Azam FC yawachomoa Simba SC nafasi ya pili saa chache baada ya kicheko

NA DIRAMAKINI

AZAM FC imeendelea kuvuruga dili la Wekundu wa Msimbazi, Simba SC ya jijini Dar es Salaam kutaka kwenda kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara baada ya kutembeza kichapo kwa Coastal Union.

Simba SC ilifanikiwa kukaa nafasi ya pili kwa saa chache leo Novemba 27, 2022 baada ya kuitandika Polisi Tanzania mabao matatu kwa moja katika dimba la Ushirika lililopo Moshi mkoani Kilimanjaro.

Matokeo yaliyoifanya Simba SC kufikisha alama 31 katika mchezo wa 14 ikizidiwa pointi moja tu na mabingwa watetezi, Yanga ambao wana mechi mbili mkononi.

Aidha, Azam FC wakiwa wenyeji leo Novemba 27, 2022 wameibuka na ushindi wa 3-2 dhidi ya Coastal Union ya jijini Tanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara usiku huu katika Dimba la Azam Complex lilopo Kata ya Chamazi Halmashauri ya Manispaa ya Temeke,Dar es Salaam.

Mabao ya Azam FC yamefungwa na James Akaminko dakika ya 56, Yahya Zayd dakika ya 70 na Iddi Nado zaidi ya dakika 90.

Aidha, kwa upande wa Coastal Union mabao yao yamefungwa na Maabad Maulid dakika ya 14 na Hamad Majimengi dakika ya 18.

Matokeo hayo yanaifanya Azam FC kufikisha alama 32 katika mchezo wa 14 na kurejea nafasi ya pili ikizidiwa tu wastani wa mabao na mabingwa watetezi, Yanga SC ambao pia wana mechi mbili mkononi.

Wakati huo huo, kwa upande wa Wagosi wa Kaya, Coastal Union baada ya kichapo cha leo Novemba 27, 2022 wanabaki na alama zao 12 za mechi 12 nafasi ya 12 ya msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news