NA DIRAMAKINI
WANANDOA Agapiti Kimaro na Catherine Mathei ni miongoni mwa watu saba waliofariki katika ajali ya gari iliyotokea Pori Namba Moja lililopo Kata ya Partimbo wilayani Kiteto mkoani Manyara.
Agapiti ambaye ni Mkuu wa Shule ya Esamatwa huku Catherine akiwa muuguzi wilayani hapa wameacha mtoto wa miezi nane.
Wengine waliofariki katika ajali hiyo iliyotokea Novemba 7,2022 saa 12:58 jioni katika eneo hilo ni Joseph Bizuku na Kadidi Saidi ambao wote ni wauguzi. Pia kuna madaktari wawili ambao ni Edward Makundi na Nickson Mhongwa pamoja na mtumishi wa maabara Celina Nyimbo.
Majeruhi waliopo katika Hospitali ya Dodoma wakipatiwa matibabu ni dereva wa gari hilo la wagonjwa lililopata ajali Juma Mbaruku (45) na dereva wa Prado, Method Malick (55) huku majeruhi wengine Ibrahim Selemani (71) na Mbaraka Shabani (44) wakilazwa katika Hospitali ya Kiteto.
Hayo yamethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, RPC George Katabazi ambapo amesema,miongoni mwa watu hao alifariki dunia baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Dodoma kwa ajili ya matibabu zaidi baada ya kutolewa katika Hospitali ya Kiteto.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Mbaraka Batenga ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama akiwa Hospitali ya Kiteto alisema ajali hiyo ilihusisha gari la wagonjwa la Kituo cha Afya Sunya lililokuwa limepeleka mgonjwa Hospitali ya Wilaya ya Kiteto likirudi likiwa limebeba watumishi kurejea eneo la kazi Sunya liligongana uso kwa uso na gari dogo aina ya Prado likitokea barabara ya Kilindi mkoani Tanga kuja Kiteto.