MRADI UJENZI WA KITUO CHA TAARIFA ZA KIJIOGRAFIA NA USIMAMIZI WA ARDHI KUANZA JIJINI DODOMA

NA ANTHONY ISHENGOMA

KATIBU Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Allan Kijazi amepokea hati ya makubaliano kutoka ujumbe wa Serikali ya Korea ya Kusini kuhusu mradi wa uanzishwaji wa kituo cha mafunzo ya taarifa za Kijiografia na usimamizi wa Ardhi leo Jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Dkt.Allan Kijazi akikabidhi Cheti cha kuhitimu mafunzo ya Kujenga uwezo kuhusu taarifa za Kijiografia na matumizi ya Ardhi kwa Bi. Aida Mtambaze ambaye ni mtumishi kutoka Wizara yake.

Mradi huo wenye thamani ya Sh.Bil.5 utatoa Mafunzo hayo kupitia Kampuni ya Lx Consortium ya Korea Kusini na utaanza hivi karibuni Jijini Dodoma baada ya kuzinduliwa na serikali ya Tanzania na Korea Kusini baada ya maandalizi kukamilika.

Akiongea na wajumbe wa manajimenti ya Wizara ya Ardhi Dkt. Kijazi amewataka watendaji wa Wizara yake kufanya kazi kwa ushirikiano ili kufanikisha mradi huo ambao ameutaja kuwa wa aina yake barani Afrika kwani mradi huo ni mpya katika nchi za Afrika.

‘’Tukifanikisha mradi huu kwangu mimi ni ushindi mkubwa na utakuwa wa mfano kwa nchi za Afrika hivyo nawaagiza kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa kufanikishwa mradi huu ambao utakuwa wa aina yake nchini na Afrika kwa ujumla,’’ameongea Dkt.Allan Kijazi, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi.
Baadhi ya wahitimu wa mafunzo ya Kujenga uwezo kuhusu taarifa za Kijiografia na matumizi ya Ardhi wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kutunukiwa vyeti vyao na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Aidha, Dkt. Kijazi amechukua fursa hiyo kuwapongeza baadhi ya watumishi wa Wizara ambao wameanza kunufaika na mafunzo ya muda mfupi ya kuwajengea uwezo kuhusu taarifa za Kijiografia na Utawala wa ardhi mafunzo ambayo yametolewa na kampuni ya LX Consortium ya korea iliyotoa mafunzo hayo kwa njia ya mtandao.

Utekelezaji wa mradi huo mkubwa unakuja kufuatia kusainiwa hivi kwa karibuni kwa hati ya makubaliano kati ya Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Tanzania Dkt Angeline Mabula na yule wa Ardhi, Miundombinu na Usafirishaji wa Korea Kusini Bw. Won Hee-ryong katika mji wa Seoul Korea Kusini kipitia hati ya makubaliano (MOU) ya ushirikiano kwenye sekta ya ardhi na menejimenti ya taarifa za kijiografia.

Makubaliano ya nchi hizo mbili yanalenga kuweka mazingira rafiki kwa watanzania kupata utaalam na uzoefu kwenye nyanja za upimaji na ramani kupitia mipango/miradi ya mafunzo ya kuendeleza rasilimali watu kwa maendeleo endelevu ya sekta ya ardhi, ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa fursa zaidi kwa watanzania kupata mafunzo ya muda mrefu nchini Korea.
Wajumbe wa Manajementi ya Wizara ya Ardhi wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kukamilisha zoezi la kubadilishana hati ya makubaliano kuhusu mradi wa ujenzi wa Kituo cha Taarifa za Kijiografia na Matumizi ya Ardhi kati ya Wizara na Ujumbe kutoka Korea kusini mapema leo jijini Dodoma.

Aidha kuanza kwa utekelezaji wa mradi huu kutaimarisha ushikiano uliopo kati ya Wizara ya Ardhi ya Tanzania na ile ya Korea Kusini katika kukuza matumizi ya teknolojia za kisasa kwenye sekta ya ardhi ili kuboresha utoaji huduma katika fani zote za utawala wa ardhi na kutimiza azma ya Serikali ya kusajili ardhi yote nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news