NA FRESHA KINASA
KATIKA kuadhimisha siku 16 za kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia, Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) kwa kushirikiana na Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Serengeti mkoani Mara wametoa elimu ya ukatili wa kijinsia katika Shule ya Msingi Mapinduzi Day iliyopo wilayani Serengeti na msaada wa taulo kwa wanafunzi wa kike shuleni hapo.
Kauli mbiu ya mwaka huu inasema 'kila uhai unathamani tokomeza mauaji na ukatili wa wanawake na watoto' ambapo yamaenza rasmi Novemba 25, 2022 na kilele chake itakuwa Desemba 10, 2022.
Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania limekuwa likifanya kazi na Dawati la Jinsia na Watoto, Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Jamii ambapo linajishughulisha na mapambano ya vitendo vya ukatili wa Kijinsia katika Mkoa wa Mara chini ya Mkurugenzi wake, Rhobi Samwelly.
Ambapo lin avituo viwili kikiwemo Kituo cha Nyumba Salama Kiabakari kilichopo wilayani Butima na Kituo cha Hope Mugumu Nyumba Salama katika Wilaya ya Serengeti.
Vituo hivyo hutoa hifadhi kwa wasichana ambao hukimbia ukatili wa aina mbalimbali ikiwemo ukeketaji na ndoa za utotoni pamoja na kuwapa msaada wa kisaikolojia, mahitaji yao muhimu, kuwaendeleza kielimu na kifani wakiwa katika vituo hivyo ili wafikie ndoto zao.
Akizungumza na wanafunzi wa shule hiyo Novemba 24, 2022. Afisa Mwelimishaji Jamii kutoka Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, Bw. Emmanuel Goodluck amesema, vitendo vya ukatili wa kijinsia ni kikwazo cha ustawi bora wa maendeleo, kwani vinarudisha nyuma maendeleo na kuathiri afya. Hivyo kila mmoja aunge mkono juhudi za serikali na wadau wa mapambano ya vitendo hivyo.
"Mfano ukeketaji una madhara ikiwemo kutoka damu nyingi wakati wa kukeketwa, kuandaliwa kuozeshwa na hivyo kukatisha masomo, hatari ya kupata magonjwa ya kuambukiza, kuathiri kisaikolojia kutokana na kufanyiwa ukeketaji kwa lazima pamoja na kupata ulemavu kwa hiyo ukeketaji haufai lazima upingwe."amesema Goodluck.
"Vipo pia vipigo kwa wanawake na watoto, vitendo vya ulawiti kwa watoto na ubakaji hivi pia vina athari kubwa kwa ustawi wa jamii yetu,"amesema Goodluck.
Pia, amewaomba wanafunzi hao kuwa mabalozi wa kutoa elimu ya madhara ya ukatili wa kijinsia waliyoipata katika kuhakikisha kwamba ukatili unakwisha.
Suzan John ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya Sekondari Twiboke ambaye anaishi Kituo cha Hope Mugumu Nyumba Salama baada ya kukimbia ukeketaji kutoka kwao, ameiomba serikali kuendelea kutoa elimu kwa jamii na kusimamia vikali sheria kuwaadhibu wanaofanya vitendo vya ukatili kwani wanakwamisha watoto wa kike kufikia ndoto zao.
Kwa upande wao wanafunzi wa kike shuleni hapo wakizungumza na DIRAMAKINI wamepongeza kutolewa kwa elimu hiyo sambamba na kupewa taulo za kike, kwani zitawasaidia kujistiri na kuondokana na kutohudhuria masomo wakati wa hedhi.
Anna Lange ni Mkuu wa Shule ya Sekondari Mapinduzi Day amesema kuwa, jamii inapaswa kuweka mkazo katika elimu hasa kuwasomesha watoto wa kike, kwani wakielimika jamii nzima inapata manufaa katika nyanja ya kijamii na kiuchumi.
Pi, amepongeza kazi zinazofanywa na Shirika la Hope for Girls katika kupambana na vitendo vya ukatili na kuwasaidia wasichana kufanikisha malengo yao kwa kuwapa mahitaji muhimu na kuwaendeleza kielimu.
Pius Julius Kahabi ni Inspekta wa Polisi Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi Kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Serengeti amewataka wanafunzi hao kutoa taarifa za vitendo vya ukatili wa kijinsia katika ofisi za Serikali,polisi na ofisi za maendeleo ya jamii.
Amesema, Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Serengeti limejipanga kwa kushirikiana na Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania na wadau mbalimbali kuunda mabaraza katika shule za msingi na sekondari wilayani humo.
"Tumejipanga tutazunguka wilaya nzima kuunda mabaraza ya ukatili wa kijinsia. Kuna watoto wengi wanafanyiwa ukatili taarifa hazitolewi, lakini hizi klabu tutakazoziunda zitakwenda kuibua ukatili katika maeneo yao, lengo ni kuhakikisha ulinzi na usalama kwa watoto unakuwepo, kwani ukatili ni kosa kisheria. Tunahitaji kuwa na nguvu ya pamoja katika kukomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia katika Wilaya ya Serengeti,''amesema Kahabi.
Tags
Habari
HGWT
Kataa Ukatili
Mkoa wa Mara
Serengeti
Siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia
Unyanyasaji na Ukatili wa Kijinsia