Baraza la Mawaziri latoa maagizo uchunguzi ajali ya ndege Ziwa Victoria

NA DIRAMAKINI

BARAZA la Mawaziri limewaelekeza wataalamu wa ndani kushirikiana na wataalamu kutoka nje ya nchi kufanya uchunguzi kuhusu ajali ya ndege ya Precision Air iliyotokea Novemba 6, 2022 ili kupata chanzo cha ajali na mapendekezo ya hatua zitakazochukuliwa.

Hayo yamesemwa leo Novemba 14,2022 na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa wakati akizungumza baada ya kikao cha dharura cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma na kuongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Msigwa amesema, baraza hilo limetoa maelekezo hayo kwa kuzingatia kuwa Tanzania imetiliana saini katika mikataba mbalimbali ya kimataifa ambayo inasimamia usafiri wa anga na hatua zinazopaswa kuchukuliwa mara baada ya ajali ya anga kutokea.
“Baraza limeelekeza vitengo vyote vinavyohusika na kukabiliana na majanga viimarishwe kwa namna mbalimbali ambazo zitatuwezesha sisi kama nchi kuongeza uwezo zaidi ya tulionao sasa katika kukabiliana na majanga pale yanapotokea.

"Na tutamaliza na ripoti kamili ambayo inatolewa ndani ya miezi 12 baada ya ajali kutokea, hatua hizi zote tayari zimeshaanza,”amefafanua.

Pia Msigwa ametaja hatua tatu zinazofanyika katika uchunguzi ikiwemo timu ya uchunguzi ya ajali ya ndege ambayo inafanya uchunguzi wake na kutoa maelezo ya awali ndani ya siku 14, inafuatiwa na ripoti ya awali ambayo inatolewa ndani ya siku 30.

Msemaji huyo amewataka wananchi kuendelea kuwa watulivu wakati uchunguzi huu unafanyika na baada ya uchunguzi kukamilika watajulishwa.

Wakati huo huo, Baraza la Mawaziri limewashukuru na kuwapongeza wote waliohusika katika uokozi baada ya ajali hiyo kutokea.

Katika ajali hiyo ambayo ilianguka Ziwa Victoria karibu na Uwanja wa Ndege wa Bukoba mkoani Kagera siku ya Jumapili, Novemba 6, mwaka huu ilisababisha vifo vya watu 19 wakiwemo abiria na wahudumu huku zaidi ya 20 wakinusurika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news