NA LWAGA MWAMBANDE
NOVEMBA 24, 2022 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema ameridhishwa na maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) naSerikali itaendelea kuhakikisha mradi huo unajengwa kwa viwango na kukamilika kama ilivyobainishwa kwenye mkataba.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa ujenzi wa reli hiyo unaendelea vizuri katika vipande vyote na kwamba Serikali itahakikisha mradi huo haukwami na itakabiliana na viashiria vyote vinavyoweza kukwamisha utekelezaji wake.
Ameyasema hayo wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa Stesheni Kuu ya Dodoma katika eneo la Mkonze jijini Dodoma. Waziri Mkuu baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa stesheni hiyo, amewataka Watanzania wanaoshiriki katika ujenzi wa mradi huo wasimamie usalama wa mradi na wawe walinzi ili ukamilike kama ilivyokusudiwa.
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema,hatua ya Serikali kuwekeza katika miundombinu ya kisasa hususani reli hiyo ni hatua njema ambayo inalenga kustawisha uchumi wa jamii na Taifa kwa ujumla,hivyo tuendelee kuunga mkono juhudi hizo na kuziombea mema, endelea;
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema,hatua ya Serikali kuwekeza katika miundombinu ya kisasa hususani reli hiyo ni hatua njema ambayo inalenga kustawisha uchumi wa jamii na Taifa kwa ujumla,hivyo tuendelee kuunga mkono juhudi hizo na kuziombea mema, endelea;
1.Hii reli ya kisasa, ujenzi kukamilika,
Hilo ndilo lengo hasa, Serikali metamka,
Kwetu tamko hamasa, tuendako tutafika,
Kazi Reli ya Kisasa, hadi itakamilika.
2.Huyu Waziri Mkuu, maneno ametamka,
Kwamba kazi hii kuu, hadi mwisho itafika,
Vikwazo vya juu juu, vyote tutashughulika,
Kazi Reli ya Kisasa, hadi itakamilika.
3.Ujenzi unaridhisha, Majaliwa katamka,
Ni kazi wanasongesha, reli iweze jengeka,
Taarifa zatukosha, kwamba kazi yafanyika,
Kazi Reli ya Kisasa, hadi itakamilika.
4.Tena chakufurahisha, kwa viwango yajengeka,
Hadi kuikamilisha, sote tuje kuridhika,
Iweze tusafirisha, na uchumi kujengeka,
Kazi Reli ya Kisasa, hadi itakamilika.
5.Na tena ujenzi huko, kazi inavyofanyika,
Vipande vyote vya huko, wako wanawajibika,
Kwa mipango iliyoko, ni mwendo kuchakarika,
Kazi Reli ya Kisasa, hadi itakamilika.
6.Wito bora umetoka, sisi sote twahusika,
Hasa wanaohusika, kujenga ndiyo hakika,
Usalama wahusika, usije kuhujumika,
Kazi Reli ya Kisasa, hadi itakamilika.
7.Reli ya Kisasa moja, hadi kitaeleweka,
Serikali kwa pamoja, kwingine yawajibika,
Ndivyo inajenga hoja, ya kwamba inatumika,
Kazi Reli ya Kisasa, hadi itakamilika.
8.Serikali ya Samia, majukumu imeshika,
Sekta kuangalia, zipate kuimarika,
Reli barabara pia, afya pia yaboreka,
Kazi Reli ya Kisasa, hadi itakamilika.
9.Kazi inaendelea, miradi inajengeka,
Reli inaendelea, umeme wanasimika,
Shule tunachekelea, malengo yanafikika,
Kazi Reli ya Kisasa, hadi itakamilika.
10.Mema tuombee heri, ili Yazidi fanyika,
Hii ya kwetu safari, tukizidi kuinuka,
Tufike pale pazuri, huduma tukitosheka,
Kazi Reli ya Kisasa, hadi itakamilika.
11.Dar-Morogoro vile, karibu ya kamilika,
Hapa tunapewa shule, vitu vinanunulika,
Mabehewa teletele, ili yaweze tumika,
Kazi Reli ya Kisasa, hadi itakamilika.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602