NA FRESHA KINASA
HALMASHAURI ya Wilaya ya Musoma mkoani Mara kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la Victoria Farming and Fishing Organization (VIFAFIO) lililopo Musoma mkoani Mara wamezindua Mwongozo wa Taifa wa Dawati la Ulinzi na Usalama wa Mtoto ndani na nje ya shule katika shule ya Sekondari Kasoma na Shule ya Msingi Seka zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Musoma mkoani Mara.
Uzinduzi huo umefanyika Novemba 4, 2022 katika shule hizo kwa kuzingatia muundo wake wakiwemo walimu wawili wa malezi na unasihi upande wa Kasoma Sekondari ambao wataratibu na kusimamia dawati hilo na wajumbe ambao ni wanafunzi 11 vinara ambao wamechaguliwa kwa kuzingatia jinsi na mjumbe mmoja kutoka bodi ya shule.
Huku upande wa Shule ya Msingi Seka wakichaguliwa wanafunzi 15 kwa mujibu wa mwongozo huo, walimu walezi wawili na unasihi,wanafunzi wenye ulemavu wawili, pamoja na mwakilishi mmoja kutoka kamati ya shule ya msingi Seka ambao watajumuika kuunda dawati hilo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Mratibu wa Shirika la VIFAFIO, Robinson Wangaso amesema kuwa, mwongozo huo umezinduliwa na Serikali hivi karibuni lengo kuu ukiwa ni kuweka mfumo wa ulinzi na usalama wa mtoto dhidi ya vitendo vya ukatili shuleni na katika jamii.
Wangaso ameongeza kuwa, malengo mahususi mengine ni kuweka utaratibu rafiki kwa watoto kutoa taarifa za vitendo vya ukatili shuleni, kuweka utaratibu wa kushughulikia masuala ya ukatili unaofanyika ndani na nje ya shule, kuimarisha huduma za ushauri nasaha na unasihi kwa watoto zitolewazo shuleni.
Amebainisha kuwa, Dawati la Ulinzi na Usalama wa mtoto katika kila shule ya msingi na sekondari litakuwa ni jukwaa la watoto kujadili, kupeana taarifa za kujilinda dhidi ya vitendo vya ukatili, na namna ya kutoa taarifa za ukatili ili ziweze kushughulikiwa na walimu na walezi kupitia rufaa. Kwani linaratibiwa kuanzia kila kijiji/ mtaa kupitia mfumo uliowekwa na MTAKUWWA.
"Umuhimu wa Mwongozo huu ni kuimarisha mfumo wa kuzuia matukio ya ukatili yasitokee shuleni kama ilivyoainishwa kwenye MTAKUWWA, kushirikiana na wadau mbalimbali, wananchi, viongozi wa dini, vyombo vya ulinzi katika kuimarisha ulinzi na usalama wa mtoto, kuweka na kuimarisha mifumo ya ulinzi wa mtoto shuleni na nje ya shule,"amesema Wangaso.
Tafuteni Kihoo ni Mwalimu wa Malezi wa Dawati hilo amelishukuru Sshirika la VIFAFIO na Serikali kwa kuleta mwongozo huo ambapo amesema utakuwa dira na chachu ya kuimarisha mapambano ya vitendo vya ukatili shuleni hapo, ili kuhakikisha wanafunzi wanaondokana na vitendo vya ukatili.
Samwelly Daud ni mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Seka ambapo amesema kwamba kupitia mwongozo huo atajifunza mambo mengi yatakayo msaidia kutoa elimu kwa wenzake juu ya madhara ya vitendo vya ukatili na sehemu sahihi za kuripoti matukio ya ukatili.