NA DIRAMAKINI
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, leo Jumamosi Novemba 12, 2022 amewasili mkoani Iringa kwa ajili ya Ufungaji wa Maonesho ya Utalii ya Karibu Kusini 2022.
Ufungaji wa Maonesho hayo unatarajiwa kufanyika hapo Novemba 13, 2022 kwenye Viwanja vya Kihesa-Kilolo, katika Halmashauri ya Iringa Mjini.
Awali, Mheshimiwa Othman, ambaye amewasili hapo akitokea mkoani Dodoma, amepokea taarifa fupi ya utekelezaji, kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Bi.Halima Dendego.
Taarifa hiyo, pamoja na mambo mengine, imeeleza mafanikio makubwa yakiwemo ya ubunifu katika Sekta ya Utalii, sambamba na ufanikishaji wa huduma za maji safi na umeme kwa vijiji vyote 360 vya mkoa huo, ukitoa takriban 37 ambavyo juhudi zinaendelea kuhakikisha navyo vinafikishiwa upatikanaji wa mahitaji hayo muhimu.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo fupi, Mkoa wa Iringa ambao unashikilia nafasi ya pili kwa kima cha juu cha Pato la mwananchi wa Tanzania, baada ya Dar es Salaam, umetajwa pia kuwa ni kiunganishi muhimu cha Sekta ya Utalii kwa upande wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
Katika salamu zake, baada ya kupokea ripoti hiyo, Mheshimiwa Othman ameshukuru na kupongeza juhudi zinazochukuliwa na Uongozi wa Mkoa wa Iringa katika kuhamasisha maendeleo, zikiwemo za ubunifu katika sekta ya utalii, upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Nduli, pamoja na mikakati imara ya kuwasogezea wananchi huduma muhimu za kijamii.
Amesema sekta ya utalii ni nyenzo muhimu ya maendeleo ambapo ikitumika ipasavyo inaweza kuifungua Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kiuchumi.
Amefahamisha kuwa, Sekta ya Utalii ni kiunganishi muhimu cha kukuza umoja na mashirikiano baina ya pande zote na pia ni sehemu muhimu ya kuimarisha Muungano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Mheshimiwa Othman ameutaja Mkoa wa Iringa akisema, "ni darasa muhimu linaloweza kuifunza Zanzibar kuhusu utalii wa mazingira".
Aidha amesema kuwa, pamoja na changamoto ziliopo, hasa kwa upande wa Zanzibar, zikiwemo za kasi ya ukuaji wa miji na ongezeko la watu, na kwa mujibu wa Taarifa za Sensa ya hivi karibuni, ukilinganisha na uchache wa ardhi ya Visiwani, bali nafuu na faraja kubwa bado inapatikana kupitia Sekta ya Utalii.
Mheshimiwa Othman ametoa wito kwa Uongozi wa Mkoa wa Iringa, kutumia fursa kubwa iliyopo sasa, ya Mashirika mengi binfsi ya Ndege, ili kuutangaza Utalii wa Mikoa ya Kusini mwa Tanzania.