Maagizo ya Rais Dkt.Mwinyi kwa mabalozi yagusa sekta za umma na binafsi

NA MWANDISHI WETU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewataka mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nje kujenga uhusiano wa karibu na taasisi za umma na binafsi za pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuiwezesha Tanzania kunufaika na fursa mbalimbali zilizopo katika maeneo yao ya uwakilishi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika picha ya pamoja na kamati ya maandalizi ya mkutano
Zanzibar, Novemba 18, 2022.

Mhe. Rais Dkt. Mwinyi ametoa wito huo Novemba 18,2022 wakati akizungumza na mabalozi wa Tanzania katika mkutano wao unaondelea jijini Zanzibar. 

Amesema, katika utendaji wa kila siku, ni muhimu mabalozi hao wakahakikisha vipaumbele vyao vinaendana na vile vilivyopo katika Mpango wa Serikali zote mbili na kuzingatia Dira ya Mandeleo ya Zanzibar ya Mwaka 2050; Mpango wa Maendeleo wa Zanzibar wa Mwaka 2021-2026 na Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020 katika utekelezaji wa majukumu yao.
Meza Kuu ikiongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika picha ya pamoja Uongozi na Menejimenti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akiwahutubia mabalozi wa Tanzania nje ya nchi wakati wa mkutano uliofanyika Zanzibar.

Kadhalika, Mhe. Rais Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na kuweka mikakati mbalimbali ili kuhakikisha sekta mbalimbali zikiwemo za biashara, viwanda, kilimo, ufugaji na uchumi wa buluu zinaendelea kuchangia uchumi wa Zanzibar lakini pia Serikali yake imeendelea kuboresha Sekta mbalimbali kwa kuondoa urasimu katika sekta ya uwekezaji na ufanyaji biashara ili kuiwezesha Zanzibar kufikia mapinduzi ya uchumi.
Sehemu ya Mabalozi wakifuatilia mkutano kati yao na Mhe. Rais Hussein Ali Mwinyi.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wizara wakati wa mkutano kati ya Mhe. Rais Hussein Ali Mwinyi na Mabalozi.

Aidha, Mhe. Rais Mwinyi ameongeza kuwa, Serikali yake ya Awamu ya Nane hivi sasa inatekeleza Sera ya Uchumi wa Buluu ambayo inalenga kuhakikisha kunakuwa na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari ili kuinua hali ya maisha ya Wazanzibari kupitia sekta za Uchumi wa Buluu ikiwemo utalii, Ujenzi wa Bandari, uvuvi na ufugaji wa samaki, ukulima wa mwani, nishati ya mafuta na gesi pamoja na biashara ya usafirishaji wa baharini.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga akizungumza kama mshereheshaji wakati wa mkutano kati ya Mhe. Rais Hussein Ali Mwinyi na Mabalozi.

“Serikali ya Zanzibar imeendelea kufanya maboresho mbalimbali ikiwemo kuondoa urasimu katika usajili wa biashara na uwekezaji; kuimarisha huduma za umeme na maji; kuimarisha huduma za viwanja vya ndege na sasa Serikali imekamilisha Mpango Mkuu wa Kujenga Bandari Jumuishi ya Mangapwani. Bandari hii itahusisha bandari ya mizigo, bandari ya mafuta na gesi, bandari ya uvuvi na bandari ya bidhaa za nafaka. Niwaombe Waheshimiwa Mabalozi mtakaporudi kwenye vituo vyenu vya kazi, mkaeleze kwa ufasaha maboresho yaliyofanyika ili kushawishi, wawekezaji na wafanyabiashara kuja kwa wingi hapa Zanzibar,"amesisitiza Mhe. Rais Mwinyi.
Sehemu ya Mabalozi wakifuatilia mkutano kati yao na Mhe. Rais Hussein Ali Mwinyi.

Akizungumzia masuala ya Utalii ambayo ni sekta muhimu kwa uchumi wa Zanzibar, Mhe. Rais Mwinyi amepongeza jitihada zinazofanywa na Balozi za kuwaunganisha wadau wa nje wa sekta ya utalii na kuiwezesha Zanzibar kutangaza fursa na vivutio vya utalii na kusababisha watalii na wageni wengi wa kimataifa kuja kutembelea Zanzibar.

“Kama sote tunavyoshuhudia, sekta ya utalii imeendelea kukua hapa Tanzania. Juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali zetu mbili pamoja na Balozi zetu zimewezesha Sekta hii iliyokuwa imeathiriwa vibaya na janga la UVIKO-19 kurejea kwa kasi kubwa. Idadi ya watalii kutoka nje walioingia Zanzibar mwezi Agosti 2022 ni 61,388 ukilinganisha na watalii 34, 425 katika mwezi Agosti 2022. Kwa kipindi cha miezi minane Januari hadi Agosti 2022 Zanzibar imepokea watalii 322,748 ikiwa ni ongezeko la asilimia 27.6 ukilinganisha na kipindi hicho mwaka 2021. Lengo letu ni kuongeza idadi ya watalii kutoka 538,264 mwaka 2019 hadi kufikia 850,000 ifikapo mwaka 2025, Balozi zetu zina nafasi kubwa kuchangia kufanikisha lengo hilo,”amesema Mhe. Rais Mwinyi.

Mhe. Rais Mwinyi alitumia fursa hiyo pia kuwapongeza Mabalozi kwa kazi nzuri wanayoifanya na kuitaka Wizara kuwajengea uwezo watumishi kwa kuweka mazingira wezeshi ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi zaidi.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiwasilisha salamu za Wizara kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi wakati wa Mkutano wa mabalozi wa Tanzania Nje ya Nchi.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax amemshukuru Mhe. Rais Mwinyi na Wananchi wa Zanzibar kwa kuridhia Mkutano huo ufanyike Zanzibar na kusema kuwa ukarimu uliooneshwa ni wa kipekee.

Pia alisema kuwa Mkutano wa Mabalozi wenye Kaulimbiu “Mwelekeo Mpya Katika Kuimarisha Diplomasia ya Uchumi” unafanyika ili kuiwezesha Wizara na Mabalozi kupokea maelekezo kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ili kujipanga kutekeleza Sera ya Mambo ya Nje yenye msisitizo katika Diplomasia ya Uchumi kwa kuzingatia mwelekeo na mabadiliko mbalimbali yanayoendelea duniani kwa manufa mapana ya Wananchi wa Watanzania.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab akitoa neno la utangulizi wakati wa mkutano kati ya Mhe. Rais Hussein Ali Mwinyi na Mabalozi.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Mohammed Rajab alisema jumla ya Mabalozi 41, Wawakilishi wa Kudumu wa Umoja wa Mataifa Wanne, Makonseli Wakuu watano, Menejimenti ay Wizara na Taasisi za Wizara zimeshiriki Mkutano huo muhimu ambao unalenga kupokea maelekezo ya viongozi wa kitaifa na kutoa mwelekeo na uelewa wa pamoja katika kuboresha utendaji wa Wizara.

Awali akizungumza kwenye Mkutano huo, Amidi Mkuu wa Mabalozi ambaye pia ni Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mhe. Dkt. Asha-Rose Migiro amesema katika kipindi cha siku tano za uwepo wao Zanzibar Mabalozi wamejifunza masuala mbalimbali kupitia mada zilizowasilishwa na Wataalam na Wadau mbalimbali ambazo zote zililenga kuboresha utendaji na kuwawezesha Mabalozi kujipanga upya katika utekelezaji wa majukumu yao. 

Pia alipongeza namna Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya Uongozi wa Mhe. Rais Mwinyi kwa maboresho makubwa inayoendelea kuyafanya katika sekta mbalimbali na namna ilivyojipanga kutumia fursa za kikanda na kimataifa ikiwemo zile zilizopo katika Soko Huru la Biashara Barani Afrika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news