HUDUMA ZA FEDHA: WATUMIAJI WALINDWE

NA LWAGA MWAMBANDE

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.Philip Mpango ameitaka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuhakikisha kuwa huduma za fedha zinafika na kutumika vijijini na kwamba maslahi ya watumiaji wa huduma hizo yanalindwa.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na Gavana, Prof. Florens Luoga, alipotembelea banda la BoT katika Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha yanayofanyika katika Viwanja vya Rockcity Mall jijini Mwanza.

Dkt.Mpango ametoa maagizo hayo Novemba 24, 2022 alipotembelea banda la BoT katika Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha yanayofanyika katika Viwanja vya Rock City Mall jijini Mwanza ambapo alipokelewa na Gavana wa BoT, Prof. Florens Luoga.

Mheshimiwa Dkt.Mpango amesema, mtu anakwenda benki kukopa, lakini baadae msaada aliopewa kwenye benki wa kusimamia mradi husika unakosa umakini, halafu wanapeleka wanasheria kuuza mali na wanunuzi wa hizo mali wanatoka kwenye benki hizo hizo za biashara.

Pia, Dkt.Mpango ameitaka BoT kuendelea kufanya kazi kwa karibu na Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) ili kupunguza viwango vya riba wanavyotozwa wananchi wanapochukua mikopo.

"Najua Benki Kuu imechukua jitihada za makusudi. Ninyi mnakopesha (mabenki) kwa asilimia tatu, lakini wao wanakopesha kwa asilimia tisa. Mfanye kazi kwa karibu na mabenki na TBA mtafute dawa ya riba kuwa juu,”alielekeza Makamu wa Rais Dkt.Mpango.

Kwa nini Benki Kuu ya Tanzania? Ni kwa sababu, Serikali imeipa jukumu la kudhibiti na kusimamia benki zote, taasisi za fedha na Bureau de Change nchini.

Zaidi ya hayo, Benki Kuu ya Tanzania ina jukumu la kudhibiti na kusimamia masuala yote ya fedha ya mifuko yote ya hifadhi ya jamii (mashirika ya pensheni), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) nchini Tanzania.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, haki za walaji na huduma wanazopewa zikiwa bora ni moja wapo ya hatua muhimu ya kuchochea kasi ya maendeleo nchini, endelea;

1.Watumiaji walindwe, hizi huduma za fedha,
Wakopeshaji wafundwe, riba mikopo ya fedha,
Kama wataka wapendwe, tena waongeze ladha,
Linda haki za walaji, na huduma ziwe bora.

2.Linda haki za walaji, na huduma ziwe bora,
Benki Kuu ni hitaji, kwa huduma fedha bora,
Tena kwenu ni mtaji, mnasimamia sera,
Ni Makamu wa Rais, katoa maelekezo.

3.Ni Makamu wa Rais, katoa maelekezo,
Kwa jinsi vile ahisi, sehemu kuna uozo,
Riba ni za mwendokasi, kalikali kama tozo,
Yeye ashindwa kukopa, vipi hao wananchi?

4.Yeye ashindwa kukopa, vipi hao wananchi?
Riba mikopo ni kapa, hata uwe na makochi,
Mikopo watu waepa, kama kukimbia winchi,
Kwa hali ilivyo sasa, riba zapaswa kushuka.

5.Kwa hali ilivyo sasa, riba zapaswa kushuka,
Utambulisho kisasa, watu wanafahamika,
Wasiwasi ni makosa, bure wanagharamika,
Hatua za Serikali, riba ziweze pungua.

6.Hatua za Serikali, riba ziweze pungua,
Benki Kuu hata hili, kwa neon kawainua,
Hatua nzuri dalili, riba ziweze pungua,
Mabenki itikieni, riba ziwe za nafuu.

7.Mabenki itikieni, riba ziwe za nafuu,
Wateja saidieni, hali zao zende juu,
Hapo uchumi nchini, yatafanyika makuu,
Riba zikiwa nafuu, kwa uzalishaji bora.

8.Riba zikiwa nafuu, kwa uzalishaji bora,
Sababu ya Benki Kuu, tunaona riba bora,
Kutokea kule juu, sasa si sana zakera,
Lengo zidizi kushuka, zifike dijiti moja.

9.Lengo ziweze kushuka, zifike dijiti moja,
Hapo tutafurahika, watumiaji pamoja,
Tukope zende tumika, kwenda ongeza wateja,
Riba nafuu ni bora, kwa maendeleo yetu.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news