile online platform ambazo ziko pale zitafikisha ujumbe wako Tanzania nzima na Duniani bila kutumia mainstreams.
"Uwepo wa online tv ni chachu kubwa sana kwetu sisi na tunatamani ziendele kuongezeka ili ziweze kuwafikia watu wengi zaidi na suala la kupunguza gharama za usajili maana ni kwamba wengi watamudu kuzimiliki, kuziendesha na dhana ya kuwa na online media nyingi itakuwa imefikiwa,"amesema.

ALLY KAMWE, AFISA HABARI WA KLABU YA YANGA

"Tanzania tuna fursa kubwa sana ya kuitumia Kariakoo Derby kuitengenezea thamani ili mchezo huu uvutie watu wengi, kuna watu wengi wanaingia Tanzania kwa sababu ya Kariakoo Derby na hii kutokana na upekee iliyonayo.
"Kimsingi huu ni mchezo ulioshikilia brand ya mpira wetu na hii ipo kwenye kila nchi, kuna mchezo mmoja ambao umeshikilia brand ya mpira wa hiyo nchi kwa hiyo natamani juhudi ambazo serikali imezifanya kwa kutoa fursa kwa wawekezaji kwenye mpira sisi wadau wa michezo tusitengeneze mazingira ya watu kuona kumbe kuna kingine chenye thamani kuliko Kariakoo Derby.
"Yanga haijiandai kwa sababu ya kumfunga Simba bali inajiandaa kwa sababu ya kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC,"amesema.

AGGY SIMBA, SHABIKI WA KLABU YA SIMBA

"Tunajua Yanga wametusumbua sana miaka ya hivi karibuni na kwa kweli inatuumiza kweli sisi kama mashabiki, lakini safari hii tumesema dawa yao tumeipata tutapambana na nyie kwa namna yeyote ile na Jumapili tutaibuka na ushindi.
"Yanga msijiamini kiasi hicho msijibebe kiasi hicho kwa sababu tu mna matokeo mazuri dhidi ya Simba siku za karibuni kwenye mpira chochote kinatokea na kuweza kubadilika.

"Sisi Simba tunawaheshimu Yanga, tunajua kweli mnapambana na Simba ndiyo maana haswa mkitoka nje ya Tanzania hamfanyi kitu chochote na hamna chochote mnabaki kujivunia tu magoli ya hatua za awali na hayawasaidii wala kuwafikisha mahali.

"Safari hii tunataka kuwaonesha kwamba furaha yenu ambayo mnataka kuitafuta kwa Simba sisi tunawaambia furaha hamuwezi kuipata wala kupooza machungu ya kutolewa na Al hilaly sisi tutaongeza pale pale na tutapiga pale pale kwenye mshono kabla haujapona tunaufumua vile vile,"amesema.

JIMMY KINDOKI, SHABIKI WA KLABU YA YANGA

"Nimerelax kwa maana nikiangalia historia inaibeba Klabu ya Yanga kama ubora, lakini nikiwatazama wapinzani wetu naona kabisa kuna namna wanaitafuta furaha ambayo haihusiani na hii Derby wanajaribu kuchukua mafanikio ya sehemu nyingine wanayaleta kwenye Derby.

" Nikiangalia wenzetu naona kabisa wameshakosea namna ambavyo wameuchukulia huu Mchezo wa Derby,"amesema.
"Ukichukua siku 365 na robo ukizizidisha kwa miaka mitatu unaona kabisa ni kwa namna gani hawa Simba wamekuwa wakipata shida kwenye kuutafuta ushindi wanapocheza na Yanga.
"Klabu ya Simba kiasili na kihistoria imetokana na Yanga ndio wazazi wa hii klabu kuna watu wakati huo walijiondoa kwenye timu yetu wakaanzisha timu yao ndo wakaitengeneza Simba kwahiyo sisi tunawafahamu vizuri kuliko wao wanavyotufahamu sisi,"amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news