NA DIRAMAKINI
WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) umeeleza kwamba, unatarajia kuvuka lengo la asilimia 85 la kutoa huduma ya maji vijijini ifikapo mwaka 2025, kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mhandisi Clement Kivegalo, Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA alitoa kauli hiyo alipokutana na wahariri wa vyombo vya habari nchini tarehe 1 Novemba 2022, wakati akizungumzia mwelekeo na changamoto za taasisi hiyo.
Alisema, kutokana na umuhimu wa kazi ambazo zinafanywa na RUWASA, serikali iliongeza uwezeshaji rasilimali fedha ili kuongeza kasi ya kuwapatia wananchi waishio vijijini huduma endelevu ya maji safi na salama.
Hadi Julai 2019 upatikanaji huduma ya maji vijijini ulikuwa asilimia 64.8, pamoja na kiwango hicho hali ya huduma ya maji vijijini haikuwa ya kuridhisha.
‘‘Baadhi ujenzi wa miradi ya maji ilichukua muda mrefu ambapo miradi iliyokuwa ikikamilika, kuzinduliwa, ilidumu muda mfupi na kusababisha wananchi wa vijijini kupata adha ya maji.
“Miradi hiyo ilikuwa ikijengwa kwa gharama kubwa ikilinganishwa na uhalisia,” aliongeza. Kwa sasa, kati ya vijiji vyote nchini 12,319, vijiji 9,029 tayari vimefikiwa na huduma ya maji safi na salama.