NA FRESHA KINASA
MBUNGE wa Jimbo la Butiama mkoani Mara ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Jumanne Sagini amesema Watendaji wa Serikali wa Mkoa wa Mara wananafasi kubwa ya kuchangia maendeleo ya Mkoa huo kwa kiasi kikubwa iwapo watawajibika kikamilifu .
Amesema kuwa,utaalam walionao wanapaswa kuushusha ngazi za chini ikiwemo Halmashauri kusudi utalaam huo uweze kusaidia kuleta mageuzi chanya ya kimaendeleo kwa Wananchi katika kutatua changamoto zao za sekta mbalimbali.
Mheshimiwa Sagini ameyasema hayo Novemba 30, 2022 wakati akichangia katika kikao Cha kamati ya ushauri ya Mkoa wa Mara kilichofanyika katika ukumbi wa Uwekezaji uliopo ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo Mjini Musoma.
"Wataalam wetu wa Mkoa wa Mara mmepoa Sana, niwasihi muamke kwa kuwajibika, mfanye kazi za wananchi kwa bidii badala ya kukaa bila kishughulikia kero na changamoto walizonazo katika maeneo yao," amesema Mheshimiwa Sagini.
Ameongeza kuwa,utaalam walionao wakiushusha ngazi za chini na kufanya kazi kwa bidii kwa kutambua wajibu wao Mkoa wa Mara utapaa kiuchumi na Wananchi kupata Maendeleo thabiti.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mzee akifunga kikao hicho amewataka watendaji wa serikali mkoani Mara kujitathmini na kufanya kazi kwa weledi kumsaidi Mheshimiwa Rais Samia ambaye muda mwingi anawajibika kwa ajili ya kuleta maendeleo ya Watanzania.
Meja Jenerali Mzee amesema kuwa,Mkoa huo una changamoto mbalimbali ambazo zinapaswa kutatuliwa na Wataalam katika maeneo yao. Ambapo amesema, ushirikiano wa pamoja na uwajibikaji wa Kila kiongozi katika eneo lake utaleta tija kwa Wananchi wa Mkoa wa Mara.