HAKUNA MTOTO WA MWALIMU JULIUS KAMBARAGE NYERERE ALIYESOMA SAME SECONDARY SCHOOL,YULE KANJANJA KATUPIGA KAMBA

NA MZEE wa ATIKALI

JANA Alhamisi, Novemba 3, 2022, kuna mwandishi "Kanjanja" aliamua kuwafunga kamba mamilioni ya "Bongolanders" nchini.

Alifanikiwa sana. "Aliwaingiza kingi" kirahisi sana. Andiko lake likataradadi Makundisogozi lukuki nchini. 
 
"Mpiga Fiksi" huyu alidai kuwa Rais Nyerere alimteua Bw. Gaudiose Tibakweitira kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu baada ya kuonesha "ununda" kwa mtoto wa Rais Nyerere aliyesoma Same Secondary School.
Mke wa marehemu Gaudiose Tibakweitira, Mama Tibakweitira, amemfundisha Mzee wa Atikali Oysterbay Primary School alikokuwa Headmistress. Hivyo, Mzee wa Atikali hakuweza kuukalia kimya upotoshaji huu mkubwa dhidi ya mume wa Headmistress wake.

2. Maswali ya Kujiuliza:

2.1 Ni kwa nini mwandishi hakuandika jina lake wala namba yake ya simu?

2.2 Ni kwa nini hakumtaja jina mtoto huyo wa Rais Nyerere?

2.3 Ni kwa nini hakutoa ushahidi wowote uoneshao kuwa mtoto huyo wa Rais Nyerere alisoma Same Secondary School?

2.4 Ni kwanini hakutaja mwaka ambao mtoto huyo wa Rais Nyerere alisoma shule hiyo?

2.5 Je, ni kwa nini mwandishi huyu hakusema marehemu Gaudiose Tibakweitira alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu mwaka gani?

2.6 Ni kwa nini mwandishi huyu ameamua kumchafua mtoto wa Rais Nyerere kuwa alifanya kosa lililohitaji Rais Nyerere aende shuleni?.

2.7 Ni kwanini amemsingizia mtoto wa Rais Nyerere kuwa alimpeleka shule DC na kisha RC badala ya Rais Nyerere?

3. Tibakweitira ni Nani?


Marehemu Gaudiose Tibakweitira aliletwa duniani Jumatatu, Oktoba 9, 1933 huko Itongo,Kamachumu, Lake Province (Kagera).

Alisoma Shule ya Msingi Rutabo,Shule ya Sekondari ya Rubya Seminary,Pugu High School na Chuo cha Makerere alikohitimu shahada ya sayansi mwaka 1963. Alikuwa na akili sana darasani.

Kazi yake, baada ya kumaliza masomo, ilikuwa ni ualimu. Alikuwa ni mwalimu hodari na mwenye uwezo wa hali ya juu sana.

4. Mzee wa Atikali aingia chimbo

4.1Watoto wa Mwalimu Nyerere

Mzee wa Atikali ,baada ya kugutuka kuwa huo ni uzushi, aliwavutia waya wasoma Atikali wawili hodari ambao ni watoto wa Mwalimu. Hii ni kwa vile Mzee wa Atikali ni muumini wa falsafa ya marehemu Mwenyekiti Mao ZeDong aliyoitoa Julai 5, 1975 "No Research, No Right to Speak".

Madaraka (mtoto wa sita wa Mwalimu) alimjuza Mzee wa Atikali kuwa hizo ni fiksi, kwani hakuna mtoto wa Mwalimu aliyesoma shue hiyo. Mzee wa Atikali pia alimtwangia RC wa Manyara ambaye pia alisema hizo ni kamba.

4.2 Ukatibu Mkuu


Mzee wa Atikali alifanya utafiti na kubaini Bw. Gaudiose Tibakweitira hajawahi kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu.Wizara ya kwanza aliyotumikia kama Katibu Mkuu ilikuwa ni Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi.

Baadaye, 1983-1984, aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Vijana, Utamaduni na Michezo.Na kisha aliteuliwa kuwa Mkuu wa IDM Mzumbe 1985- 1989 alipostaafu.

4.3 Tibakweitira Hakutokea Ukuu wa Shule kuwa Katibu Mkuu

Marehemu Tibakweitira alipoteuliwa na Rais Nyerere kuwa Katibu Mkuu kwa mara ya kwanza hakuwa ametokea kuwa Mkuu wa shule. Alitokea kwenye cheo cha Mwenyekiti na Mkurugenzi wa Shirika la Usafiri la Taifa (NTC).

4.4 Tibakweitira alikuwa Mkuu wa Shule Ihungo

Mara ya mwisho Tibakweitira kuwa Mkuu wa Shule ilikuwa Ihungo Secondary School (1967-1969). Yeye alikuwa ndiye Mkuu wa kwanza Mtanzania kwenye shule hiyo akiwa kijana mdogo wa miaka 34 tu.

Alipotoka Ihungo akapelekwa Wizara ya Elimu ambako aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Msaidizi, Elimu ya Msingi.

4.5 Tibakweitira alikuwa Mkuu wa Same miaka ya mwanzoni ya 1960

Tibakweitira alikuwa ni mmoja wa "Bongolanderz" wa kwanza kuwa wakuu wa shule nchini kwani hapo kabla wakuu wa shule walikuwa Wazungu na raia wa mataifa mengine. Yeye ndiye alikuwa Mwalimu Mkuu wa kwanza Bongolander wa "Same Secondary School" Yeye alikuwa Mkuu wa shule akimpokea Bw. Raphael Isaack aliyekuwa Muisrael.

4.5 Ndugu wa Tibakweitira


Mzee wa Atikali aliongea na ndugu mmoja wa marehemu Tibakweitira (hakupenda kutajwa) aliyesema pia kuwa huo ulioandikwa na huyo mwandishi ni uongo wa kiwango cha lami.

4.6 Andrew Nyerere hakusoma Same

Kwa kuwa marehemu Tibakweitira alianza kuwa Mkuu wa Ihungo mwaka 1967, basi mtoto kiume wa Rais Nyerere ambaye angeweza kuwa sekondari kabla ya 1967 na kusoma Same Secondary School ni Andrew Nyerere aliyezaliwa 1954.

Hata hivyo, Andrew alisoma Forodhani Secondary School (ambako pia Mzee wa Atikali amesoma) enzi hizo ikiitwa St. Joseph. Hii inazidi kuonesha kuwa stori ya huyo mwandishi ni ya kubumba.

4.6: Vitabu

Shule walikosoma watoto wote wa Rais Nyerere zimetajwa kwenye vitabu mbalimbali vikiwemo hivi vifuatavyo ambavyo ni vipya-:

4.6.1. Prof. Shivji's:Development as Rebellion: A Biography of Julius Nyerere.

4.6.2.Mark Mwandosya & Juma Mwapachu's: "38 Reflections on Mwalimu Nyerere".

Kwa mujibu wa vitabu hivi, Same Secondary School haijatajwa kama moja ya shule walizosoma watoto wa Mwalimu.

5. Hitimisho:

Je, Mwandishi Kanjanja wa habari zile za uongo aliyefanikiwa kuwapiga fiksi mamilioni ya "Bongolanderz" nchini anatakiwa afanyiwe jambo gani kati ya haya mawili-:?

1. Ajengewe mnara sehemu "Ujasiri" wake; au

2. Anyakwe kwani amekengeuka kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandaoni, 2015 kinachokataza Kupiga Fiksi!

Mzee wa Atikali
0754 744 557

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news