Nabii Dkt.Joshua afichua siri ya maji yenye nguvu za kipekee Morogoro

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Umoja wa Mitume na Manabii Tanzania ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania, Nabii Dkt.Joshua Aram Mwantyala amesema, moja wapo ya mambo ambayo yeye mwenyewe yanaendelea kumfanya aendelee kumtukuza Mungu kwa bidii katika maisha yake ni pamoja na kumpa mafunuo ya maji ya uponyaji ambayo yanapatikana eneo moja tu nchini.
Ni maji ya uponyaji ambayo baada ya ufunuo kutoka kwa Mungu aliwapeleka wataalamu kwenda kuyachimba katika Mlima wa Mungu kwa Nabii Joshua uliopo Kata ya Mkundi eneo la Lug'wawa Wilaya ya Morogoro Mjini mkoani Morogoro.

Maji yenyewe

"Hapa kwetu Morogoro, Mungu alinionesha Mlima wa Maombi, niliununua miaka saba iliyopita, nilichukua hatua ya kufanya maombi kwenye huo mlima na watu wengi wameshiriki kwenye huo mlima kufanya maombi hapo mlimani.

"Hatukujua jambo lililopo kwenye huo mlima kwa sababu wakati fulani Yakobo alilala mahali fulani usiku akaona malaika wanapishana wakipanda na kushuka Mbinguni akasema mahali hapa pana Mungu.
"Wala mimi sikujua, nilikuwa sijui ila Mungu aliniotesha akasema katika mlima huu yatatoka maji na maji haya hatapatikana eneo lolote duniani, baada ya ndoto hiyo nikatafuta wataalam wakapima maji, tukalipia gharama tukachimba maji kutoka kwenye mlima yakapatikana na yalipotoka tukayagawa kwa watu wanakunywa na kwenye maeneo yao wamefanikiwa sana;

Kiongozi huyo Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania, Nabii Dkt.Joshua Aram Mwantyala ameyasema hayo katika mahojiano na DIRAMAKINI mjini humo.

Yana nguvu

"Utaziona shuhuda wapo watu waliokuwa mabubu wanaongea, wengine walikuwa na UKIMWI wamekunywa wamepima wamepona, walitengwa na ndugu zao wamekaribishwa, biashara zao zilikuwa mbaya sasa wamefanikiwa, tukaona ni jambo jema kuiambia Dunia kuwa, Mungu ametoa njia mahali pasipokuwa na njia, wewe uje upokee uponyaji kwa njia hiyo.
"Kuanzia tarehe 5 hadi 6, Februari mwaka 2023,tutakuwa na kongamano kubwa juu ya Mlima wa Mungu na kila mtu atajichotea maji kutoka kwenye mlima huu, maji yanabubujika kutoka kwemye mlima huu si kawaida.

"Jambo ambalo hutakiwi kusahau mwambie jirani yako haya maji hayauzwi. Yanatolewa bure kwa kila mtu imani ni kitu kikubwa sana, ukiamini halafu ukabaki nayo nyumbani haifanyi kitu chochote.

"Cha ajabu imani inapaswa ikutane na Neno la Mungu kitabu cha Waebrania 11: 38 kinasema, mwenye haki ataishi kwa imani. Huwezi kufanikiwa kuishi kwa imani bila kuwa na haki ya kuishi, kwa hiyo imani na haki ya imani ni Neno la Mungu linachosema kile unachoamini sababu chanzo cha imani ni neno la Kristo.
"Huyo Akida aliamini na alikuwa na anajua tayari mgonjwa wake atapona kwa imani, lakini mgonjwa hakupona mpaka alipopewa haki ya kuishi kwa hiyo imani. Yesu alimwambia yu-mzima alipomwambia imani ile ikapewa haki ya kudhihirisha alichoamini naamini haki.

Ni bure

"Narudia tena, maji yanatolewa bure, kwa wageni wote watakaokuja. Chakula kitatolewa bure kuanzia Jumamosi ya terehe 5 hadi 6 mahali pa kulala ni bure pia. Sasa Mungu akupe nini, natangaza baraka za Mungu juu yako ambazo hakuna mtu yeyote atakayezuia.

"Mwaka huu ni mwaka wa kibali chako, chukua hatua uje upokee uponyaji,kuna mtu mmoja anajiuliza kwamba mbona nazungumza juu ya maji na si kuhusu Yesu.
"Swali hili wanajiuliza watu wengi walioko kwenye dini zao lisikilize Neno la Mungu imeandikwa fanyeni yote kwa jina la Yesu Kristo. Kwa tendo au kwa Neno hakikisheni mnafanya kwa jina la Yesu.

"Tunatoa maji haya kwa jina la Yesu, mnafahamu tunaposema kwa jina la Yesu tunamaana kwa kibali cha Yesu. Maneno haya uyaweke ndani ya moyo wako, kuna mtu anajiuliza leo tunaamini maji au Mungu. Musa aligawa bahari ya Shamu alileta maji jangwani kwa fimbo, je? Tunaamini fimbo ya Musa au Mungu aliyemwambia apige maji. Naamani aliponywa ukoma kwa maji ya mto Jordani au Mungu?.

"Yesu alimponya kipofu kwa kupaka matope machoni, je? Tunayaamini matope au yeye aliyefanya jambo hili. Kina Paul, Petro mitume wa nyakati za kale kanisa la kwanza ambao ndio Baba zetu wa imani walitumia makoti, nguo, vitambaa vivuli waliponya wagonjwa.

"Je, tunaweza kuamini mavazi yao ama Mungu kwa nini leo watake kuamini tofauti na Mungu aliye juu, aliyeruhusu kutumia maji ndie anayeponya watu maji ni mali yake. Mimi ni mali yake, wewe ni mali yake Jehova Mwana wa Mungu.

Njia za Mungu

"Mungu ametoa njia baada ya njia zako zote kukwama. Sasa njoo uchukue uponyaji, njoo uchukue baraka zako kila ulichotamani kumiliki kwenye maisha yako njoo uchukue maji yanatolewa bure Morogoro Mjini kwa Nabii Joshua.
"Kitabu cha Amosi 5:7, imeandikwa hakuna Bwana Mungu hatafanya neno lolote asiwapowafunulia...manabii siri yake, inaonesha halitokei jambo la Kiungu kabla mtu fulani hajafunuliwa siri namna gani litakwenda kutokea.

"Sababu hiyo, tunaona siri nyingi zilifunuliwa kwa watu wake na utukufu wake ukaifunika Dunia wakati wana wa Israeli walipokuwa wanatafuta kutoka kwenye mikono ya Farao mtesi wao wa zaidi ya ya miaka 400, Musa alifunuliwa.

"Kubwaga fimbo yake chini ikawa nyoka ikameza nyoka zote za wachawi na waganga wa Farao. Halikuwezekana jambo hili kwenye mioyo ya wenye akili wa Dunia hii. Isipokuwa yeye Mungu aliliweka ndani ya watumishi wake.

"Sayansi isingejua jambo hili, lakini Mungu alikuwa amefahamu nini kitatokea kikaiaibisha hekima ya Dunia. Wakati mwingine pia katika mji wa Shunemu, iliyokuwa sehemu ya wana wa Isakari palikuwa na mwanamke mmoja mwenye cheo aliyekuwa akimkazania nabii kula kwake kila alipopita.
"Hata hivyo mwanamke yule akawiwa kufanya ziada. Akawa na shauku ya kumhudumia mtumishi wa Mungu vizuri. Akapendekeza kwa mumewe wamjengee Elisha chumba na kukiwekea mahitaji yote muhimu kwa mgeni muhimu. Nao wakafanya hivyo.

"Siku moja Elisha akiwa katika chumba hicho alimtuma Gehazi kumwuliza ni jambo gani mama huyo angehitaji kufanyiwa hata ikiwa ni jambo la kuhitaji kuonana na mfalme au mkuu wa majeshi, kwa fadhili ambazo amekuwa akiwatendea.

"Hata hivyo, mama huyo alijibu kuwa alikuwa na maisha ya raha na furaha tu katikati ya jamii ya watu wake naye hakuwa na hitaji la fursa nyingine yoyote kutoka kwa wenye mamlaka.

"Elisha akamwomba Gehazi mtumishi wake mawazo ya jambo ambalo wangeweza kumfanyia mama huyo. Gehazi kwa muda waliokuwa hapo aling’amua kuwa familia hiyo ingawa ilikuwa na uwezo mzuri kiuchumi, mume alikuwa ni mzee na familia haikuwa na mtoto na hivyo kukosa mrithi.

"Wazo hilo likawa jema mbele ya nabii, akamwita mwanamke yule na kumwahidi mtoto msimu kama huo mwaka uliofuata. Nayo ikawa hivyo. Kwa kumhudumia nabii, familia hiyo ikapata baraka za kinabii.

"Siku moja mtoto akiwa na baba yake shambani aliumwa ghafla, akarudishwa nyumbani lakini baada ya muda alifariki. Mama yule akajikaza wala asilie, akamlaza mtoto kwenye kitanda cha Elisha.

"Akamuaga mumewe kwenda kwa Elisha asimwambie habari za msiba. Mumewe akashangaa kwa nini alikuwa akienda kwa nabii siku hiyo ambayo haikuwa mwandamo wa mwezi wala Sabato, siku ambazo zilitumiwa na watumishi wa Mungu kufundisha watu torati na maneno ya Mungu, pamoja na hayo hakumzuia.

"Alipofika kwa Elisha na kumweleza Elisha alimtuma Gehazi na fimbo ya kinabii kwenda kumponya mtoto. Lakini pamoja na hayo mwanamke yule hakukubali kuondoka pale bila Elisha, Elisha ikabidi atii hitaji la mama huyo.
"Walipofika kwa mtoto walikuta jitihada za Gehazi zilikuwa hazijafanikiwa bado. Elisha kwa maombi akajinyosha juu ya mtoto yule mara mbili, hatimaye mtoto akafufuka na kurudisha furaha katika mji huo.

"Elisha pia alitenda miujiza mingine miwili ya kulisha watu. Katika muujiza wa kwanza wana wa manabii katika kipindi cha njaa waliandaa chakula cha mboga mwitu.

"Lakini bahati mbaya katika kuchuma wakachuma na mboga yenye sumu ikapikwa pamoja na mboga nzuri. Wakati wa kula wana wa manabii wakasikia ladha hiyo ya mboga yenye sumu na kulia “...ee mtu wa Mungu...” Elisha akatupia unga sufuriani akawa ameponya chakula na watu wakaendelea kula.
"Pia wakati mwingine tena mcha Mungu mwingine alipeleka chakula cha malimbuko kwa wana wa manabii, mikate 20 na masuke ya ngano.

"Katika torati malimbuko yalikuwa ni sehemu ya Walawi na makuhani, lakini kwa kuwa katika Israeli Walawi na makuhani walikimbia kwenda Yerusalemu baada ya Yeroboamu kuanzisha ibada ya ndama na kuweka watu wengine kuwa makuhani, kutimiza takwa hilo kama lilivyohitajika kwa sheria ikawa ni ngumu.

"Hata hivyo, palikuwepo na watu wa Mungu waliomwabudu Mungu katika roho na kweli na kwao hakukuwa na udhuru wa kuonesha shukrani kwa Bwana wao. Kwa kukosekana walawi watu hao walipeleka sadaka zao hizo kwenye nyumba za wana wa manabii.

"Ingawa sadaka hiyo likuwa ni ndogo kulingana na wingi wa wahitaji, nabii wa Bwana akaibariki sadaka hiyo ikaliwa, ikatosha na kusazwa. Kama ilivyobarikiwa sadaka hiyo, baraka za Bwana zikaambatana na mtoaji pia.

"Hii ilikuwa njia ya Mungu, ndio maana imeandikwa kwamba njia za Mungu si kama njia za wanadamu. Njia za Dunia zinaposhindwa Mungu hutumia njia zake kupitia manabii ili kufikisha msaada kwa watu wake waliolemewa sana.

"Kipo kisa cha Elisha alipokutana na jemedari wa jeshi alipokutana na Naamani alikuwa na ukoma na kwa sababu ya ukubwa wa cheo alichokuwa nacho aliweza kutafuta msaada wa Dunia yote ya kale hakupata matibabu.

"Walikwama waganga...walishindwa, wafalme hawakuweza, lakini binti mmoja tu mjakazi akamwambia mke wa Naamani laiti Bwana wangu angekuwa pamoja na mtumishi wa Mungu Nabii Elisha angepona ukoma wake.

"Naamani alipopewa ushauri huo alikwenda kwa nabii, tazama kilichotokea Nabii wa Mungu alimwambia tu Naamani neno moja dogo sana, nenda ukajichovye kwenye maji ya mto Jordani mara saba nawe utapona.

"Naamani aliposikia habari hizi alishituka sana akasema mbona kwetu kuna mito mizuri je, nisingeweza kujichovya huko? Kwa nini niende Yordani mto ambao hauna sifa njema, maji yake ni ya namna gani haya yatakase ukoma wangu?.

"Lakini watumishi wake walimwambia, Nabii amefunuliwa fanya neno hilo dogo alilokwambia, Biblia inasema alikwenda akajichovya kama alivyoambiwa akapona kabisa ukoma wake.

Siri za Mungu

"Nazungumzia juu ya siri ambazo Mungu huzifunua, nazungumzia kuhusu uwezo Jehova katika maisha yako anaposema Mungu amfunulie mtu siri yake hilo tatizo ulilonalo kwa miaka mingi kuna mtu anajua utaponaje.
"Ni rahisi na unajua utaponaje, unajua uponyaji ni kama password, mtu akiweka namba ya siri kwenye simu yake wewe usiyejua utapambana hutoweza, lakini yeye ataweka namba kirahisi sana.

"Yupo mama mmoja niliwahi kumpokea kutoka Kigoma yeye alikuwa amepooza mgongo ulikuwa umevunjika. Hakuweza kusimama wala kutambaa miaka mingi, mwanamke huyo aliletwa eneo la mkutano alinipa ushuhuda wake.

"Alisema amekwenda kwa waganga wengi sana, baada ya kushindwa kupata matitabu kwenye hospitali aliamua kwenda kwa waganga wa kienyeji alisema mganga mmojawapo alisema tiba yeke aliamua kumpaka kinyesi mwili mzima.

"Mganga alimwambia mteja wake nitakupaka kinyesi changu kikiwa bado cha moto mwili wako wote na baada ya siku tatu utatembea. Alipakwa kinyesi mwili mzima na baada ya siku tatu hakupona, hali hii inaumiza sana.

"Nakumbuka mwanamke mmoja kwenye Biblia aliyekuwa anatokwa na damu nyingi, Biblia inasema aliteseka sana na matabibu. Na huyu mama wa Kigoma aliyekuja kwenye mkutano wetu nae alipitia mateso kupitia mikono ya matabibu.

"Alikuja kwenye mkutano ilikuwa njia rahisi sana, kama yule mama aliyegusa pindo la vazi ka Yesu akapata uzima naye huyu mama nilichukua maji nikamnyunyizia matone ya maji niliyoyaombea akasimama, akatembea akarukaruka. Mungu alikuwa anajua ameweka kitu ndani yangu jinsi gani huyo mama atapona alinifunulia.

"Nimekwambia jambo halitokei Kiungu kabla Mungu hajalifunua. Mambo ya Mungu ni mafunuo na matakatifu sana, hayajawekwa hadharani ila Mungu huchagua watu wachache ambao anaweza akawasemesha ili kusaidia watu wengine,"amefafanua kwa kina Rais wa Umoja wa Mitume na Manabii Tanzania ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania, Nabii Dkt.Joshua Aram Mwantyala katika mahojiano na DIRAMAKINI.

Shuhuda

"Nimezaliwa na udata (kushindwa kutoa ulimi nje au kunyanyua ulimi juu) kwa miaka zaidi ya 40, lakini baada ya kuanza kutumia haya maji kwa kuyanywa na kuyaoga mishipa yote iliyokuwa imesababisha nisiseme sasa imefunguka na ninaimba.

"Mjukuu wangu Zakia wa Chalinze pia amezaliwa na udata wakataka kumpeleka kwa mganga nikawaambia hapana, kuna maji uponyaji kwa Nabii Joshua haya maji ndio yamemfungua kwa kuyatumia, sasa hivi tunamtuma dukani kwenda kuchukua unga,"amesema Nkumbuka wa Chalinze.

Mtoa usuhuda mwingine ambaye akutaja jina lake anasema, "Mtoto wangu alikuwa na mapepo na majini kupitia mtumishi wa Mungu, Nabii Joshua amepona kabisa, ninamshukuru sana mtumishi wa Mungu, Nabii Joshua kwa kumfungua, nawakaribisha sana watu wote waje kwa Nabii Joshua kupokea suluhu ya matatizo yao. Mungu ambariki sana,"amesema.
Aidha, mwingine amesema, "Nilikiwa na fangasi isiyopona ndani ya miaka 15, nimeteseka nimemeza vidonge bila kupona baada ya kuja kwa Nabii Joshua na kugusa maji na kunawa mikono yangu, mikono yangu sasa imepona kabisa namshukuru Nabii Joahua, kwa kunifungua kwa jina la Yesu, niwaambia watu wote waje kwa Nabii Joshua.

"Mimi nilipelekwa Kola nikalala juu ya kaburi, niriporudi nyumbani sikupona nikaenda kuchukua maji kwa Nabii Joshua nikanywa kidogo nikaanguka, sikupata fahamu kwa baadae nikahisi kitu kinatembea mwilini mwangu na kwa sasa nimepona kabisa, mwanangu nilimnyonyesha mwaka mmoja tu nikaacha kutoka na kuumwa. Lakini sasa nimepona,"ameongeza mtoa shuhuda mwingine katika madhabau ya Sauti ya Uponyaji Tanzania yenye makao yake makuu mjini Morogoro.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news