Costa Rica yaficha aibu ya mabao 7-0 kwa Japan katika Kombe la Dunia

NA DIRAMAKINI

BAO la dakika ya 81 lililofungwa na Keysher Fuller limeiwezesha Costa Rica kuibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Japan na kuziacha timu zote mbili zikiwa na alama tatu baada ya michezo miwili ya Kundi E la Kombe la Dunia.

Keysher Fuller wa Costa Rica akifurahi ushindi wa bao pekee aliloweka nyavuni.(Picha na Hannah Mckay/Reuters).

Ni katika mchezo huo wa Novemba 27, 2022 wa Kombe la Dunia la Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) katika dimba la Ahmad Bin Ali nchini Qatar ambapo Fuller aliyatumia makosa ya safu ya ulinzi wakati Japan iliposhindwa kuondoa mpira na kugonga wavu kutoka mita 18 kwa mlinda mlango wao, Shuichi Gonda.

Mechi hiyo katika kipindi cha kwanza wawili hao walionekana kukamiana ingawa hakuna aliyepata matokeo ambapo katika kipindi cha pili kilionekana bora zaidi huku Costa Rica wakitumia udhaifu wa Japan kupenya.

Kipa wa Costa Rica Keylor Navas alionesha ukomavu wa hali ya juu zaidi na kuokoa hatari kadhaa katika dakika za mwisho, hivyo kuhakikisha ushindi huo unasalia upande wao.

Japan ina mchezo mmoja wa Kundi E uliosalia na Uhispania, na Costa Rica itamenyana na Ujerumani katika mechi yake ya mwisho ya kundi.

Kama wangeshinda, Japan ingeweza kufuzu kwa hatua ya inayofuata baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 kutoka kwa Ujerumani katika mechi yake ya kwanza.

Aidha, Costa Rica ilichapwa 7-0 na Uhispania katika mchezo wake wa kwanza, hivyo matokeo hayo yamewaondolea aibu kidogo.

Licha ya Japan kuonekana kumiliki mpira haikuweza kufaidi mtanange huo.Ritsu Doan, ambaye alifunga moja ya mabao ya Japan katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Ujerumani, alionekana kuwa tishio zaidi mapema ingawa, kasi yake haikuzaa matunda.

Japan ambayo inashiriki Kombe la Dunia la saba mfululizo, imefika hatua ya mtoano mara tatu, ikipoteza kila wakati katika hatua ya 16. Costa Rica ilifika robo fainali huko Brazil mwaka 2014.

Katika mtanange huo, Japan ilifanya mabadiliko makubwa kwenye timu ambayo ilishtua Ujerumani katika mechi yao ya ufunguzi huku kocha Hajime Moriyasu akitumia kikamilifu kikosi chake cha wachezaji 26.

Naye Kocha wa Costa Rica Luis Fernando Suarez alikataa kufanya mabadiliko ya jumla kwa timu iliyopigwa na Uhispania, na kuwaacha winga chipukizi Jewison Bennette na beki Carlos Martinez kwenye benchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news