Milioni 400/- za waendesha bodaboda Arusha zachotwa benki

NA DIRAMAKINI

CHAMA cha Waendesha Bodaboda jijini Arusha (UBOJA) wamejikuta katika hali ya misuguano baada ya kubainika zaidi ya shilingi milioni 400 zimetolewa kwenye akaunti ya chama hicho huku baadhi ya fedha hizo zikidaiwa kutumika kisiasa.
Fedha hizo zinadaiwa kutolewa kwenye akaunti ya umoja huo kuanzia mwaka 2018 hadi 2021 katika mazingira ya kutatanisha na baadhi ya waliokuwa viongozi kwa kushirikiana na watu wengine bila wanachama kupewa taarifa yeyote

Katibu wa Umoja huo, Hakimu Msemo akizungumza na waandishi wa haabri alidai, fedha hizo zilikuwa ni msaada kutoka kwa wahisani pamoja na michango ya marejesho ya wanachama wa chama hicho katika kipindi hicho.

Msemo amesema, fedha hizo zimetolewa kwenye akaunti ya chama hicho kuanzia 2018 bila utaratibu na hivyo wameomba Serikali iwasaidie kupata haki yao kwani kwa zaidi ya miezi mitatu sasa wameshinda kujua hatma yao.

Pia Msemo amesema, endapo fedha hizo zikirudishwa katika akaunti yao zitawasaidia kuendelea kukopeshana pikipiki kwa wanachama wao zaidi ya 12,000 waliopo katika kata 25 za jiji hilo la Arusha katika mkoa wa Arusha.

"Tunashukuru Benki ya NMB wametupa taarifa zote za kutolewa kwa fedha tangu kufunguliwa akaunti ambapo tumebaini fedha kutolewa kwenye matawi mbalimbali bila kufuata taratibu," amesema Katibu huyo wa UBOJA.

Amedai wamebaini kiasi cha shilingi milioni 120 kilitolewa Aprili 6, 2018 kupitia tawi la NMB Ngarenaro kwenda akaunti ya moja ya jumuiya za chama kimoja cha siasa na wameonana na viongozi wao na wamekiri kupatiwa fedha hizo.

Kiongozi mmoja wa jumuiya hiyo alikiri kupokelewa fedha katika jumuiya hiyo na kueleza fedha hizo zilitumika kwa ajili ya kuwakopesha wanawake ili kujikwamua na umaskini kama ilivyokuwa kwa bodaboda hao walivyokopeshwa pikipiki.

"Hizi fedha kama unakumbuka zilikuwa zinakusanywa na Mbunge Mrisho Gambo na wafadhili wengine sisi tulipewa ili kuwakopesha wanawake wa Jiji la Arusha,” alisema kiongozi huyo ambaye aliomba jina lake lisitajwe.

Mwenyekiti umoja wa bodaboda jiji la Arusha, Okelo Constantine ameomba Serikali kutoa maelekezo kwa vyombo vya dola kulishughulikia suala hilo kwa uharaka zaidi ili kuwakwamua wanachama wao wanaosubiri mgao wa pikipiki.

Amedai wanachama hao 12,000 huchangia mapato ya serikali kwa kukata leseni ya udereva shilingi 70, 000 kila mmoja kwa miaka mitano, LATRA shilingi 17,000 kila mwaka na mafuta ya shilingi 5,000 kwa siku, hivyo huwawezesha kuchangia mapato mengi kwa Taifa.

Msemaji wa chama hicho, Joshua Samwel amedai wapo wadau wanaotaka kuwasaidia bodaboda 100 kwa kuanzia kulipa shilingi milioni 100 lakini wanakosa fedha za kuanzia kwani akaunti yao ina shilingi milioni mbili tu.

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Said Mtanda amekiri kupokea malalamiko ya viongozi na wanachama wa chama hicho na kusema,"uchunguzi wa malalamiko haya unafanyiwa kazi na vyombo husika vya dola wawe na subira.”

Kwa upande wake Mbunge wa Arusha Mjini (CCM), Mrisho Gambo ambaye alikuwa mmoja wa wasimamizi wa fedha hizo, akizungumza na wanachama wa Uboja wiki iliyopita, alishauri waliokuwa viongozi wa umoja huo watafutwe ili warejeshe fedha hizo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news