NA DIRAMAKINI
MAMLAKA ya Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imewakamata watuhumiwa 11 akiwemo kocha wa makipa wa timu ya Simba SC, Muharami Sultan (40) wakiwa na kilo 34.89 za dawa za kulevya aina ya heroin na biskuti 50 zilizotengenezwa kwa kutumia dawa ya kulevya aina ya bangi.
Akizungumza jijini Dar es Salama leo, Novemba 15, 2022 Kamishna Jenerali wa DCEA, Gerald Kusaya amesema watuhumiwa waliokamatwa na dawa za kulevya aina ya heroine ni kocha wa makipa wa Simba, Muharami Sultan (40), mmiliki wa kituo cha Cambiasso Sport Academy kilichopo Tuangoma, Kambi Zuberi Seif (40).
Pia wamo Said Matwiko mkazi Magole (41), Maulid Mzungu maarufu Mbonde (54) mkazi wa kisemvule ambaye ni ndugu na kocha wa makipa wa Simba Muharami.
Wengine ni John John maarufu Chipanda (40) ambaye jukumu lake kutafuta vijana wenye vipaji na kuwapeleka Cambiasso Sport Academy.
Pia wamo Rajabu Dhahabu (32)) mkazi wa Tabata, Seleman Matola Said (24) mkazi wa Temeke Wailes, Hussein Pazi (41) mfanyabiashara na Ramadhani Chalamila (27) mkazi wa Kongowe.
Aidha, Kusaya amesema pia DCEA imemkamata mfanyabiashara na mkazi wa Kaloleni Arusha, Abdulnasir Haruon Kombo (30) akiwa na biskuti pakiti 50 zilizotengenezwa kwa kutumia dawa za kulevya aina ya bangi kama moja ya malighafi akiwa anaziuza katika eneo la Kaloleni jijini Arusha.
Amesema katika tukio hilo la ukamataji wa biskuti zenye bangi, wamefanikiwa kumkamata mtuhumiwa mwingine anayeitwa Hassan Ismail (25) mkazi wa Olasiti jijini Arusha anayesadikiwa kuwa ndiye mtengeneza biskuti hizo.
Amesema ukamataji huo ni muendelezo wa operesheni zinazofanyika katika maeneo mbali mbali nchi.
“Uwepo wa bidhaa za vyakula vinavyotengenezwa kwa kutumia bangi vimeanza kushamiri hapa nchini, itakumbukwa mwaka 2020-2021 mamlaka ilikamata bangi iliyosindikwa mfano wa jam, Keki na Asali katika matukio tofauti,” amesema.
Amesema, tatizo hilo limeshamiri nchini hasa ikizingatiwa kuwa wafanyabiashara wenye nia ovu hutumia vyakula vinavyopendwa na Watoto mfano pipi, keki, iche cream na biskuti hivyo kuwepo na uwezekano wa kuwaingiza waotot kwenye matumizi ya dawa la kulevya bila kujua na hatimaye kuwa waraibu.