'Kocha wa makipa' Simba SC, wenzake wapandishwa kizimbani Kisutu kwa tuhuma za kufanya biashara dawa za kulevya

NA DIRAMAKINI

BWANA Muharami Sultan (40) ambaye alikuwa kocha wa makipa Simba SC na wenzake wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za usafirishaji wa dawa za kulevya.
Sultan na wenzake wamesomewa mashitaka hayo leo Novemba 21,2022 na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Merry Mrio na Wakili wa utetezi Daudi Mzeri.

Mbali na huyo pia kuna mmiliki wa Kituo cha Cambiasso Sport Academy kilichopo Tuangoma, Kambi Zuberi Seif, Said Matwiko mkazi wa Magole, Maulid Mzungu maarufu Mbonde (54) mkazi wa Kisemvule na John John maarufu Chipanda (40) ambaye jukumu lake ni kutafuta vijana wenye vipaji na kuwapeleka Cambiasso Sport Academy na Sara Joseph.

Mwanga ameieleza mahakama kuwa, watuhumiwa wanakabiliwa na mashitaka mawili ya usafilishaji wa dawa za kulevya

Katika hati ya mashitaka imeeleza kuwa, hivi karibuni katika Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina heroin zenye uzito wa kilogramu 27.1.

Pia shitaka la pili wanatuhumiwa kulitenda mnamo Novemba 4, 2022 ndani ya Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani walikutwa wakisafirisha dawa aina heroin zenye uzito wa kilogramu 7.79.

Baada ya kusomewa mashitaka hayo Hakimu Mrio amewaeleza watuhumiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwani Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikilizwa kesi hiyo.

Wakili Mwanga ameieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado unaemdelea.

Kesi hiyo imehairishwa hadi Desemba 5,2022 kwa ajili ya kutajwa na watuhumiwa wamerudishwa rumande.

Haya yanajiri ikiwa ni siku chache zimepita baada ya Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) kuwakamata watuhumiwa 11 akiwemo kocha wa makipa wa timu ya Simba SC, Muharami Sultan (40) wakiwa na kilo 34.89 za dawa za kulevya aina ya heroin na biskuti 50 zilizotengenezwa kwa kutumia dawa ya kulevya aina ya bangi.
Akizungumza jijini Dar es Salama, Novemba 15, 2022 Kamishna Jenerali wa DCEA, Gerald Kusaya a alisema watuhumiwa waliokamatwa na dawa za kulevya aina ya heroine ni kocha wa makipa wa Simba, Muharami Sultan (40), mmiliki wa kituo cha Cambiasso Sport Academy kilichopo Tuangoma, Kambi Zuberi Seif (40).

Pia wamo Said Matwiko mkazi Magole (41), Maulid Mzungu maarufu Mbonde (54) mkazi wa kisemvule ambaye ni ndugu na kocha wa makipa wa Simba Muharami.

Wengine ni John John maarufu Chipanda (40) ambaye jukumu lake kutafuta vijana wenye vipaji na kuwapeleka Cambiasso Sport Academy.
Pia wamo Rajabu Dhahabu (32)) mkazi wa Tabata, Seleman Matola Said (24) mkazi wa Temeke Wailes, Hussein Pazi (41) mfanyabiashara na Ramadhani Chalamila (27) mkazi wa Kongowe.

Aidha, Kusaya alisema pia DCEA ilimkamata mfanyabiashara na mkazi wa Kaloleni Arusha, Abdulnasir Haruon Kombo (30) akiwa na biskuti pakiti 50 zilizotengenezwa kwa kutumia dawa za kulevya aina ya bangi kama moja ya malighafi akiwa anaziuza katika eneo la Kaloleni jijini Arusha.

Alisema katika tukio hilo la ukamataji wa biskuti zenye bangi, walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa mwingine anayeitwa Hassan Ismail (25) mkazi wa Olasiti jijini Arusha anayesadikiwa kuwa ndiye mtengeneza biskuti hizo.

Alisema ukamataji huo ni muendelezo wa operesheni zinazofanyika katika maeneo mbali mbali nchi.

“Uwepo wa bidhaa za vyakula vinavyotengenezwa kwa kutumia bangi vimeanza kushamiri hapa nchini, itakumbukwa mwaka 2020-2021 mamlaka ilikamata bangi iliyosindikwa mfano wa jam, Keki na Asali katika matukio tofauti,” amesema.
Amesema, tatizo hilo limeshamiri nchini hasa ikizingatiwa kuwa wafanyabiashara wenye nia ovu hutumia vyakula vinavyopendwa na Watoto mfano pipi, keki, iche cream na biskuti hivyo kuwepo na uwezekano wa kuwaingiza waotot kwenye matumizi ya dawa la kulevya bila kujua na hatimaye kuwa waraibu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news