NA MWANDISHI WETU
NAIBU Waziri Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Patrobas Katambi ameiasa jamii na wadau kuendelea kuchangia fedha katika Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI (ATF) ili kusaidia katika utekelezaji wa shughuli za afua za UKIMWI nchini.
Naibu Waziri Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Patrobas Katambi akihutubia wakati wa shughuli ya mbio za Marathon zinazolenga kuhamasisha uchangiaji wa Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI yaani AIDS Trust Fund (ATF) zilizohitimishwa katika Uwanja wa Ilulu mkoani Lindi leo Novemba 27, 2022. (Picha na OWM).
Ameyasema hayo leo Novemba 27,2022 wakati akihutubia kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa kwenye shughuli za mbio za nyika (Marathon) za kuchangia mfuko huo kwa kuanzia Uwanja wa Ilulu na kumalizikia katika uwaja huo kwa kukimbia kilomita 21,10 na 5 zilizowakilisha taswira ya utayari wa kila mmoja wetu kuchangia mfuko huu kwa hali na mali.
Amesema, kustawi kwa mfuko huu kutasaidia kupunguza utegemezi wa rasilimali fedha kutoka kwa wahisani wa nchi za kigeni na kueleza kuwa uwepo wa mfuko imara unatupa uhakika wa uendelevu wa afua za UKIMWI nchini.
Mhe. Katambi amewapongeza washiriki wote wa mbio hizo huku akotoa rai kwa jamii kuendelea kujitokeza kuchangia mfuko huo kuwa na uhakika wa fedha katika utekelezaji wa afua za masuala ya UKIMWI.
"Kipekee, niwashukuru Wadhamini na Washiriki wote wa Mbio hizi za ATF Marathon 2022 Lindi. Asanteni sana kwa kuchangia Mfuko huu na kushiriki mbio hizi za Marathon, natoa wito kwa Makampuni, Asasi mbalimbali na wananchi wote kuendelea kuhamasika kuchangia mfuko wetu kupitia akaunti ya Benki namba 20110033895 iliyopo Benki ya NMB na namba za simu ya mkononi 0684 90 90 90 kwa ajili ya kuboresha na uendelevu wa huduma za kudhibiti VVU na UKIMWI na hivyo, kuimarisha afya na kuokoa maisha ya Watanzania,"amesisitiza Mhe.Katambi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI nchini Dkt. Leonard Maboko akizungumza wakati wa hafla hiyo.
Amefafanua kuwa, Serikali inauchukulia kwa uzito mkubwa mfuko huo na kuahidi kuendelea kushirikiana na Wadau wote ili kuona namna bora, endelevu na ya uhakika ya kutunisha mfuko huu.
Aidha, Mfuko huo ulianzishwa takribani miaka saba iliyopita na yamepatikana mafanikio makubwa sana kwani umeweza kukusanya jumla ya shilingi 4,993,373,407.24.
"Fedha hizi zimesaidia sana kutekeleza afua mbalimbali za UKIMWI ikiwemo ununuzi wa dawa za magonjwa nyemelezi kwa WAVIU ambapo kiasi cha shilingi Bilioni 1.56 zilitolewa kwa Wizara ya Afya kusaidia upatikanaji wa dawa hizo," amesema.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bw.Kaspar Mmuya akizungumza wakati wa hafla hiyo.
Sambamba na hilo, Mfuko umesaidia ujenzi wa upanuzi wa Kituo cha Afya Mererani kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara ambacho licha ya kutoa huduma nyingine za afya, kituo hicho kinatumika kutoa huduma za dawa za kufubaza VVU yaani ARV kwa WAVIU na kuwa kitovu cha uelimishaji wa wananchi kujiepusha na maambukizo mapya ya VVU, ambapo kiasi cha Shilingi milioni 245 zilitumika.
Akieleza hali ya maambukizi mapya ya VVU alisema, kundi la vijana linaongoza hivyo ni muhimu kuwekeza nguvu zaidi ili kulilinda kundi hilo ambalo ndilo nguvu kazi ya Taifa.
"Kwa mujibu wa takwimu zetu, vijana wapo kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizo mapya. Kwa hiyo kutekelezwa kwa afua za kinga kwa vijana ni mkakati mkubwa wa Taifa wa kuwakinga vijana wetu na maambukizo ya VVU,"amesema.
Serikali kwa kushirikiana na Wadau inafanya juhudi kubwa kuuimarisha Mfuko huu, hususan kuufanya uwe na chanzo cha uhakika na endelevu na kuimarisha usimamizi wake ili kukabilina na changamoto zinazoukabili Mfuko huo kwa sasa.
Kauli Mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI mwaka huu 2022 ni “IMARISHA USAWA”. Kauli mbiu hii inatukumbusha lengo kuu la kuhakikisha usawa kwa wote katika upatikanaji wa huduma za kudhibiti VVU na UKIMWI na hakuna mtu atakaeachwa nyuma, ili kufikia lengo la kidunia la Sifuri Tatu (yaani Maambukizi Mapya Sifuri, Vifo vitokanavyo na UKIMWI Sifuri na Unyanyapaa Sifuri).l
Juhudi zote za kutekeleza lengo hili ziende sambamba na mazingira ya usawa, makundi yote ya kijamii yafikiwe na huduma za VVU na UKIMWI kwa sababu hiyo, tunahitaji nguvu ya pamoja ikiwemo mabadiliko ya tabia na kuachana na mitindo ya maisha inayochochea maambukizi VVU.
“Tujitokeze kwa wingi tangu Maadhimisho haya yalipoanza hadi siku ya kilele ili kuungana na Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye atakuwa Mgeni Rasmi Siku ya Kilele,”alisitiza Mhe. Katambi.