Mwenyekiti wa Chama cha ADC Taifa aibua mambo 12

NA GODFREY NNKO

CHAMA cha Alliance for Demecratic Change (ADC) kimewataka viongozi wote nchini kufanya kazi kwa bidii ili kuyatimiza maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi ya kuwaletea maendeleo Watanzania.
Hayo yamesemwa Novemba 22, 2022 na Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa, Mheshimiwa Hamad Rashid Mohamed wakati akifungua Mkutano wa Bodi ya Uongozi Taifa wa chama hicho uliofanyika jijini Dar es Salaam

Ufumbuzi

"Ufumbuzi wa matatizo upo,ndio jambo la msingi. Tunamuomba sana Mheshimiwa Rais na tunashukuru sana kwa juhudi zake.Lakini mkono mmoja haulambwi, tunahitaji viongozi wote tushirikiane kuhakikisha matatizo ya watanzania yanakwisha. Viongozi wetu wakuu wameonesha juhudi kubwa,"amesema.
Pia Alliance for Demecratic Change (ADC) kimeipongeza Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuhakikisha zinadhibiti mfumuko wa bei ya mafuta hususani petroli na dizeli ambayo kama yangeendelea kuuzwa kulingana na soko la dunia maumivu yangekuwa makubwa.

Umeme

"Na tunashukuru juhudi zilizochukuliwa kwa ajili ya kupatikana kwa umeme, lakini kwa bahati mbaya sana umeme bado ni tatizo, tumewasikia juzi TANESCO wakitoa maelezo wakasema wanahitaji miezi walau 36 kuhakikisha tatizo la umeme linamalizika tunawashukuru sana kwa mpango wao, lakini inaelekea sasa wameanza kufanya utaratibu mzima wa kukusanya mapato.

"Lakini wanapata ushauri mbalimbali wa kuwekeza katika umeme, lakini hawazingatii mfano kila mkoa ukiweza kuwa na megawati 30 za umeme wa jua ama upepo ni dhahiri kabisa umeme wa Gridi Kuu ya Taifa ungeweza kupata nafuu ukapelekwa viwandani.

"Wapo wawekezaji kadhaa akiwemo kutoka Ujerumani na wengineo wako tayari waweke angalau megawati 30 za umeme wa jua katika mikoa isiyopungua mitano, hawajibiwi hata barua yao pamoja na kusukuma kwa Waziri hakuna anayejibu.Fedha yao,teknolojia yao na kila kitu chao, lakini bado tunalalamika kuna tatizo.
"Tunawaomba sana TANESCO fungueni dawati, ADC inawaomba, dawati ambalo litahudumia watu watakaozalisha umeme. Hali hiyo hiyo Zanzibar tumewapelekea mapendekezo ya kutumia takataka kuzalisha umeme majibu hayapatikani.

"Kwa hiyo Serikali hairespond kwa juhudi zinazofanywa na Rais wetu, kwa kusema waje wawekeze. Lakini kwa ndani huku ukiritimba bado ni mkubwa mno, wawekezaji hao kupata fursa ya kuitumia ili watanzania waondokane na shida walizo nazo.

Mfumuko

"Tunaishukuru serikali kwa kujitahidi kuchukua hatua mbalimbali kudhibiti mfumko wa bei, moja kupunguza bei ya mafuta ambayo ndio chanzo kikubwa sana cha kuongeza bei katika nchi.

"Mafuta yalitoka shilingi 3,900. Mpaka sasa ni shilingi 2,900 kwa lita. Lakini mfumuko wa bei bado upo mchele ulikuwa 1, 900 hadi sasa ni shilingi 3,400 kw akilo.

"Tena mchele wa ndani, debe la unga shilingi 36,000, sasa ukiona bado bei ya mafuta haijapanda unauliza mfumuko wa bei uko wapi vipo nyanzo vidogo vidogo,lakini chanzo kikubwa ni hicho. Lipo tatizo ambalo halijawa addressed properly na Serikali.
"Nimefuatilia sana hotuba ya Waziri wa Fedha nakubaliana naye kabisa, ulimwenguni kumeharibika, Waingereza mfumuko upo asilimia nane, Wafaransa asilimia sita, Wajerumani asilimia nane, nakadhalika lakini matatizo yao yanaeleweka ni nishati na chakula kutoka Ukraine, lakini sisi hatuna shida hiyo.

"Serikali imejitahidi kuweka bei ya mafuta nzuri na kodi wamejitahidi kuzirekebisha, lakini bado bei ya chakula ni kubwa kuna nini? ADC tunaomba sana Benki Kuu ya Tanzania ambayo ni mahususi kabisa kwa kuraribu masuala mazima ya fedha, masuala ya kodi, masuala ya riba na mikopo wahakikishe kabisa bei ya chakula inalingana pale tulipotoka shilingi 1,900 ya kilo ya mchele.

"Leo ni kilo ya mchele ni shilingi 3,400 kwa kilo. Tunarudi katika umaskini wa hali ya juu sana, juhudi za Rais zinakuwa hazionekani. Tunaiomba Serikali suala la mfumuko wa bei ya vyakula ni la kufa na kupona wakae kitako wakitaka msasa, ADC sisi tupo tayari kuwasaidia."amesema Mheshimiwa Rashid.

Kilimo

"Mbali na hayo Serikali imetoa ruzuku ya mbolea, hilo ni jambo nzuri sana, cha msingi ni kuhakikisha ruzuku hii inafika kwa wakulima wenyewe japo tumeona kuna wajanja wanaificha hiyo mbolea waiuze kwa bei za mitaani.
"Wahakikishe mbolea inawafikia wakulima wenyewe, tunamshukuru sana na tumemuona Waziri Bashe anajitahidi, lakini viongozi wa mikoa na wilaya wanafanya nini? Viongozi wa tarafa na kata wanafanya nini?.

"Na hili ni eneo ambalo bado Serikali haijaunganisha nguvu zake baina ya TAMISEMI na Wizara ya Kilimo.Kuna wafanyakazi wengi wa TAMISEMI wangeweza kabisa kushiriki programu za kilimo na hali ya wananchi ikabadilika wanaachiwa maafisa wa kilimo peke yao, ADC tunaomba TAMISEMI na Wizara ya Kilimo wakae pamoja ili zile fursa zinazotolewa na Serikali ziwafikie wakulima kwa wakati na kwa bei rahisi,"amesema Mheshimiwa Rashid.

Demokrasia

"Tunamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi kwa pamoja wote kushirikiana na wadau wa siasa na hatimaye wakaunda vikosi kazi ambavyo vimetoa taarifa zake na taarifa hizo kwa maelezo ya viongozi wetu zitafanyiwa kazi.
"Tunaomba sana suala la mikutano ya hadhara liruhusiwe mapema iwekanavyo, hakuna sababu yoyote ya msingi, katiba iko wazi, sheria iko wazi, lakini mikutano ya hadhara ndio uhai wa vyama vya siasa hatuwezi kuuza sera zetu nzuri, kukutana na wananchi ambao bado hawajatuunga mkono mpaka watakapotusikia. Naomba sana Serikali iruhusu mikutano ya hadhara mapema iwezekavyo ili vyama vya siasa viweze kufanya kazi yake.

Tume

Wakati huo huo, Mheshimiwa Rashid amesema, "Tunaziomba taasisi nyingine hasa tume za uchaguzi wanapofanya mabadikiko ya sheria ya uchaguzi wakavitenga nje vyama siasa, wajue vinawatenga wadau wa siasa hizo na sheria zitakuwa hazina msingi wowote.

"Hivi sasa tume inapitisha wataalam wake ili kuangalia sheria ya uchaguzi, lakini hawavishirikishi vyama vya siasa hilo ni kosa, hiwezi kutunga sheria kama mdau mkubwa wa sheria hiyo haujamshirikisha, kanuni za bunge zinakataa kabisa zinasema lazima mswada wowote wa sheria unaokwenda bungeni uwe umewashirikisha wadau wakuu wa sheria hiyo. Hili ADC hatuko radhi nalo, tunalikemea na tulikataa wala sio suala la kubembeleza ni haki.

"Tunamuomba Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi na Mkurugenzi wake wahakikishe ushiriki wa vyama vya siasa katika marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa unazingatiwa,"amesema.

Amani

"Nakipongeza sana ADC, chama chetu kwa kuamini uwepo wa Mwenyezi Mungu ametuambia tuishi kwa amani, upendo kwa kusaidia na kuleana ADC tumelitekeleza hilo, kwenye amani watu wanaweza kusaidiana, kupendana na kuheshimiana.

"Tunahitaji kuheshimu katiba na sheria za nchi tulitonayo, na kuheshimu huku iwe kwetu sote tunaokula viapo, tunaosimamia utekelezaji katiba hiyo na sisi raia ambao katiba ndio msingi wa maendeleo,"amesema.
"Rais amepiga mstari amesema kwamba kama tuliua tukalaumia akasema yaishe tunajenga Tanzania moja na hakuna mwenye hati miliki ya Tanzania ila Watanzania wenyewe nataka nikupongeze sana Mheshimiwa Rais.

"Mmesikia vita vya Ukraine na watu wakawa na mashaka nyukilia itatumika. Nyukilia ni maji, chakula na nishati sio nyukilia mzinga maana njaa inaua kuliko mzinga wenyewe, kwa hiyo vitu vitatu hivi ndio nyukilia.

"Ndio maana Europe mkaona ikahangaika...Watanzania hatuna sababu lazima tuzalishe chakula cha kutosha tunamuomba Mheshimiwa Rais wote tusipuuze suala la kilimo ni muhimu sana, tunaziona juhudi zinazofanyika,"amesema

Miti

"Basi kwetu tuanzishe, hivi kila shule ikiwa na migomba mitano, miembe mitano, mipapai mitano baada ya miaka mitano wanafunzi watakuwa na njaa?.

"Serikali juzi imezindua programu nzuri sana ya kupanda miti kwenye vyanzo vya maji, ADC mapema aana tuliliona tukasena kwamba kila Mtanzania mwenye umri angalau miaka 15 apande walau mti mmoja tungekuwa na miti mingapi kwa sasa miti isiyopungua milioni 30.

"Kwa hiyo tunatoa tangazo tena Serikali imetoa programu nzuri kwa kupanda miti kwenye vyanzo vya maji, na sisi tunasema tuandae miti kila mahala panapo stahili uwe wa chakula uwe wa biashara, matunda, tupandeni miti kuna nchi asilimia 75 yenyewe imepanda miti watu wanakwenda wanafanya utalii wa miti kwetu kule Pemba kuna msitu unaitwa Ngezi watalii hata wa Kiitaliano walikuwa wanakuja pale kumbe kuna miti ambayo ina dawa kwingine haipatikani unaweza kuwa na almasi mfukoni ukadhani unajiwe.

Sheria kali

"Arabuni kukata mti au tawi la mti adhabu yake ni kali kweli kweli, tunahitaji kuwa na sheria kali Arabuni kukata mti au tawi la mti ni bora umuue mtu, adhabu yake ni kali kweli tatizo hili la kukosa mvua, joto ni kwa sababu mazingira hatukuyatunza vizuri.
Heshima kubwa ni kutunza miti yetu pale kisiwani Pemba tulikuwa na mikarafuu isiyopungu milioni 2.5 nenda kaangalie sasa...haipo joto limeongezeka sana mahala ambapo palikuwa na baridi ya aina yake.

"Suala la miti ADC inaiomba Serikali tupitishe sheria kali sana kwa mtu anayekata miti...ukikata mti maana yake unapoteza uhai wa mtu, tunaiomba Serikali iunge mkono suala hili ili iwasaidie wananchi na vijana wetu kwa kuongeza kasi katika shule, taasisi kwa kupanda miti hasa ya matunda,"amesema.

Bima

"Tunaishukuru Serikali kwa kuanzisha sera ya afya ya kuwa na bima ya afya kwa wote, ninaomba kuishauri serikali. Bima ya afya itafanya kazi kama vituo vya afya vitakuwa na watendaji, vifaa tiba pamoja na dawa. Bahati nzuri nimekaa Wizara ya Afya...dawa unanunua hazifiki kwa walengwa, mpaka naondoka wizarani upatikanaji wa dawa ulikuwa asilimia 94, lakini vifaa tiba ni tatizo.

"Kwa hiyo ushauri wangu kwa serikali badala ya kutuuzia vifaa tununue huduma kweli kwa sababu wao kila mwaka wanabadili teknolojia inabidi wewe ukanunue kingine kwa serikali zetu maskini hizi utanunua MRI ngapi CT scan ngapi, utanunua X-ray ngapi.

"Bima hii ambayo tunataka kuitangaza ama shirika la bima litacollapse ama huduma kuharibika ama hakuna watu wa kufanya kazi, ama watu watakuwa wana bima, lakini hawapati huduma. Tunaomba sana Serikali mzingatie sana suala la vifaa tiba kuingia mikataba na wazalishaji wa vifaa hivyo,"amesema Mheshimiwa Rashid.

Dagaa

Akizungumzia kuhusu dagaa wa Zanzibar ambao wanatajwa kuwa na soko kubwa nchini Kongo, Mheshimiwa Rashid anasema, "kilo moja ya dagaa ni dola nane,Wakongo walichokifanya wale wanunuzi wa dagaa wametoka Kongo wamekuja Zanzibar na Tanzania kwa ujumla wao wamefanya uwekezaji, vijana wetu wakawa ni manamba wafanyakazi wao, wanazalisha, wanachukua, wanasafirisha wanakwenda kuuza kwao hizo dola nane hazipatikani kwetu.

"Kama kuna eneo ambalo tunapoteza ajira,teknolojia haitumiki vizuri,rasimali za watu hazitumiki vizuri tunapoteza vijana wetu ajira ambayo haina sababu ya kupotea kwenda Kongo.

"Tumezungumza na Balozi aliyeko Zaire amesema wavue waje mpakani pale wafungue maduka yao sio waje humu ndani,"amesema.

Maji

"ADC tulizungumzia suala la maji ambalo ni kero, ukichukulia Bara la Afrika, Tanzania ina asilimia 6.2 ya idadi ya maji yaliyoko Afrika tumeeleza kwenye ilani yetu 2015. Inasikitisha sana tunazungumzia mvua, Mwenyezi Mungu anatupa mvua maji yanayotoka kwenye mito, milimani yanayokwenda baharini yanatisha ingelikuwa wanatekeleza Sera ya ADC ya kuhakikisha tunavuna maji ya mvua tusingelikuwa na shida.

"Ukitaka mfano nenda Dodoma kwenye Wizara ya Maji wana tenki la lita 100,000 la maji ya mvua, hilo lingefanyika shida ya maji isingekuwepo...

"Lakini wenzetu Waisraeli wameenda mbali zaidi wanateka maji kutokana na hewa unaweka mashine ya lita 20 yanavuta maji safi sana, hatufanyi na tumeleta hizo teknolojia nchini.

"Mbaya zaidi kuna visima ambavyo vimechimbwa na Serikali kwa kutumia mikopo ya World Bank, IMF na taasisi zingine,lakini visima hivi baadhi yake wanasema vina chumvi na madini vimetelekezwa havifanyi kazi. Teknolojia ya kusafisha maji hayo ipo, mwaka 2014 mimi mwenyewe nilileta mashine kutoka Marekani, Amos Makalla alikuwa Naibu Waziri wa Maji, mashine hiyo tulipoikita kwenye mto Msimbazi maji yaliyopimwa pale na watu wa maji yalikuwa safi kuliko maji ya kunywa ya chupa, mashine hiyo inatumia upepo, jua na umeme wa kawaida gharama yake ni ndogo. Sasa hivi zimeteremka bei kule Marekani.
"Kutokana na crisis hii nikawaambia Serikali kuna teknolojia hii. Kuna visima vingi vimechimbwa vimefukiwa na maji yapo yana chumvi na madini nunueni hizi mashine na wenye mashine wanasema kwamba mkinunua 10 wapo tayari kujenga kiwanda cha kuzalisha mashine hapa Tanzania, lakini Serikali haijibu hata barua jambo ambalo linasikitisha sana," amesema Mheshimiwa Hamad.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news