Fadhil Maganya amng'oa Dkt.Edmund Mdolwa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa

NA DIRAMAKINI

KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bw.Fadhil Maganya amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa akimshinda aliyekuwa mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Dkt.Edmund Mdolwa.
Wajumbe 578 kati ya 835 wa mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa ndiyo walimchagua Fadhil Maganya kuwa mwenyekiti mpya wa jumuiya hiyo.

Maganya ameibuka kidedea akimshinda aliyekuwa Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Dkt. Edmund Mdolwa aliyepata kura 64.

Matokeo hayo yametangazwa Novemba 25, 2022 baada ya wasimamizi wa uchaguzi kuhesabu kura kwa zaidi ya saa saba.

Wagombea walimaliza kuomba kura saa 12 jioni na kisha kufuata upigaji na uhesabuji wa kura ambapo shughuli hiyo ilidumu hadi za saa saba usiku na ndipo msimamizi wa uchaguzi alipotangaza matokeo.

Akitangaza matokeo hayo jijini Dodoma, msimamizi wa uchaguzi huo, Maalim Kombo Hassan amesema Maganya ameibuka kidedea kwa kupata kura 578 kati ya kura 835 zilizopigwa huku kura mbili zikiharibika.

Maganya aliwashinda wagombea wengine saba akiwemo Dkt.Mndolwa. Katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti, Msimamizi huyo amemtangaza Doto Iddi Mabrouk kuwa mshindi kwa kupata kura 530 kati ya 736 zilizopigwa akiwashinda wagombea wengine wanne.

Katika nafasi ya wajumbe watatu wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Tanzania Bara, Mwenyekiti huyo amewatangaza Hamoud Abuu Jumaa, Waziri wa Madini, Dkt.Doto Biteko na George Gandye kuwa washindi.

Jumaa alipata kura 569, Biteko 535 na Gandye 238 kati ya kura 825 zilizopigwa huku kura saba zikiharibika.

Katika nafasi hiyo, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angelina Mabula alipata kura 232 huku Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima akipata kura 195.

Kwa upande wa Baraza Kuu kundi la Zanzibar, Msimamizi huyo aliwatangaza Christina Antony aliyepata kura 325, Ally Issa Ally, kura 397 na Time Bakari kura 441.

Baraza Kuu Bara walioshinda ni Ally Kassim Mandai aliyepata kura 220, Lulu Abas Mtemvu kura 248 na Saad Mohammed Khimji kura 298.

Peter Kasera aliibuka mshindi wa uwakilishi UVCCM kwa kupata kura 264 na kwa upande wa Uwakilishi wa UWT mshindi akiwa ni Asha Juma Ferouz aliyepata kura 287 akiwashinda wagombea wengine watatu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news