BREAKING NEWS: Waasi wa Al-Shabab washambulia hoteli ya Mogadishu inayotumiwa na maafisa wa Somalia

NA DIRAMAKINI

WAPIGANAJI wa kundi lenye silaha la al-Shabab wameshambulia hoteli inayotumiwa na maafisa wa Serikali katika mji mkuu wa Somalia wa Mogadishu.

Hayo ni kwa mujibu wa afisa wa polisi na maafisa wa serikali leo Novemba 27, 2022 huku maafisa wa usalama wakisema kuwa watu hao wenye silaha walikuwa wamevalia fulana za kujitoa mhanga.

Bado hakukuwa na taarifa zozote kuhusu majeruhi katika shambulizi hilo la hivi punde lililodaiwa na kundi la al-Shabab. Baadhi ya mashirika ya habari ikiwemo Al Jazeera hayakuweza kuthibitisha kwa kina madai kwamba lilikuwa shambulio la kujitoa mhanga.

Washambuliaji hao walivamia hoteli ya Villa Rose, iliyo karibu na Ikulu ya Rais, wakiwa na vilipuzi na bunduki, alisema afisa wa polisi Mohammed Abdi leo Novemba 27, 2022. Haijabainika mara moja ni washambuliaji wangapi, alisema.

Baadhi ya maafisa wa serikali katika Hoteli ya Villa Rose waliokolewa baada ya kutumia madirisha kutoroka, alisema Mohammed Abdi, mmoja wa maafisa wa polisi.

Waziri wa Mazingira, Adam Aw Hirsi, aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba alikuwa salama baada ya mlipuko huo wa kigaidi uliolenga makazi yake katika hoteli, ambapo maafisa wengi wa serikali hukaa.

"Tulitikiswa na mlipuko mkubwa, ukifuatiwa na majibizano makubwa ya risasi,"amesema Ahmed Abdullahi, anayeishi karibu na eneo la tukio.

"Tuko ndani tu na tunasikiliza milio ya risasi." Shambulio hilo linakuja wakati al-Shabaab wakizidisha mashambulizi nchini Somalia, huku takribani watu 100 wakiuawa katika milipuko miwili ya magari katika mji mkuu wa Somalia Oktoba 30, mwaka huu.

"Watu wetu waliouawa kikatili ... ni pamoja na mama na watoto wao mikononi mwao, baba ambao walikuwa katika matibabu, wanafunzi waliopelekwa kusoma, wafanyabiashara ambao walikuwa wakihangaika na maisha ya familia zao," Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud alisema baada ya kutembelea eneo la mlipuko Oktoba 30, mwaka huu.

Aidha, takribani watu 21 waliuawa mwezi Agosti, mwaka huu wakati al-Shabab waliposhambulia hoteli moja mjini Mogadishu. Kundi hilo lililojihami pia lilidai kushambulia hoteli moja katika mji wa Kusini wa Kismayo mwezi uliopita na kusababisha vifo vya watu tisa.

Al-Shabab, kikundi chenye silaha chenye mafungamano na al-Qaeda kinachopigana nchini Somalia kwa zaidi ya muongo mmoja, kinataka kupindua serikali kuu ya nchi hiyo na kuanzisha utawala wake kwa kuzingatia tafsiri kali ya sheria za Kiislamu.

Kundi hilo linatumia kampeni ya milipuko ya mabomu nchini Somalia na kwingineko, na malengo yamejumuisha mitambo ya kijeshi pamoja na hoteli, vituo vya ununuzi, na maeneo yenye shughuli nyingi za magari.

Wapiganaji wake walifukuzwa kutoka Mogadishu mwaka 2011 na vikosi vya Kulinda Amani vya Umoja wa Afrika. Lakini bado wanadhibiti maeneo ya mashambani ya Somalia na wameongeza mashambulizi tangu Rais Mohamud aingie madarakani mwezi Mei na kuahidi kutekeleza vita vya kila namna dhidi ya kundi hilo.

Rais Mohamud akiungwa mkono na Marekani na wanamgambo washirika wa ndani, ameanzisha mashambulizi dhidi ya kundi hilo, ingawa matokeo yamekuwa madogo.(Mashirika)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news