ENYI KIDATO CHA NNE:Wazazi twawaombea

NA LWAGA MWAMBANDE

JUNI 14, 2022 bungeni jijini Dodoma, Serikali ilisema elimu ya msingi hadi kidato cha sita itatolewa bila malipo ili kuwapa nafasi wanafunzi wote wanaotoka kwenye familia maskini kuendelea na masomo.
Pia kukabiliana na mimba za utotoni, mwamko duni wa elimu kwa baadhi ya jamii na utoro sanjari na wale wasioendelea kwa mujibu wa sheria (ufaulu).

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.Mwigulu Nchemba aliyabainisha hayo wakati akisoma Bajeti ya Serikali ya mwaka wa Fedha 2022-2023 huku akisisitiza Serikali itaendelea kujenga mabweni kwenye maeneo hatari kwa watoto wa kike.

“Kwa sasa wanafunzi wa kidato cha tano ni takribani 90,825 na kidato cha sita ni 56,880. Mahitaji ya fedha ni zaidi ya shilingi bilioni 10 (10,339,350,000). Ili kuwapunguzia gharama watoto hao kama Mhe.Rais alivyoielekeza wizara, napendekeza kufuta ada kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita. Kwa hatua hiyo, elimu bila ada ni kuanzia shule za msingi mpaka kidato cha sita,"alisisitiza Waziri Dkt.Nchemba.

Aidha, alisema Serikali itaendelea kuimarisha elimu ya ufundi hususani katika vyuo vya kati kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kujiajiri ama kuajiriwa. 

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, uamuzi huu wa kishujaa wa Serikali si tija kwa wazazi tu, bali pia kwa wanafunzi wenye bidii na umakini katika kujibu mitihani yao inayoendelea leo ya Kidato cha Nne, kikubwa anasema tunawaombea kila la heri, endelea;


1. Enyi kidato cha nne, wazazi twawaombea,
Hiyo miaka minne, iwe ya kuendelea,
Kuna madaraja mane, yale juu pendelea,
Mtihani uwe mwema, matokeo yawe mema.

2. Twatamani kusikia, nyie hamjapotea,
Pepa mnajipigia, Vile tunapendelea,
Matokeo kuingia, muweze kuendelea,
Mtihani uwe mwema, matokeo yawe mema.

3. Nanyi walimu walezi, hongera zetu pokea,
Kweli mmefanya kazi, kwa wanetu kuwalea,
Hata wale mabitozi, nidhamu imerejea,
Mtihani uwe mwema,matokeo yawe mema.

4. Pia serikali yetu, kongole zenu pokea,
Kwa kufanya ya kiutu, ada kutuondolea,
Kufanya watoto wetu, na sisi kuchekelea,
Mtihani uwe mwema, matokeo yawe mema.

5. Baraza la Mitihani, kazi inaendelea,
Huu kwenu mtihani, mitihani tutolea,
Watoto madarasani, msije kuwakosea,
Mtihani uwe mwema, matokeo yawe mema.

6. Na wasimamizi wote, msije kupendelea,
Mkala yenu mapozi, danganya ikatokea,
Saidia wanafunzi, maelekezo tolea,
Mtihani uwe mwema, matokeo yawe mema.

7. Vyombo vya usafiri, watoto mwatubebea,
Mwendo katika safari, taratibu pendelea,
Msijeleta hatari, pepa linaendelea,
Mtihani uwe mwema, matokeo yawe mema.

8. Kwa wazazi na walezi, maombi yaendelea,
Sote tunapenda wazi, elimu kuendelea,
Wavuke hiki kiunzi, mbele wakiendelea,
Mtihani uwe mwema, matokeo yawe mema.

9. Mtihani Form Four, kidogo naelezea,
Kifaulu hilo goo, mbele utaendelea,
Yajayo wewe jogoo, kote wanakupokea,
Mtihani uwe mwema, matokeo yawe mema.

10. Mungu wetu twakujia, maombi twakutolea,
Wanafunzi angalia, pepa linaendelea,
Uweze wasimamia, bila pa kutelezea,
Mtihani uwe mwema, matokeo yawe mema.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news