KUNDI LINALOIPUNGUZIA SERIKALI MZIGO

NA ADELADIUS MAKWEGA

MARA baada ya darasa la saba kufanya mitihani yao ya kumaliza shule za msingi, wazazi wenye vipato huanza kuhangaika kutafuta shule binafsi za kujiunga na kidato cha kwanza kwa watoto wao bila ya kujali kuwa watoto hao watafaulu darasa la saba na kupangiwa shule za sekondari za umma.

Wazazi hao wenye uwezo wa kulipa karo katika shule binafsi, Mwalimu Julius Nyerere alisema bayana kuwa wazazi hawa wanaipunguzia serikali mzigo wa kusomesha, hilo likipunguza gharama kadhaa kwa serikali kwani idadi hiyo inapunguza idadi ya wanafunzi wanaosoma shule za umma. 

Gharama hiyo inayopungua unaweza kuiona katika vifaa vya kufundishia, zana za kujifunzia, gharama ya chakula na hata kupunguza idadi ya wanafunzi wanasomeshwa katika darasa moja katika shule hizi za umma.

Hawa ni wazazi au walezi wanaosaidia kuipunguzia mzigo huo serikali yetu, hiyo serikali ni mimi na wewe na fedha hizo zinatumika kwa matumizi mengine. 

Sifa hiyo ambayo binafsi ninawaita wazazi au walezi wazuri, Mwalimu Nyerere aliitoa katika hotuba yake katika Chuo cha Ualimu Kigurunyembe (sasa Chuo cha Ualimu Morogoro) alipokuwa akisisitiza nguvu ya mwalimu katika masuala ya elimu miaka 70, enzi ya utawala wake.

Mwanakwetu kwa sasa wazazi hao waliosifiwa sana na Julius Nyerere wanawatafutia watoto wao shule hizo za binafsi ili wajiunge na masomo hayo kwa kidato cha kwanza. 

Kama kila mmoja wetu angekuwa na bahati ya kusikiliza mazungumzo mengi ya wazazi au walezi hawa katika simu zao mijadala ni juu ya shule ipi nzuri, interview wanafanya lini? Ada kiasi gani ? Mwanangu amepata shule ile na ile, shule za seminari zinatoa elimu bora na mengine mengi.

Lakini lipo kundi la wazazi wengi wale ambao Mwalimu Nyerere hakuwakusifia ambao wanangoja serikali itangaze matokeo ya darasa la saba na wajue watoto wao wamefaulu shule zipi. 

Hawa ndiyo ndugu zake Mwanakwetu. Kundi hilo ndilo linalozalisha kundi lililosifiwa, maana wengi hawakuwapo katika kundi alilosifia mwalimu wakati huo baada ya wao kusoma katika shule za umma lakini sasa wao wamejaliwa kuwapo katika kundi hilo isipokuwa Mwanakwetu peke yake.

Kundi kubwa na la walio wengi linangonja matokeo ya darasa ka saba wakiyasubiri mithili ya nyota ya jaha kujua wana wao wamepangiwa wapi ili waanze kidato cha kwanza.

Katika kundi hili wapo ndugu zangu wanaosoma shule za msingi zilizopo katika Kata ya Mbagala-Dar es Salaam, kata hii kwa mwaka 2022 pekee ina shule za msingi tano nazo ni Mbagala wanafunzi 3598 kati ya hao 378 wamehitimu la saba, Kizinga wanafunzi 3211 na 351 wamemaliza la saba, Mbagala Annex ina wanafunzi 2621 na 283 ndiyo wanangoja matokeo ya la saba pia kuna shule za Mbagala Islamic na Great Vision. Kati ya shule hizo tatu za mwanzo ni za umma na mbili za mwisho ni binafsi.

Kwa takwimu hizo shule zote zina wanafunzi 10,000. Kwa wastani wanafunzi 400 kwa kila darasa la saba kwa shule za umma. Kwa shule za umma pekee darasa la saba waliohitimu wanakaribia 1012 na kwa ufaulu wa sasa karibu wanafunzi wote hao wanajiunga na kidato cha kwanza.

Ndiyo kusema wanafunzi elfu moja kama watajiunga na kidato cha kwanza katika shule moja ya umma na kwa darasa lenye wanafunzi 40 kidato cha kwanza kitakuwa na mikondo karibu 25.

Mikondo hiyo inaweza kupungua kwa kuwa wazazi wengine watoto wao watakuwa katika kundi lile lililosifiwa na Mwalimu Nyerere, kwa hiyo kata hiyo inahitaji shule ya sekondari yenye madarasa hata 15 ya kupokea kidato cha kwanza kwa wale nduguze Mwanakwetu kwa kubanana hata madarasa nane yanatosha kwa kuanzia tu.

La kustajabisha hadi sasa Novemba, 2022 kata hii haina shule ya sekondari, bali kubwa la kutarajia ni hisani ya kusoma katika shule za kata zingine ambayo hisani hiyo hata mie Mwanakwetu nilipewa mwaka 1990 nikidamka katika Kata ya Mbagala na kusoma Upanga ilipo Tambaza Sekondari, Mwanakwetu hii ni hisani ya muda mrefu sana lazima ifikie kikomo.

Najua msomaji wangu unaweza kujiuliza je Mwanakwetu na yeye hayupo katika kundi lile lililosifiwa na Mwalimu Nyerere? Jibu lake ni hili, wanangu baadhi yao wapo katika shule za kata na wengine wapo katika shule binafsi ndiyo kusema mie sipo moja kwa moja katika kundi lile alilosifia Mwalimu Nyerere, mie ni nusu bini nusu na ndiyo maana kilio changu kwa kujengwa shule ya sekondari ya Kata ya Mbagala ni kikubwa na machozi yake yatakoma kama sekondari hiyo kama itajengwa, kinyume chake machozi yangu yatajaza pipa huku macho yangu yazidi kuwa mekundu.

Wakati kwa sasa wale waliosifiwa na Mwalimu Nyerere wakitafuta shule za watoto wao zile nzuri nzuri, zinazofanya vizuri vizuri tukumbuke kuwa kuna kundi kubwa la wanafunzi zaidi ya 1000 wameufanya mtihani wa darasa la saba katika Kata ya Mbagala na watafaulu huku hawana tumaini labda hisani ya kata zingine tu machoni pao.

Mwanakwetu usidhani nimewasahau wale wa Mbagala Isilamic (820-wote) na (56- watahiniwa) na Great Vision (259 wote) na (27-watahiniwa) na wao wana haki ya kusoma katika shule za umma na watapangiwa japokuwa hawa wengi wa wazazi / walezi wao ni wale waliosifiwa na Mwalimu Nyerere.

Msomaji wangu kumbuka sifa ya kuwa katika kundi alilolisifia Mwalimu Nyerere inaweza kukuponyoka kwa ugonjwa, kifo au kufilisika na watoto wakajiunga na shule za umma, kuna umuhimu mkubwa sana kwa shule za umma.

Jambo hili lifanyike kwa dharula, kitendo cha kukosekana shule ya sekondari ya kata si jambo zuri, kama wanafunzi hao elfu moja na ushehe wakipangiwa shule ya sekondari jirani na makazi yao watasoma vizuri, katika mazingira mazuri na hapo baadae wataingia katika kundi lile lililosifiwa na Mwalimu Nyerere kwa kuwa watakuwa wanajiweza na wataipungizia serikali yetu mzigo.
Niishie hapo kwa leo, kwako Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ndugu yetu, kaka yetu, Amos Makala tunakutaja tena na tena, tunakutaja tena kwa mara ya pili kwa jina lako, kaka yetu Amosi wa Makala saidia jambo hili. Kwa hisani yako na kwa hisani ya mamlaka uliyopewa tusaidie kwa jambo hili na sie wa Mbagala tuingie katika kundi lile linaloipunguzia serikali mzigo, kundi lile lililosifiwa na Mwalimu Nyerere.

makwadeladius@gmail.com
0717649257.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news