KUPATA WATOTO NI MPANGO WA MUNGU

NA ADELADIUS MAKWEGA

WAKRISTO wameambiwa kuwa wasifadhaike wanapokosa watoto, kwani mpango wa Mungu kwa mwanadamu si kuzaana kimwili tu bali kuzaliana kiroho, haya yamehubiriwa katika misa ya Jumapili ya Novemba 6, 2022 katika Kanisa la Bikira Maria Immakulata, Parokia ya Chamwino Ikulu, Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma na Padri Paul Mapalala.

Akihubiri kwa msisitizo mkubwa, uliojaa utulivu, akitamka neno kwa neno katika kanisa lililotulia ndani ya misa hiyo ya dominika hii, kiongozi huyu wa kanisa amesema kuwa,
“Tunapoishi katika maisha yetu, kwa sisi wanadamu kuna kuoa na kuolewa, huo ndiyo mpaka wetu, Mungu yeye anajua namna gani anaweza kuongeza binadamu katika ulimwengu huu ili vizazi vyetu viendelea, mtu anapokosa watoto mara nyingi anafadhaika sana, hapo kibinadamu inaonekena uhai wa familia haupo na hata familia nzima inamdharau ndugu huyo kuwa si chochote si lolote. Ndugu zangu, fahamuni kuwa kwa mpango wa Mungu sivyo, kila mmoja wetu Mungu wetu anao mpango wake kwake na ndiyo maana tupo watawa, huku familia ya Mungu inaendelea.”

Mahubiri hayo yakiendelea kuhubiriwa katika misa hiyo Padri Mapalala alisema kuwa ufalme wa Mungu ni wa wote waliojaliwa na wasiojaliwa watoto, aliongeza kuwa matengemeo yoyote ya binadamu siyo kwa mawazo yetu bali ni kwa mipango ya Mungu.

Kwa wale wanaojaliwa kutamani kuwa na familia wafuate utaratibu wa kufunga ndoa kwa mpangilio na kuwalea watoto hao kwa sifa na utukufu wa Mungu.

Misa hiyo ambayo iliambatana na maombi kadhaa likiwamo la kuombea viongozi wetu pia iliombea kuamsha ndani yetu furaha ya kushirikisha uzima wa milele katika ulimwengu ujao.

Mwishoni mwa misa hii mwandishi wa habari hii ameshuhudia viongozi kadhaa wa jumuiya ndogo ndogo ambao ni umoja unaounda parokia hiyo wakila kiapo mbele ya paroko wao mara baada ya kuchaguliwa kuongoza jumuiya hizo.

Nayo hali ya hewa ya eneo la Chamwino Ikulu imeendelea kuwa ya jua kali wakati mchana huku joto lake likiambatana na upepo unapoza ukali wa jua hilo na mazingira ya Dodoma wakati usiku yakiwa na baridi kidogo hali hiyo ya hewa ikiwa tofauti ya joto la Dar es Salaam lenye fukuto zito.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news