Afrika Kusini yasogeza fursa za kiuchumi Tanzania kupitia Sekta ya Sanaa na Utamaduni

NA GODFREY NNKO

MSIMU wa utamaduni kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Afrika Kusini umeanza rasmi leo huku fursa mbalimbali za kiuchumi zikitarajiwa kupatikana kupitia Sekta ya Sanaa na Utamaduni nchini.

Hayo yamesemwa leo Novemba 18, 2022 jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, Bw.Saidi Yakubu wakati akizungumzia kuhusu kuanza kwa msimu huo ambao unatarajiwa kwenda sambamba na matukio mbalimbali.

Mbali na Nocawe Noncedo Mafu ambaye ni Naibu Waziri wa Michezo na Burudani, Sanaa na Utamaduni wa Jamhuri ya Afrika Kusini pia Naibu Katibu Mkuu, Yakubu aliambatana na maafisa waandamizi kutoka serikalini, wakiwemo ubalozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania.

"Moja wapo ya faida ya msimu huu ni kukuza diplomasia ya nchi zetu na na kuikumbuka historia ya ukombozi wa Bara la Afrika.

"Kupitia onesho hili la sanaa, hata wasanii wetu watanufaika kwa kupata ajira za muda na pia kupitia maonesho ya kazi za sanaa, utamaduni na ubunifu pia wasanii wetu watapata fursa ya kuuza na kuonesha baadhi ya kazi zao za mikono na pia kuimarisha ushirikiano wa sekta zetu za utamaduni, sanaa na michezo na hii ni sehemu ya utekelezaji wa Mkataba wa Utamaduni ambao ulisainiwa mwaka 2011.

"Wasanii pia watabadilishana uwezo wa kufanya kazi za sanaa na ubunifu, kuimarisha mbinu na kujifunza mbinu ya uhifadhi na uendelezaji wa tekeknolojia ya ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika.

"Vile vile, msimu huu wa utamaduni wa Afrika Kusini utafungua madirisha ya uwekezaji wa biashara katika sekta ya utamaduni, sanaa na michezo,"amesema Bw.Yakubu.

Naibu Katibu Mkuu, Yakubu amesema katika wiki hii ya maadhimisho ya utamaduni wa Afrika Kusini leo ndio ufunguzi rasmi ambapo utafanywa na Mheshimiwa Waziri Mohamed Mchengerwa kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa.

"Kutakuwa na burudani nyingi na vikundi vingi kutoka Afrika Kusini ukumbi wa Mlimani City. Tunatarajia watu 1,000 watakuwepo katika uzinduzi huu. Baada ya hapo wataelekea Morogoro ambako kutakuwa na mhadhara kwa umma watapiga picha ambayo inazungunzia mchango wa Tanzania katika ukombozi wa Afrika Kusini kesho katika Ukumbi wa Mandela katika Kampasi ya Solomon Mahlangu iliyopo Mazimbu Chuo Kikuu cha Sokoine na hii itakuwa saa 11:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni.

"Na kutakuwa na wahadhiri mbalimbali wa ndani na nje ya nchi wakizungumzia mchango wa Tanzania katika ukombozi wa Afrika Kusini, watetembelea maeneo ya historia ya ukombozi wa Afrika Kusini ambayo yapo hapa Tanzania, mengine yapo Kinondoni Mkoa wa Dar es salaam, mengine yapo Kongwa mkoani Dodoma ambapo pia watatembelea huko tarehe 21 mwezi Novemba 2022.

"Na baada ya hapo kutakuwa na ufunguzi wa tamasha la maonesho ya filamu kuanzia tarehe 22 hadi 27 yatakuwa yanafanyika katika Ukumbi wa Makumbusho. Siku zote hizo kutakuwa na filamu kuanzia saa 12:00 jioni na siku zote hizi kutakuwa na filamu za Afrika Kusini zikioneshwa katika eneo hilo,"amefafanua Bw.Yakubu.

Katika hatua nyingine amebainisha kuwa, kutokana na sekta ya sanaa, utamaduni na michezo kuwa na fursa kabambe za kiuchumi pia kutakuwa na semina kuhusu biashara.

"Lakini pia siku hizi michezo, sanaa na utamaduni ni biashara kwa hiyo kutakuwa na semina kuhusu biashara na kazi za sanaa, kwa hiyo hii njia nyingine ya kupata uzoefu kutoka kwa wenzetu wa Afrika Kusini.

"Semina ambayo itafanyika tarehe 23 Novemba katika Ukumbi wa Makumbusho kuanzia saa 3:00 hadi saa 7:00 mchana, lakini vile vile kutakuwa na uzinduzi wa picha za kuchora ambazo zina ujumbe wa ukombozi katika jengo ambalo likikuwa linamilikiwa na Kamati ya Ukombozi hapa hapa Dar es Salaam karibu na Ubalozi wa Msumbiji,"amefafanua Bw.Yakubu.

Pia amesema kuwa, "Lakini pia kutakuwa na uzinduzi wa tamasha la ngoma za asili za Tanzania na Afrika Kusini ambayo itafanyika pia katika eneo la Makumbusho tarehe 25 Novemba, 2022 hii sasa itakuwa jioni.

"Halafu tamasha hili litafungwa Zanzibar, tunategemea mmoja wa viongozi wakuu wa Zanzibar atakuwa mgeni rasmi hiyo itakuwa tarehe 27, kuanzia saa 4:00 asubuhi mpaka saa 10:00 jioni. Baada ya hapo watarejea Dar es Salaam ambapo tarehe 2 hadi 4 Desemba 2022 watakuwa na fasheni shoo au onesho la mtindo na mavazi la Afrika Kusini hili linaendana na wiki ya mavazi ya Mswahili na wao watajiunga kwa hiyo karibuni sana katika moja ya maeneo haya," amesema Bw.Yakubu.

Kwa upande wake, Nocawe Noncedo Mafu ambaye ni Naibu Waziri wa Michezo na Burudani, Sanaa na Utamaduni wa Jamhuri ya Afrika Kusini amesema,Taifa hilo lina mambo mengi ya kujivunia kutoka Tanzania ambayo yamejengwa katika historia ya kipekee kuanzia ukombozi wa Bara la Afrika hadi leo.

Mheshimiwa Mafu amefafanua kuwa,Sekta ya Sanaa, Michezo na Utamaduni ina fursa nyingi za kiuchumi ambazo zikiratibiwa vema kama lilivyokusudi la Serikali zote mbili itafungua fursa nyingi za kiuchumi ikiwemo ajira kwa makundi mbalimbali ya wananchi.

Amesema, tamasha hilo linalenga kukuza uhusiano wa Tanzania na Afrika ya Kusini,kudumisha na kukuza utamadani na kubadilishana uzoefu.

"Nchi hii kwetu sisi ni kama nyumbani kwetu,Afrika Kusini na Tanzania ina uhusiano wa kihistoria tokea zamani,Mwalimu Julius Nyerere alipigana kwa hali na mali kuhakikisha Afrika Kusini inapata uhuru wake,"amesema Naibu Waziri huyo.

Pia ameongeza kuwa, licha ya burudani zitakazotolewa kwenye msimu wa tamasha hilo kutakuwa na semina ya biashara ya kazi za sanaa ikiwemo muziki, maonesho ya filamu,maonesho ya picha za kuchora kutoka Afrika ya Kusini.

"Tunategemea tamasha hili litaimarisha mahusiano yetu,baina ya nchi zote mbili na watu wake, kufanya utalii,kukuza diplomasia,wasanii kupata uzoefu na fursa mpya pamoja na kukuza uelewa wa sanaa na biashara,"ameongeza Mheshimiwa Naibu Waziri Mafu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news