KODI YA ARDHI LIPA: Unaweza kunyang’anywa

NA LWAGA MWAMBANDE

NOVEMBA 18, 2022 Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imewajulisha wananchi kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi (SURA ya 113) kifungu cha 44 kila mmiliki wa ardhi anatakiwa kutimiza masharti ya umiliki ikiwa ni pamoja na sharti la kulipa kodi ya pango la ardhi kila mwaka.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Allan Kijazi pia ameeleza kuwa, baadhi ya wamiliki wamevunja sharti hilo kwa mujibu wa kifungu cha 45 la kulipa kodi ya pango la ardhi kila mwaka.

Hivyo,wananchi wote wanaodaiwa kodi ya pango la ardhi wanapewa nafasi ya mwisho kulipa kodi ya pango ndani ya siku 30 kuanzia Novemba 18, 2022.

Dkt.Kijazi amesema, baada ya muda huu kupita taratibu za kisheria za ubatilisho wa miliki zitaendelea.Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema,kodi ya pango la ardhi, kulipa ni wajibu wetu, endelea;


1.Mna siku thelathini, kodi ya ardhi lipa,
Msisubiri faini, kwa kuchelewa kulipa,
Hizo siku hesabuni, acheni kukopa kopa,
Ni Wizara ya Ardhi, imeshatoa tangazo.

2.Ni Wizara ya Ardhi, imeshatoa tangazo,
Wenye ardhi ni hadhi, fuateni miongozo,
Lipa kodi ya ardhi, vile mnao uwezo,
Viwango vya kawaida, kusiwe visingizio.

3.Viwango vya kawaida, kusiwe visingizio,
Siku thelathini muda, kulitafuta salio,
Msijeipata shida, lijapokuwa fagio,
Ukilipa kodi hiyo, unalijenga taifa.

4.Ukilipa kodi hiyo, unalijenga taifa,
Bila kuilipa hiyo, ni adui wa taifa,
Vile ardhi unayo, hata inakupa sifa,
Hebu sasa ilipie, usijekusumbuliwa.

5.Hebu sasa ilipie, usijekusumbuliwa,
Serikali ikujie, ardhi kuchukuliwa,
Nyumanyuma sisalie, ndiyo umeshaambiwa,
Timiza wajibu wako, kutekeleza sheria.

6.Timiza wajibu wako, kutekeleza sheria,
Ili wengine wenzako, waweze kuwapimia,
Usibaki peke yako, ardhi unaringia,
Na tena kuna tishio, unaweza kunyang’anywa.

7.Na tena kuna tishio, unaweza kunyang’anywa,
Ukiziba masikio, japo sasa unakanywa,
Kujifunga mtandio, bila kodi kukusanywa,
Ardhi yako ni yetu, sisi ndiyo serikali.

8.Ardhi yako ni yetu, sisi ndiyo serikali,
Hutulipi hiyo yetu, takufukuzia mbali,
Tutwae ardhi yetu, tuwape wenye akili,
Kodi pango la ardhi, kulipa wajibu wetu.

9.Kodi pango la ardhi, kulipa wajibu wetu,
Tusiyalete maudhi, kwa kufanya utukutu,
Tuzilinde zetu hadhi, tumekumbushwa kiutu,
Ardhi ya kwetu sote, vema tuihudumie.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news