BUNDI WA GAMBOSHI SEHEMU YA 55

NA WILLIAM BOMBOM

Ilipoishia...siku moja tulialikwa kwenye kikao cha wachawi wa mji wa Nguruka. Kikao hicho kilifanyika kweye uwanja wa shule ya msingi Nyangabo, kikao hicho kikihudhuriwa na wachawi wachache sana kulingana na unyeti wake...

Endelea

Kwa kuwa kutoka mji wa Majengo ilipo kambi yetu mpaka uwanja wa shule ya msingi Nyangabo haikuwa mbali niliamua kutumia usafiri wa upepo.

Kabla ya kwenda kwenye kikao hicho, nilifanya maandalizi ikiwa ni pamoja na kuangalia njia. Miongoni mwa watu walio makini katika shughuli zao ni pamoja na wachawi.

Kazi ya kichawi haitofautiani sana katika umakini na mafundi umeme, kosa moja hupelekea kupoteza uhai wa mtu. Nilitazama njia na kubaini hakukuwa na shida.

Nilitoka kambini kwetu mida ya saa tano usiku, wakati naelekea kikaoni njiani nilikutana na wanga wengi wakiendelea na shughuli zao.

Kutoka kambini nilikamata njia ya bohari la tumbaku kisha nikanyoosha mpaka sheli ya issa. Baada ya hapo nilipinda kulia nikanyoosha njia inayopita shule ya msingi Umoja.

Nilipofika soko la Bweru niliendelea kulifuata barabara kuu hadi kanisa la shika neno tenda neno kisha nikapinda kushoto.

Nilipovuka kwa Emma niliachana na barabara iendayo soko la Nguruka kupitia msikiti, nilinyoosha huku nikipapita posta, kituo cha afya na mawasiliano. Punde si punde nikawasili kwenye kikao hicho, kilikuwa ni kikao cha washirika wachache.

Kabla ya kuingia kwenye viunga vya uwanja wa shule hiyo,THE BOMBOM nilianza kubanwa kifua. Katika uzoefu wangu wa kazi hii, kubanwa kifua ni ishara mbaya.

Ni ishara inayoonesha uwepo wa nguvu nyingine kinzani ya madawa inayotoka nje. Niliamua kurudi nyuma ili kujipanga zaidi, pale uwanjani kulikuwa na wachawi wachache walioonekana kulala usingizi wa pono.

Hii pia ilinifanya kushituka, maana siyo kawaida kwa wachawi kusinzia katika maeneo ya kazi. Yamkini hapa kulikuwa na tatizo, tena kulikuwa na tatizo lililotakiwa ufumbuzi haraka. Wakati nikiwa pembeni ya uwanja huo, ghafla niliwaona wachawi wawili hewani wakiwa kwenye ungo.

Haikuwa tabu kuwatambua kwa maana sisi wachawi tunajuana. Ule ungo ukiwa hewani, ulipoingia tu kwenye eneo la uwanja huo wa shule ya msingi Nyangabo ulianza kuporomoka.

Hili lilikuwa geni machoni mwangu, kuporomoka kwa ungo kwetu ilikuwa ni tukio la fedheha. Kupitia hili ndipo hisia zangu nilibaini zilikuwa za kweli, hata hivyo niliendelea kujiuliza kwa nini tukio hili sikuliona mwanzo wakati nafanya maandalizi ya kuja kwenye kikao? Baada ya kuwaza na kuwazua jibu lililoniijia kichwani lilikuwa ni kuzidiwa kwa ujuzi wa madawa.

Wale wachawi wenzangu walipinduka na ungo wao na kuumia vibaya. Tayari nilibaini kuwa pale uwanjani palikuwa pamefanyiwa mizungu. Kila mchawi aliyeshuka eneo hilo alipata ajali iliyopelekea kuumia.

Jambo hilo halikuwa zuri niliamua kurudi kambini haraka ili kwenda kujipanga, niliogopa kuingia kichwa kichwa kwenye mziki huo.

Nilipofika kambini badala ya kufanya kazi iliyonipeleka nilijikuta nimeshikwa na usingizi nikalala usingizi mzito.

Hapa nikiri tu kuwa nguvu iliyokuwa nyuma ya pazia ilikuwa imara,THE BOMBOM nilielekea kuzidiwa ujanja. Nilishituka asubuhi na mapema, taarifa nilizokutana nazo toka kwa wachawi wenzangu zilinichanganya zaidi.

Kulikuwa na tukio la wachawi kushindwa kuondoka kwenye uwanja wa shule ya msingi Nyangabo. Asubuhi hiyo watu walimiminika eneo hilo kwenda kushuhudia tukio hilo la kihistoria.

Ulikuwa ni udhalili wa hali ya juu, tayari nilikuwa nimeshabaini uhusika wa mganga huyu kwenye tukio hilo. Hakika mganga huyo alikuwa mwiba ulioshika vyema kooni mwetu, kwa kuwa alikuwa ameanzisha vita bila kinyongo niliipokea.

Wakati nikitafakari njia sahihi za kumshughulikia ndipo tunabaini kuwa mganga huyo ndiye aliyehusika kumzuia fundi kuja kujenga.

Mganga huyo alionekana kuwa jeuri, hakuogopa jambo lolote toka kwetu. Silaha yake kubwa ilikuwa ni kutufanya wachawi kusahau matukio hayo haraka vichwani mwetu.

Kupitia matukio hayo,THE BOMBOM nilihapa kumshughulikia mganga huyo kwa hali na mali. Waganga wa namna hii huwa ni mwiba kwa jamii ya kichawi, huwa hawakubali hata kutuachia watu wetu endapo wamekimbilia kwao.

Ndiyo maana yule kijana alikimbilia hapo, hata huyu fundi kakimbilia hapo kwa kujua mazindiko yaliyopo nyumbani hapo tusingeweza kuingia.

Kupitia matukio hayo nilianzisha vita dhidi ya mganga huyo, niliweka mitego yangu vyema nikitafakari eneo nitakalomuumiza mganga huyo.

Maana tulipojaribu kuingia nyumbani kwake ilishindikana, aliweka zindiko lisilopitika kwa namna yeyote. Tukajaribu kutafuta mate, mkojo, kinyesi, machozi au nywele zake tukabaini kavizindika.

Mganga huyu alikuwa kiboko alionekana kujidhatiti vilivyo vyema. Hatimaye tukapata mbinu nyingine, tulimtegeshea mwanamke mzuri tuliyekuwa tumemlipa ujira mzuri ili amtongoze.

Yule mwanamke alikuwa siyo mchawi bali ni mtoto wa mchawi mwenzetu. Lengo la kumtuma mwanamke huyo ilikuwa ni kumruhusu afanye mapenzi na mganga huyo kisha atuletee shahawa za mganga huyo.

Hapa niseme kidogo, wachawi huwa tuna njia nyingi za kumpata hasimu wetu. Kupitia shahawa alizotembea na mwanamke huyo bila kutumia mpira, tungeweza kummaliza mganga huyo. Kwa kuwa kulikuwa na donge nono kwa mwanamke huyo, aliingia kazini kumsaka mganga huyo ili atimize malengo yake.

Waswahili walisema "hakuna mkate mgumu mbele ya chai". Baada ya muda mganga alinasa, maana wapo wachawi waliokabidhiwa jukumu la kumfuatilia mwanamke huyo. Walifuatilia mienendo yake toka asubuhi mpaka jioni pasipo yeye kuwabaini, nimeshasema yeye hakuwa mchawi hivyo asingeweza kuwaona wachawi.

Tulikuwa tumempa maelekezo ya kuwa mara tu baada ya kufanya ngono na mganga huyo alipaswa kujisafisha kwa kitambaa fulani tulichompa.

Kisha kitambaa hicho angetuletea kwa ajili ya shughuli zetu, tungetumia shahawa zake mganga huyo kumshikisha adabu.

Hapa niseme kidogo, mchawi anaweza kukuloga kupitia kivuli ama jasho lako na akakuchukua kirahisi. Anaweza kukuloga kupitia kipande cha nguo zako au kupitia mate yako. Hivyo ni vigumu kumkwepa anapokuwa anakutafuta.

Siku ikafika ya mwanamke huyo kukutana na mganga huyo ili kuvunja amri ya sita. Haya ndiyo maradhi makubwa ya mganga huyo, ndiyo maana tulimtegeshea mtoto chombo.

Kwa kuwa mganga alikuwa na wake wawili nyumbani kwake, aliamua kumpanga vichakani mama wa watu. Siku zote wazinzi mashuhuru huwa hawatumii nyumba za kulala wageni.

Vichakani, viwanja vya shule, madarasani, porini au kwenye mapagala ndiyo sehemu sahihi kumfanyia ufusika wao.

Yule mwanamke tayari alikuwa ameshatutaarifu juu ya miadi hiyo na mahala watakapokutana. Kulingana na uwezo wa madawa ya mganga huyo.

Siku hiyo tulikuwa makini asituone kama tulikuwa tukimfuatilia. Tuliwahi kufika eneo la tukio na kujificha kichakani, aliyefuatia kufika ni yule mwanamke akaenda kukaa kwenye kichaka kilichokuwa mbali kidogo na tulipokuwa sisi.

Ghafla tulimuona mganga akija kwa kunyata kama dume la nyani. Uso wake ulikuwa na furaha isiyo kifani, alikuwa kavaa koti na msuli wapambanaji nadhani mnanielewa.

Hakuweza kubaini uwepo wetu maeneo hayo, yule mwanamke alimuita maana mganga alikuwa hajamuona. Ile sauti ilimnyong'onyeza mganga huyo, ilikuwa ni sauti ya kumtoa nyoka pangoni. Haki ya nani wanawawake ni viumbe hatari, yaliyokuwa yanakwenda kumkuta mganga huyo ni siri yetu. Ghafla...

Mambo ndiyo yanaiva, mganga kaingia kwenye kumi na nane za THE BOMBOM, je atachomoka?

Endelea kujiandaa kusoma simulizi ya KANISA LA KICHAWI na KABURI LA RAIS WA HOVYO ambazo zitakuwa zinatumwa kila juma mara mbilimbili.

WABONYE?

THE BOMBOM

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news